Rekodi alizoweka Dabo miezi 12 Azam FC

Na Badrudin Yahaya

KOCHA Yusuph Dabo, ametimuliwa na uongozi wa Azam FC baada ya timu kuanza msimu wa 2024-25 kwa kusuasua kwenye michuano ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Licha ya Azam FC kuweka lengo la kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza lakini ndoto zao ziliishia njiani msimu huu baada ya kutolewa na APR ya Rwanda kwa kufungwa jumla ya mabao 2-1 baada ya mechi mbili.

Kutokana na uamuzi huo wa kumfuta kazi Kocha Dabo sambamba na wasaidizi wake, zifuatazo ni takwimu za Msenegal huyo ambaye alihudumu ndani ya Azam FC kwa takribani mwaka mmoja.

Ligi Kuu

Tangu amejiunga na Azam FC, Dabo ameisimamia timu katika mechi 31 za ligi ambapo hizo ni mchanganyiko wa msimu uliopita wa 2023-24 na msimu huu mpya ambapo tayari wamecheza mechi moja.

Katika mechi 30 za msimu uliopita, Azam FC walipata ushindi wa mechi 21 huku wakitoka sare mechi 6 na mechi walizofungwa ni 3. Matokeo hayo yaliwafanya kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo.

Msimu huu wa 2024-25, Azam FC wameshuka dimbani mara moja na kulazimishwa suluhu dhidi ya JKT Tanzania. Hiyo inamaana kuwa katika mechi 31 alizosimamia Dabo, timu imepata ushindi katika mechi 21, sare 6, na vichapo 3.

Michuano ya FA Cup

Akiwa Kocha wa Azam FC, Dabo msimu uliopita, aliiongoza timu hiyo kufika fainali ya michuano ya FA baada ya kushinda katika michezo minne, hata hivyo walijikuta wakipoteza mchezo mmoja kwa kufungwa na Yanga kwenye hatua ya fainali.

Kimataifa

Msimu uliopita, Azam FC walishiriki michuano ya Shirikisho Afrika ambapo hatua ya awali walipangwa dhidi ya Bahir Dar Kenema F.C ya Ethiopia. Licha ya Azam kushinda 2-1 mchezo wa kwanza nyumbani na wao walijikuta wakifungwa 2-1 ugenini na kisha kuondolewa kwa mikwaju ya penati.

Msimu huu, Azam FC walishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo walishinda bao 1-0 kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya APR na wakafungwa 2-0 ugenini na kutupwa nje.

Michuano mingine

Azam FC pia walishiriki michuano ya Ngao ya Jamii ambapo msimu uliopita walishika nafasi ya tatu baada ya kufungwa mchezo wa kwanza na Yanga na kisha wao kushinda mchezo dhidi ya Singida Big Stars ambao ulikuwa ni wakusaka mshindi wa tatu.

Msimu huu, walishiriki tena michuano hiyo na walimaliza nafasi ya pili baada ya kuifunga Coastal Union katika mchezo wa nusu fainali lakini wao wakafungwa na Yanga katika mchezo wa fainali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *