Na Mwandishi Wetu
KLABU za soka nchini za Simba SC, Yanga SC na Azam FC, zimekutanishwa kwa pamoja kwenye shindano la Kimataifa la kuhifadhi na kusoma Quran kwa wanawake, linalotajiwa kufanyika Jumamosi Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kuanzia asubuhi.
Shindano hilo lililoanzishwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), huku likitarajiwa kuanza mapema asubuhi, pia limemualika Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa mgeni rasmi wa shindano hilo litakaloshirikisha wanawake wa nchi 12 duniani.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema ni furaha kubwa kushiriki katika uhamasishaji wa shindano hilo litakaloshirikisha wanawake wa Tanzania, akiwemo Rais Samia, akiwa kama mgeni rasmi.
“Simba ni timu kubwa barani Afrika, hivyo kualikwa katika shindano hili kusema chochote sambamba na kualika wadau wa michezo wakiwemo wa Simba, ni jambo la kumshukuru Mungu, nikiamini Uwanja wa Taifa Jumamosi utajaa kwa sababu hakutakuwa na viingilio,” amesema Ally.
Kwa upande wa Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amewataka Watanzania wote wanaofuatilia michezo wakiwemo mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga kuitumia Jumamosi kama siku maalum ya kushuhudia neno la Mungu.
“Siku ya Jumamosi Yanga hatutakuwa na ratiba yoyote, hivyo wote wakiwepo wachezaji na viongozi wetu tutajaa katika Uwanja wa Taifa kushuhudia shindano hili lenye maana kubwa katika nchi yetu, ukizingatia kuwa Rais wa nchi, mama yetu Samia atakuwa mgeni rasmi,” amesema Kamwe.
Pia Ofisa Habari wa Azam FC, Hashimu Ibwe, amesema mpira wa miguu ni mchezo wa furaha, mazoezi na hauhusiani na uadui, ndio maana kwa pamoja wameunganishwa na BAKWATA katika kulisemea shindano la wanawake la kusoma na kuhifadhi Quran.
“Isingekuwa mchezo wa mpira tusingejumuishwa kwa pamoja na viongozi wa dini wakubwa kwa lengo la kufanikisha mashindano haya, ambapo nasi kama Azam tunafurahia kuwepo hapa sambamba na kuguswa na mgeni rasmi, Dkt. Samia siku ya Jumamosi,” amesema Ibwe.
Kwa mujibu wa BAKWATA, shindano hilo linatambua umuhimu wa michezo, hali iliyowalazimu kuwaalika wasemaji wa klabu hizo kubwa nchini kushiriki katika kuhamasisha wafuasi wao wahudhurie kwa wingi kwenye shindano hilo la Kimataifa.