Simba yaweka mnara 4G Mwenge

Na Asha Kigundula

TIMU ya Simba SC, imeendelea kuwa na mwanzo mzuri wa Ligi Kuu Bara baada ya kuitandika Fountain Gate FC mabao 4-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam.

Ushindi huo umeifanya Simba kushinda mechi mbili mfululizo za ligi hiyo na kukaa kileleni mwa msimamo ikiwa na alama 6 sawa na Singida Black Stars ila zinatofautiana kwa mabao huku Mashujaa FC ikifuata ikiwa na alama 4.

Katika mchezo huo, straika Steven Mukwala ambaye kwa muda mrefu amekuwa akihaha kucheka na nyavu, alifunga bao la pili dakika 44 huku Edwin Balua akitangulia kufunga kwa kichwa akiunganisha krosi ya Charles Jean Ahoua.

Mabao mengine ya Simba yalifungwa na MVP wa Ivory Coast, Ahoua kwa shuti kali nje ya eneo la hatari na la ushindi likifungwa na mtokea benchi, Valentino Mashaka aliyeingia badala ya Mukwala.

Hata hivyo Kipa wa Fountain Gate, Seleman Fikirini, alionesha umakini wake langoni kwa kupunguza idadi zaidi ya mabao kwani kama si uhodari wake wangefungwa zaidi ya hayo.

Ukiachana na mabao hayo, Ahoua alionekana kuwa katika kiwango bora zaidi kama ilivyotarajiwa na mashabiki wengi wa Simba kwani licha ya kufunga bao moja lakini alitengeneza mengine mawili kwa Balua na Mashaka.

Fountain Gate licha ya kuonekana ikicheza kwa kujiamini kuanzia nyuma lakini ilikosa ufanisi katika umaliziaji kwani winga zao, Dickson Ambundo na Salum Kihimbwa pamoja na straika, Hashi Kilemile walikuwa wakizidiwa idadi na walinzi wa Simba walionekana kuwa wengi kushinda wao.

Mara nyingi Gate ikifanikiwa kupora mpira golini kwao na kufanya shambulizi la kushtukiza walijikuta katika hali hiyo na kusababisha kuwa na idadi ndogo ya mashuti yaliyolenga na yasiyolenga goli na kufanya muda mwingi wa mchezo, Kipa Mousa Camara kuwa likizo.

Ligi hiyo itaendelea Jumatano kwa JKT Tanzania kuikaribisha Azam FC huku Alhamisi KMC ikiumana na Coastal Union na Kagera Sugar itaumana na Yanga SC katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Kaitaba, Kagera.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *