NDC yasaini mkataba wa uwekezaji na FUJIAN wa dola milioni 77.45

Na Mwandishi Wetu, Njombe

SHIRIKA la Taifa la Maendeleo (NDC), limesaini mkataba wa ubia wa uwekezaji na Kampuni ya Fujian Hexingwang Industry Tanzania Co. Limited wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 77.45 ili kuchochea uchumi wa kisasa unaoongozwa na sekta ya viwanda mama.

Mkataba huo unahusisha uchimbaji na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata chuma ghafi kilichopo Maganga Matitu, Wilaya ya Ludewa mkoani hapa.

Uwekezaji huo wa kimkakati ni wa kwanza wa aina yake nchini Tanzania tangu dunia ilipoingia kwenye zama za chuma (iron age).

Mkataba huo wa uwekezaji wa ubia umesainiwa mkoani hapa mbele ya Mgeni Rasmi, Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Dotto Biteko (Mb) ambaye pia ni Waziri wa Nishati.

Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini mkataba huo, Dkt. Biteko alisema, hatua ya kusaini mkataba huo ni matokeo ya juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha rasilimali zilizopo nchini zinawanufaisha wananchi.

Alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa muumini wa kuikaribisha sekta binafsi kuungana na sekta ya umma ili kufungamanisha mashirkiano baina ya pande mbili katika kukuza uchumi wa nchi yetu.

“Kwa utekelezaji wa mradi huu pamoja na mingine, dhamira yake ni kuhakikisha chuma kinapatikana hapa nchini,”alisema Dkt. Biteko.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exhaud Kigahe, alisema kusainiwa kwa Mkataba huo kutachangia kujenga uchumi wa viwanda na kufungua fursa nyingi za kiuchumi katika Mkoa wa Njombe na Taifa kwa ujumla.

Aliongeza mahitaji ya chuma hapa nchini ni makubwa, ambapo asilimia kubwa chuma kinachotumika hulazimika kuagizwa kutoka nje ya nchi.

“Uhakiki wa taarifa za mashapo uliofanyika katika mradi huu wa Maganga Matitu umeonesha uwepo wa mashapo ya chuma tani milioni 10,” alisema Kigahe.

Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NDC, Dkt. Edwin Mhede alisema, chuma ghafi ni zaidi ya madini kwani kina mchango mkubwa kwa maendeleo ya viwanda mama ambavyo huongeza thamani ya chuma ghafi na kuzalisha bidhaa za chuma kwa matumizi mbalimbali ya viwanda.

Aliongeza mkataba huo ni ushahidi usioghoshiwa kuwa ufanisi wa kiutendaji wa NDC unaeondelea kuboreshwa umeongeza imani kwa jamii na ndio maana mbia mwenza wa sekta binafsi (FUJIAN) sasa amevutiwa na kuwa na imani ya kuungana na mbia mwezake wa sekta ya umma (NDC) ili kufanikisha uwekezaji huu wa kimkakati.

Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo kwa mgeni rasmi, Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe, alisema mkataba huo umesainiwa kutokana na majadiliano ya muda mrefu baina ya pande zote mbili.

Alisema kwa mujibu wa mkataba huo, mwekezaji atatoa mchango wake wa ubia wa uwekezaji kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 77.45 kama mtaji (equity) na sio mkopo.

Pia, atajenga mgodi wa chuma wenye uwezo wa kuzalisha tani milioni 1 kwa mwaka na kiwanda cha kuchenjua chuma ghafi.

Makubaliano mengine katika mkataba huu ni pamoja na mwekezaji mwenza (FUJIAN) kulipa fidia ama kabla au ifikapo Januari 2025.

Halmashauri ya Ludewa imekamilisha uthamini wa mali za wananchi 385 watakaolipwa shilingi 4,215,600,214.47 ili kupisha shughuli za mradi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *