Na Badrudin Yahaya
BODI ya Ligi Kuu Tanzania Bara, imefanya maboresho ya ratiba ambapo sasa mchezo kati ya wenyeji Azam FC dhidi ya Simba umepangwa kuchezwa Septemba 26 kuanzia saa 12 jioni katika uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.
Katika ratiba ya awali, mchezo huo wa mzunguko wa nne haukuwa umepangiwa siku.
Azam FC kabla ya kukutana na Simba SC, Septemba italazimika kucheza mechi tatu ambapo Septemba 13 itacheza dhidi ya Pamba Jiji na kisha Septemba 19 itakuwa ugenini dhidi ya KMC na Septemba 22 watamaliza na Coastal Union.
Wakati Azam FC wakiwa na mechi za ligi, Simba wao watakuwa na kibarua chao cha mechi za mikondo miwili Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al-Ahli Tripol ya Libya.
Mbali na mabadiliko hayo, lakini pia Bodi ya Ligi imetangaza kuwa mchezo kati ya wenyeji Simba dhidi ya Yanga ambao awali ulipangwa kuchezwa katika dimba la KMC Complex, Dar es Salaam sasa utafanyika katika Uwanja wa Benjamini Mkapa, Oktoba 19.