Msuva aamua kujiunga na Al Talaba ya Iraq

Na Mwandishi Wetu

KLABU ya Al Talaba inayoshiriki Ligi Kuu nchini Iraq, imekamilisha usajili wa winga wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva akitokea timu ya Al-Najma iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la Kwanza Saudi Arabia.

Msuva, 30, anatarajia kujiunga na timu hiyo ambayo ipo kwenye maandalizi ya kuelekea msimu wa 2024-25 ambao utaanza hivi karibuni.

Winga huyo ambaye pia anacheza timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, alihusishwa na usajili wa kujiunga na timu kadhaa za hapa nyumbani katika dirisha la usajili ambalo lilifungwa wiki iliyopita.

Akiwa Tanzania, Msuva aliwahi kupita katika timu ya vijana ya Azam FC kabla ya kutimkia Moro United lakini umaarufu wake mkubwa aliupatia Yanga ambapo alicheza kwa mafanikio kwa miaka mitano 2012-17.

Msimu wake wa mwisho kucheza soka la Tanzania ambao ni 2016-17, aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom enzi hizo na alishinda jumla ya mataji manne ya ligi akiwa na Yanga.

Mbali na Yanga lakini winga huyo pia amewahi kucheza timu za Difaa El-Jadid na Wydad Casablanca zote za Morocco na JS Kabyle ya Algeria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *