Mashirika 2,000 kushiriki Jukwaa la NaCoNGO Dodoma

Na Zahoro Mlanzi

MASHIRIKA 2,000, yanatarajiwa kushiriki katika Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali litakalofanyika kuanzia Septemba 4 hadi 6, mwaka huu jijini Dodoma lenye lengo la kubadilishana uzoefu na kushirikishana changamoto ili kutengeneza mazingira wezeshi kwa mashirika hayo.

Jukwaa hilo limeandaliwa na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo, Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu chini ya Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa NaCoNGO, Jasper Makala, amesema jukwaa hilo hufanyika kila mwaka na kwa mwaka huu litakuwa ni la nne kufanyika ambalo litashirikisha wageni mbalimbali kutoka Tanzania Bara na wengine kutokea nchi jirani.

‘Tunatarajia ushiriki wa zaidi ya mashirika 2,000 katika jukwaa hili la mwaka, miongoni mwa nchi zilizothibitisha kushiriki ni Uganda, Zambia, Malawi na Ethiopia Pamoja na Balozi mbali mbali zilizopo nchini na mashirika ya kimataifa,” amesema Makala.

Amesema katika jukwaa hilo litakalofanyika kwa siku tatu kutakuwa na matukio mbalimbali yakiwemo maonesho ya kazi za mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na huduma mbalimbali.

Amesema pia kutakuwa na huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi, semina elekezi kwa wajumbe wa baraza hilo na wasajili wasaidizi, mikutano ya pembeni ya kujengeana uwezo na uzinduzi wa kampeni ya kutokomeza utapiamlo kwa watoto.

“Kauli mbiu ya jukwaa la mwaka huu ni “Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni wadau muhimu, washirikishwe katika kukuza utawala bora” na pia tunatarajia Naibu Waziri Mkuu, Dotto Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati kuwa mgeni rasmi wa jukwaa hilo,” amesema.

Ameongeza ili kufanya baraza liweze kufanya majukumu yake ipasavyo uongozi wa sasa umeanzisha mchakato wa kupitia kanuni zake za muhimu ambazo zitawezesha baraza kufanya majukumu yake kwa weledi zaidi.

 “Mapitio haya yanalenga kuja na mustakabali mzuri wa sekta ya NGOs nchini Tanzania na kwamba baraza limedhamiria kushirikiana zadi na Serikali ili kuboresha mazingira ambayo NGOs, Serikali na wadau wa maendeleo wanaweza kuboresha mashirikiano yenye tija na hatimaye kuwezesha jamii kunufaika na huduma zilizoimarishwa zinazotolewa na sekta ya NGOs,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *