Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imedhamini sh. milioni 40.5 kwenye mashindano ya Ndondo Cup ikishirikiana na uongozi wa Michezo wa Shadaka.
Udhamini huo muhimu unaashiria dhamira ya TRA ya kukuza ushirikishwaji wa jamii kupitia michezo huku ikikuza mipango muhimu ya elimu ya kodi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, amesema ushirikiano huo na Ndondo Cup ni fursa ya kipekee kwa TRA kuwasiliana na wananchi kwa njia sahihi.
“Kupitia michezo, tunaweza kufikia hadhira kubwa zaidi ili kuwaelimisha na kuwashawishi kufahamu suluhisho la kisasa zaidi la Stempu za Ushuru za Kielektroniki katika kuhakikisha uhalisi wa bidhaa. Zaidi ya hayo, tunaamini kuwa kupitia mpango huu, tunaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa tabia za watumiaji na kuchangia katika lengo pana la kuimarisha uzingatiaji wa kodi kote nchini.’ amesema Katombo.
Amesema sehemu ya ushirikiano huo, TRA kwa kushirikiana na kampuni ya SICPA, ambaye ni mshirika mkuu wa teknolojia wa Stempu za Kielektroniki za Ushuru za TRA, itatumia jukwaa la Ndondo Cup kuhamasisha na kuelimisha umma kuhusu Stempu zake za Kielektroniki za Ushuru (ETS) na kampeni ya Hakiki Stampu.
“Ujumbe muhimu wa udhamini huu ni kuangazia umuhimu wa kuhakiki bidhaa kabla ya kuzitumia ili kuhakikisha kuwa ni salama, ni halisi na zinatii kanuni za kodi,” amesisitiza Kayombo.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Usimamizi wa Michezo wa Shadaka, Shaffih Dauda, ameshukuru kwa msaada wa TRA, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kampuni katika kuongeza thamani ya michezo ya ndani.
‘Tunafuraha kuwa na TRA kama wadhamini wakuu wa Ndondo Cup mwaka huu. Udhamini huu sio tu kwamba unasaidia maendeleo ya soka la chini lakini pia una lengo kubwa zaidi kwa kuelimisha umma juu ya masuala muhimu ya kodi, vilevile viwanja vyetu vya michezo vinajaa bidhaa mbalimbali, hivyo tunatarajia ushirikiano huu ili kuhakikisha teknolojia hii inasaidia. Tujikinge na bidhaa feki kwa tunapokuwa viwanjani’, amesema Dauda.
Lakini pia ikumbukwe katika michuano ya mwaka huu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametia mkono wake kwa kutoa zawadi ya ‘Goli la Mama’ ambapo kila timu itakayofunga bao kuanzia hatua ya robo fainali na kuibuka na ushindi italamba sh. 500,000.
Mbali na zawadi hiyo, Rais Samia pia ametangaza zawadi kubwa kwa timu itakayoshinda michuano ya Ndondo Cup. Bingwa wa michuano hiyo atapata zawadi ya shilingi milioni 5, wakati timu itakayoshika nafasi ya pili itazawadiwa shilingi milioni 2.
Zawadi hizo zinalenga kuongeza hamasa kwa wachezaji, kuhakikisha wanatoa uwezo wao wote kwenye mchezo, na pia kuonyesha kwamba jitihada zao zinatambulika na kuthaminiwa na serikali.