Rais Samia alivyowezesha kukuza mtaji wa Diana

Na Salha Mohamed

“TANZANIA ni Mahali Sahihi pa biashara na uwekezaji”. Kauli mbiu hii imetumika kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba yaliyokuwa yakifanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Katika kuzingatia ufanyaji biashara na uwekezaji kwa wafanyabiashara hapa nchini, Serikali imetenga kiasi cha sh. bilioni 18.5 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali nchini.

Fedha hizo zitatolewa kama mikopo yenye masharti nafuu kupitia Benki ya NMB kwa miaka miwili kukopeshwa wafanyabiashara wadogo na wakati kwa riba yaa silimia saba.

Serikali mara zote imekuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia wajasiriamali kwa kuwajengea mazingira mazuri ya kufanya biashara zao.

Mikakati hiyo ni pamoja na kuzalisha bidhaa bora na kupata masoko ya uhakika.

Diana Mkaudiya ni mjasiriamali anayejihusisha na biashara ya kutengeneza vitu vya asili kama shanga na uzi katika mkoa wa Arusha, anayemiliki kampuni inayotambulika kwa jina la Bethel Hands Product ambayo inajihusisha na biashara ya vitu vya asili na kuajiri vijana wanne.

Anasema mwaka 2012 ameanza biashara hiyo mkoani Arusha baada ya kukaa muda mrefu tangu alivyomaliza kidato cha nne mwaka 2004 bila kujihusisha na jambo lolote.

“Mwaka 2004 nilimaliza kidato cha nne, nilikuwepo tu nyumbani bila kujishughulisha na kitu chochote, sikuvutiwa na kitu ni mtu aliniambia tu kuna biashara njoo ufanye, ndipo nikaajiriwa dukani kufanya biashara ya vitu vya asili na hapo ndipo nikaanza kuipenda kazi.

“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwani naendeleaa kukua kwani ni nimekuwa nikishughulika zaidi na kazi zangu za mikono kwa kutumia shanga na uzi,” anasema.

Anasema hadi sasa soko la biashara hiyo limekuwa kwasababu ameanza na mtaji wa Shs. 500,000 na sasa mtaji umefikia sh milioni 10.

Anasema mafanikio hayo yamewezesha kuvalisha wanamitindo mbalimbali ambao wanapenda kuvaa kitamaduni na kufanya urembo wa asili kwenye nyumba.

Mwamko wa biashara

Diana anasema kwa sasa mwamko wa biashara hiyo ni mkubwa kwasababu Watanzania wameelewa namna ya kutumia na kupamba kitamaduni.

“Sasa hivi imekuwa si jambo la kushangaza kwamba mtu akivaa kitamaduni kwa mfano kuvaa shanga, kupamba nyumba na shanga si tatizo tena kama zamani watu kuhusisha na imani za kishirikina au mambo ya kichawi, sasa imekuwa ni kwenda na wakati (fasheni),” anasema.

Anasema soko limekuwa kubwa kwasababu wanaovaa vitu vya shanga au kitamaduni watu wanamuona aliyevaa kama mzungu fulani yaani thamani inaongezeka kwa utofauti.

Anasema kwa sasa anao wateja wa ndani na nje ya Tanzania ambapo soko kubwa la bidhaa yake likiwa ni Marekani ambapo kuna mteja mkubwa anayevalisha warembo (ma-miss) nchini humo.

Anafafanua kuwa Soko lingine lipo nchi ya Afrika ya Kusini na Comoro kwa upande wa Afrika Mashariki ambao si wanunuzi sana wa bidhaa hiyo lakini wamekuwa wakipambana na Wakenya kwani nao soko la shanga ni kubwa.

Anasema watu ambao wamekuwa wakinunua bidhaa hiyo kwa Afrika Mashariki ni Uganda na nje ya Jumuiya hiyo ni Saudi Arabia.

Anasema kwa Tanzania soko kubwa lipo mkoani Arusha lakini mteja popote atakapokuwepo anapelekewa bidhaa zake.

Kuhusiana na upambaji nyumbani aliwashauri watu watumie bidhaa za asili kama shanga kwa sababu inapendeza na ni kitu cha tofauti ukilinganisha na mapambo yanayoletwa kutoka nje ya nchi.

Changamoto

Diana anasema wakati anaanza biashara hiyo alikumabana na changamoto za soko kuwa chini, sehemu ya kuuzia bidhaa zake, kutofahamika na wateja na baadhi kutokuwa na imani na biashara hiyo huku wengine wakihusisha na imani za kishirikina.

“Hakuna changamoto kubwa ninayokutana nayo ikiwemo ya kikodi kwa sababu sehemu ninayofanyia biashara hakuna kodi kubwa ninayolipa zaidi ya Shs. 100,000 kwangu naona ni sawa na hainiumizi,” anasema.

Ameishukuru Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kuwakadiria kodi ya kiwango kimoja ambayo haiumizi kwasababu hulipa Shs. 100,000 kwa mwaka na Shs. 25,000 kwa awamu hivyo haimelemei.

“Zamani tulikuwa tunakadiriwa Shs. 360,000 hadi Shs. 500,000 sasa hivi wameturekebishia na kutufanyia Shs. 100,000 kwa kweli tunamshukuru Rais Dkt. Samia kwasababu ametufanyia kitu kizuri,” anasema.

Aidha anasema Serikali mara nyingi nimekuwa ikihimiza watu kutumia bidhaa za nyumbani za asili, nawashauri Watanzania wapende vitu vyao vya asili, utamaduni kwani wakipenda watanunua na kukuza biashara hii kiuchumi.

Amzungumzia Samia

Diana anasema Rais Samia Suhuhu Hassan amekuwa kiongozi wa kuigwa na wa mfano kwa wanawake kutokana na uthubutu alionao.

“Rais Samia ni kiongozi hodari kwasababu ametusaidia wanawake na kuwapa kujikubali na kujithamini na kujiona kuwa wanaweza,” anasema.

Katika maonesho ya Sabasaba, Diana anasema kwa mara ya tano na kumshukuru Mungu kwasababu walichokipata kupitia maonesho hayo si kibaya.

Baadhi ya waliofika Sabasaba

Maridhia Athumani, mkazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa wananchi ambao wamefika katika banda hilo ambapo amepongeza kazi za mikono ya Diana.

Anasema Diana ameweka thamani vitu vya asili na kuviongezea naksi ya shanga.

“Kwa kweli nimevutiwa sana na bidhaa za asili kwasababu nimejifunza aina mpya ya kupamba nyumba kupitia shanga na vitu vya uzi kwa kweli ifike wakati Watanzania tuthamini vitu vya kwetu kukuza uchumi wa nchi na wajasirimali wetu,” anasema Rose Ndauka mkazi wa Kinondoni.

Anasema kila mtu akithamini vitu vya ndani ya nchi vitaongezewa thamani jambo ambalo litafanya kutambulika zaidi ndani na nje ya nchi kwa sababu ukuaji wa uchumi sehemu yoyote huonekana pindi unapotoa kipaumbele kwa tamaduni za nchi husuka.

Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha watu kutumia na kuthamini bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi kwa kuleta maendeleo hivyo anapaswa kuungwa mkono kwa juhudi kubwa.

Mikakati ya serikali kwa wajasiriamali

Serikali imeweka mipango kadhaa ya kuwasaidia wajasiriamali kuzalisha bidhaa bora ili kupata masoko ya uhakika.

Mikakati hiyo ni pamoja na kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuwasaidia wajasiriamali wadogo kupata maeneo au majengo ya kuzalishia bidhaa zao, kuwapatia mitaji kupita Mfuko wa NEDF na nembo ya ubora wa bidhaa zao kwa miaka mitatu bila gharama.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe anasema kupitia SIDO, TBS na Wakala wa Vipimo (WMA) kuendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali kuhusu kanuni za uzalishaji wenye tija, elimu ya utambuzi wa vifungashio na ufungashaji bora.

Pia anasema SIDO kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), kuendelea kuandaa na kuratibu maonesho mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwa ni sehemu ya kuchagiza ukuaji wa soko la bidhaa zinazozalishwa na Wajasiriamali.

Kuhusiana na mpango wa serikali wa kufanya mapitio ya sera ya biashara na sera ya wajasilimali wadogo alisema lemgo la serikali ni kuhakikisha wajasiriamali wanazalisha bidhaa zenye ubora.

“Ni kweli sera hizo zimepitwa na wakati na kuwa Serikali imeshaanza taratibu za mapitio ili ziweze kuendena na hali ya soko la ndani na nje na mahitaji ya sasa ya wajasiliamali,” anasema.

Pia serikali imepanga kuweka mazingira mazuri kwa wajasiriamali kuweza kuzalisha bidhaa bora na zenye viwango bora Vilevile Kigahe alisema SIDO imekuwa na uwezo mdogo wa kuwezesha mitaji kwa wajasiriamali ambao wamekuwa wakiongezeka kila wakati.

Anasema Serikali imeacha mchakato wa kuibadili sheria iliyoanzisha SIDO ili kuondoka kuwa taasisi ya uwezeshaji bali iweze kujiendesha kibiashara, sheria baada ya kuhudumia ianze kujiendesha kibiashara na kukidhi mahitaji ya wajasiliamali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *