Rais Samia azipa ‘tano’ Yanga, Simba CAF

Na Mwandishi Wetu

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezipongeza timu za Yanga na Simba ambazo zimeikiwa kukata tiketi ya kushiriki hatua ya makundi ya michuano ya CAF msimu wa 2024-25 huku akiahidi kuendelea kuziunga mkono katika ushiriki wao.

Jumamosi timu ya Yanga ilikuwa ya kwanza kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya CBE ya Ethiopia katika mchezo uliofanyika Uwanja wa New Aman Complex, Zanzibar.

Siku iliyofuata Simba nao iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Al Ahly Tripol ya Libya na kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Shirikisho Afrika.

Katika salamu zake, Rais Samia alisema ushindi wa Yanga na Simba ni burudani tosha kwa watanzania wengi wapenda soka na hivyo aliahidi kuendeleza hamasa zake katika michezo.

“Endeleeni kutupa burudani, hamasa yangu na dua za kheri toka kwa mamilioni ya Watanzania daima ziko pamoja nanyi,” alisema.

Katika kuhakikisha hamasa ya Rais Samia inaendelea kuziinua timu zinazoshiriki michuano ya kimataifa, hadi sasa Yanga tayari wamevuna shilingi milioni 85 kama zawadi ya ‘Goli la Mama’ huku Simba wakivuna shilingi milioni 15 na Azam ambao tayari wametoka wakiambulia shilingi milioni 5.

Wakati huo huo, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, amezipongeza Simba na Yanga kwa hatua waliyopiga katika michuano ya kimataifa msimu huu.

Aidha Karia amempongeza Rais Samia akimtaja kuwa ndio chachu ya mafanikio yote ya klabu zetu nchini zinazoshiriki michuano ya kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *