Katimba ahamasisha waumini wa Anglican kujiandikisha daftari la mpiga kura

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Zainab Katimba, ametoa wito kwa waumini wa Kanisa la Anglican nchini kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura.

Lengo ni kuwa na uhakika wa kupata fursa ya kuchagua viongozi bora watakaoliletea taifa maendeleo.

Katimba ametoa wito huo wakati akimuwakilisha Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko kwenye ibada ya harambee maalumu ya ujenzi wa Kanisa Kuu la Andrea Mtakatifu la Uaskofu lililopo Kasulu Dayosisi ya Western Tanganyika.

“Sote tunafahamu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezindua zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura hapa mkoani Kigoma, hivyo niwakumbushe kujiandikisha na kuboresha taarifa zenu ili kumuunga mkono Mhe. Rais kwa kuchagua viongozi watakaoshirikiana nae kuleta maendeleo nchini,” Katimba amesisitiza.

Katimba amesema zoezi la kuboresha daftari la kudumu la mpiga kura mkoani Kigoma litakuwa la siku saba hivyo wananchi wajitokeze mapema kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ili kupata sifa ya kushiriki uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025.

Aidha, Katimba amewasilisha mchango wa Sh. milioni 20 uliotolewa na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko kuchangia ujenzi wa wa Kanisa Kuu la Andrea Mtakatifu la Uaskofu lililopo Kasulu Dayosisi ya Western Tanganyika.

Akizungumzia ushiriki wa waumini katika maboresho ya Daftari la Kudumu la Mpiga Kura, Baba Askofu Emanuel Charles Bwata amemhakikishia Katimba kuwa, kanisa linawaamasisha waumini kujiandikisha na kuongeza kuwa binafsi yeye alishaanza kuwahamasisha kabla ya Mhe. Waziri Mkuu kuzindua rasmi zoezi hilo mkoani Kigoma.

Aidha, Baba Askofu Emanuel Charles Bwata amemshukuru Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko kwa kutoa mchango wa shilingi milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa Kuu la Andrea Mtakatifu la Uaskofu la Kasulu.

Jumla ya Sh. milioni 134,134,200 zilipatikana katika ibada hiyo ya harambee maalumu ya ujenzi wa Kanisa Kuu la Andrea Mtakatifu la Uaskofu lililopo Kasulu Dayosisi ya Western Tanganyika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *