Simba yaanza kwa kishindo Ligi Kuu NBC

Na Badrudin Yahaya

KLABU ya Soka ya Simba, imeanza vyema kampeni za kusaka taji la Ligi Kuu ya NBC msimu huu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya KMC kwenye mchezo wao wa mzunguko wa kwanza uliochezwa katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam.

Licha ya Simba kutawala sehemu kubwa ya mchezo huo lakini ilionekana kukosa meno makali ya kutumia nafasi ambazo walizipata katika mchezo huo.

Mlinzi wa kati raia wa Cameroon, Che Fondoh Malone, ndiye alifunga akaunti ya mabao kwa Simba akifunga bao kipindi cha kwanza baada ya kupokea krosi ya Jean Charles Ahoua. Bao hilo lilidumu hadi timu zote zinakwenda mapumziko.

Kipindi cha pili Kocha wa Simba, Fadlu Davids, aliwatoa Steven Mukwala, Mzamiru Yassin na Ahoua na nafasi zao zilichukukuliwa na Valentino Mashaka, Augustine Okajepha na Kibu Denis.

Mabadiliko hayo yalionekana kuzaa matunda kwa Simba kwani ilizidisha mashambulizi kwenye lango la Tabora United na kufanikiwa kufunga bao la pili kupitia kwa Mashaka ambaye ni mchezaji mpya ndani ya timu hiyo akitokea Geita Gold.

Wakati mchezo ukiwa unaelekea mwishoni, Simba ilipata bao la tatu lililofungwa na Awesu Awesu ambaye naye aliingia tangu kipindi cha kwanza kuchukuwa nafasi ya Joshua Mutale ambaye alipata majeraha.

Awesu amefunga bao hilo ikiwa ni siku chache tangu amemaliza sakata lake la usajili ambalo liliihusisha timu yake ya zamani ya KMC.

Mara baada ya ushindi huo Simba, inakwea juu kwenye msimamo wa NBC kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya Singida Black Stars ambao nao waliibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Ken Gold katika mchezo uliochezwa mapema mchana.

Simba na Singida Black Stars zinatarajia kukutana katika mchezo wa mzunguko wa pili ambao utachezwa Jumapili ijayo katika dimba la KMC Complex.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *