Dkt. Biteko apongeza jitihada za CRDB Bank Marathon kusaidia jamii

Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko, ameipongeza taasisi ya CRDB Bank Foundation kwa kuendelea kuandaa mbio za CRDB Bank Marathon ambazo zimejielekeza katika kusaidia jitihada za serikali kuboresha sekta ya afya, kusaidia wenye uhitaji pamoja na kukuza ustawi wa jamii.

Dkt. Biteko alitoa pongezi hizo wakati wa kilele cha msimu wa tano wa CRDB Bank Marathon ambapo jumla ya sh. milioni 350 zimekusanywa kwa ajili ya kusaidia watoto wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI), huduma za afya kwa wakinamama wenye ujauzito hatarishi hospitali ya CCBRT na uwezeshaji wa vijana.

“Niwapongeze kwa kuendelea kusaidia matibabu ya wakinamama na watoto wetu. Wakinamama ndio wamebeba uchumi wa Taifa letu. Lakini pia wakinama ndio waangalizi wa familia zetu hususani watoto.

 Hivyo ukiimarisha afya ya mama na watoto umeimarisha afya ya Taifa,” alisema Dkt Biteko huku akisema Serikali na Watanzania wanaona jitihada hizo zinazofanywa na Benki ya CRDB kupitia CRDB Bank Foundation.

Kwa upande wake, Waziri wa Sanaa, Utamaduni, na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro, alisema CRDB Bank Marathon imesaidia kwa kiasi kikubwa kuchochea ari ya michezo nchini.

Ndumbaro alisema mbio hizo zimekuwa jukwaa muhimu kwa wanariadha nchini kuonyesha vipaji vyao katika jukwaa la kimataifa kwani mbio hizo zimesajiliwa kimataifa na Shirikisho la Upimaji Mbio Kimataifa (AIMS) na Shirikisho la Riadha Duniani (World Athletic).

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema katika kiasi cha fedha kilichokusanywa, sh. milioni 100 zitasaidia watoto wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo JKCI ambapo sh. milioni 100 nyingine zitasaidia huduma za afya kwa wakinamama wenye ujauzito hatarishi hospitali ya CCBRT na sh. milioni 150 zitasaidia uwezeshwaji kwa vijana.

Pia Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Bank Foundation, Martin Warioba, alisema mbizo hizo zimeshirikisa wanamichezo zaidi ya 8,000 ambazo jumla ya sh. milioni 98.7 zimetumika kuzawadia washindi 60 wa mbio za kilometa 42, 21, 10, 5 pamoja na mbio za baiskeli za kilometa 65.

Warioba alisema lengo la mwakani ni kupata washiriki 10,000 Tanzania, huku malengo ya washiriki Burundi na DR Congo yakiwa ni 3,000 kila nchi.

Katika mbio hizo, Joyloyce Kemuma wa Kenya alishinda mbio kilometa 42 upande wa wanawake wakati kwa upande wa wanaume, Mkenya, Moses Nengichi alishinda.

Katika Kilometa 21 upande wa wanawake ni Sara Makera kutoka Tanzania alishinda wakati kwa upande wa wanaume, Joseph Panga aliibuka kidedea.

Kwa upande wa Kilometa 10, Hamida Nasoro wa Tanzania aliibuka mshindi na kwa upande wa wanaume, Mtanzania Mao Hindo Ako alishinda.

Kwa upande wa baiskeli, Paul Lumoria, alishinda na kufuatiwa na Richard Laizer na Joseph Thuku ambapo kwa upande wa wanawake mshindi alikuwa Jamila Abdallah na kufuatiwa na Monica Jelimo na Julia Miringu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *