Benki ya TCB kushirikiana na Bunge kuinua wajasiriamali

KATIKA jitihada za kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi za kifedha na mihimili ya serikali, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Adam Mihayo, amemtembelea na kuzungumza na Spika wa Bunge la Tanzania, Tulia Ackson.

Mihayo aliambatana na Mkurugenzi wa Biashara za Wateja Wadogo na wa Kati wa benki hiyo, Lilian Mtali, katika ziara hiyo ambayo inafungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya Benki ya TCB na Bunge la Tanzania katika kuwainua wajasiriamali wadogo na wa kati nchini.

Mihayo alisema mazungumzo hayo yalijikita katika masuala nyeti yanayohusu majimbo mbalimbali katika jitihada za kuendelea kuwainua wajasiriamali wadogo na wa kati.

“Kwa kutambua mchango mkubwa wa kundi hili la wabunge katika ukuaji uchumi na uzalishaji wa ajira mpya, mazungumzo yetu yamejikita katika kuanzisha mpango wa ruzuku, mikopo ya riba nafuu na misamaha ya kodi kwa wajasiriamali,” alisema Mihayo.

Alisema miradi hiyo itasaidia kukuza na kuchochea mazingira ya biashara kwa wajasiriamali pamoja na biashara zao.

“Lengo letu sio kutoa jibu moja kwa nchi nzima, kuwezi kuwa na suluhisho moja kwa watu wote, ndiyo maana ni muhimu kuwasikiliza wadau wengi iwezekanavyo,” alisema Mihayo.

Naye Spika Tulia, alisema  umuhimu wa ushirikiano huo na kusisitiza wajibu wa Bunge katika kutunga sera zinazowezesha maendeleo ya wajasiriamali na kuhakikisha kwamba biashara zao zinapata rasilimali zinazohitajika ili kukua.

“Maendeleo ya wajasiriamali ni muhimu kwa ukuaji uchumi wa Taifa letu, kupitia ushirikiano huu na Benki ya TCB, tunaweza kutengeneza mazingira yatakayowezesha ukuaji wa biashara,“ alisema.


Kikao hicho kilihitimishwa kwa azimio la ushirikiano wa pamoja na kuendelea kubuni nyanja mbalimbali za ushirikiano lengo likiwa kuinua sekta ya wajasiriamali nchini.

Ushirikiano huu unategemewa kufungua miradi mbalimbali itakayosaidia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *