Azma ya Samia kuulisha ulimwengu kutimia kwa kufanya kilimo biashara

Na Daniel Mbega, Dar es Salaam

ILE azma ya muda mrefu ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba Tanzania inao uwezo wa kuulisha ulimwengu sasa inaelekea kwenye mkondo sahihi kutokana na jitihada kubwa ambazo serikali yake inazifanya, hasa kwa kuwawekea mazingira wezeshi wakulima nchini.

Kutimia kwa azma hiyo kunafuatia pia agizo ambalo Rais Samia alilitoa mwishoni mwa wiki wakati akiwa mkoani Katavi, ambapo aliwataka Watanzania waachane na utamaduni wa ‘kulima na kula’ na sasa wageukie kwenye kilimo cha biashara.

“…Tutoke kwenye kulima na kula, tufanye biashara,” akasisitiza Rais Samia.

Na akaeleza wazi kwamba, bei ya mahindi kwa mwaka huu itaanzia Shs. 600 kwa kilo moja, jambo ambalo limewapa faraja kubwa wakulima ambao kwa miaka mingi wamekuwa hawanufaiki na kilimo chao kwa kupatiwa bei hafifu na walanguzi, wakati wanatumia nguvu na gharama kubwa.

“Niwaahidi wana Katavi jicho la Serikali lipo katika Mkoa huu, lengo ni kuufungua Mkoa wa Katavi kwa njia zote na kama mnavyojua Bandari ya Karema tumeshaimaliza na imeanza kazi na sasa tunaenda kujenga barabara inayounganisha Bandari hiyo ili kufikisha bidhaa na mazao katika soko,” alisema Dkt. Samia wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Kibaoni – Mlele (km 50) ambao umefika asilimia 15.

Mara kwa mara Rais Samia amekuwa akisisitiza kwamba, Tanzania inao uwezo mkubwa wa kuzalisha chakula kingi ambacho kinaweza kukidhi mahitaji ya ndani na ziada ikauzwa nje ili wakulima wapate fedha zitakazokuza uchumi wao.

Itakumbukwa kuwa, wakati akizindua Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) inayowahusisha vijana na wanawake katika kilimo, Rais Samia alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka malengo ya kuzalisha 20% ya mahitaji ya nafaka barani Afrika.

Katika kuyafikia malengo hayo, Rais Samia akasema, wamejikita katika kuboresha miundombinu ya umwagiliaji, kilimo ambacho ni cha uhakika kuliko cha kutegemea mvua.

Na ana haki ya kusema hivyo kwa sababu, katika hali ya sasa hata kabla ya utekelezaji wa Programu ya BBT, Tanzania inajitahidi kuzalisha chakula cha kutosha, licha ya changamoto ya ukame inayoikabili Dunia.

Kwa mfano, mwaka 2020/21 uzalishaji wa mahindi nchini ulikuwa tani milioni 6.53, wakati mahitaji halisi ya Taifa ni tani milioni 6. Kipindi hicho pia Tanzania ilizalisha tani milioni 1.85 za mchele, wakati mahitaji ni tani milioni 1.

Kwahiyo kulikuwa na ziada ya kutosha, na ndiyo ilitumika hata kuwauzia majirani ambao walikuwa wakikabiliwa na janga la njaa kama Kenya, Sudan Kusini, Malawi na Zambia lililochangiwa pia na mataifa hayo kusitisha shughuli za kawaida (lockdown) wakati wa janga la Uviko-19, wakati sisi tuliendelea na shughuli kama kawaida huku mamlaka zikiweka miongozo ya tahadhari.

Afrika kwa sasa iko katika uhaba mkubwa wa chakula ambao haujawahi kutokea katika miongo kadhaa, ambapo takriban watu milioni 282 barani humo wanakabiliwa na baa la njaa.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), idadi hiyo inaweza kuongezeka hadi kufikia milioni 310 ifikapo mwaka 2030.

Shirika la Fedha Duniani (IMF) linasema bei za bidhaa za chakula Kusini mwa Jangwa la Sahara zilipanda kwa wastani wa 23.9% katika kipindi cha mwaka 2020-2022, ukiwa ni mfumko mkubwa wa bei kuwahi kutokea tangu mwaka 2008 wakati hali hiyo ilipojitokeza duniani.

Changamoto za kidunia zimesababisha hali hiyo, kwani nchi nyingi katika ukanda huo zinategemea kuagiza nje chakula, hususan ngano, mafuta ya kupikia, na mchele.

Bei za mazao yaliyozalishwa ndani katika baadhi ya nchi zilipanda kutokana na usambazaji wa ndani kuvurugika, kushuka kwa thamani ya sarafu, gharama kubwa za mbolea na pembejeo nyingine.

Nchini Nigeria kwa mfano, bei za mihogo na mahindi zilipanda maradufu ingawa mazao hayo yanazalishwa ndani, wakati nchini Ghana bei ya mihogo ilipanda kwa 78% katika mwaka 2020-2021 kutokana na gharama za uzalishaji na changamoto ya usafiri, miongoni mwa sababu nyingi.

“Kwa kutumia takwimu kutoka nchi 15 katika mazao makuu ya chakula kwenye ukanda huo (mihogo, mahindi, mafuta ya kupikia, mchele na ngano), tumebaini kwamba pamoja na bei za dunia, utegemezi wa kuagiza kutoka nje, kiwango cha uzalishaji wa mazao ya chakula, na thamani ya sarafu vimesababisha kupanda kwa bei za chakula,” ilisema IMF.

FAO ikasema kwamba, kuongezeka kwa mahitaji ya chakula na kubadilika kwa tabia za matumizi kunachangia uagizaji mkubwa wa chakula nje ya Afrika, ambayo imepanda kutoka Dola bilioni 35 mwaka 2015 hadi zaidi ya Dola bilioni 110 mwaka 2021.

Takriban aina 15 za chakula zinaagizwa kutoka nje ya Afrika, zikiwemo aina tano za vyakula vikuu kama ngano, sukari, mchele, nyama na maharage.

Aidha, FAO imebainisha kwamba, gharama za kimataifa za uagizaji chakula kutoka nje zilikadiriwa kupanda hadi dola za Marekani trilioni 1.94 mwaka 2022, zaidi ya ilivyotarajiwa hapo awali, kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa Novemba 11, 2022 na shirika hilo.

Utabiri huo mpya ulioainishwa katika mtazamo wa chakula wa FAO ulidhihirisha kiwango cha juu zaidi na ongezeko la asilimia 10 zaidi ya kiwango kilichoweka rekodi cha mwaka 2021, ingawa kasi ya ongezeko hilo ilitarajiwa kupungua kutokana na ongezeko la bei ya juu ya chakula duniani na kushuka kwa thamani ya sarafu dhidi ya dola ya Marekani. 

Sababu zote hizo mbili zinapima uwezo wa kununua wa nchi zinazoagiza chakula na kiwango cha chakula kinachoagizwa kutoka nje.

Sehemu kubwa ya ongezeko la gharama hizo linachangiwa na nchi zenye mapato ya juu, kutokana na bei ya juu zaidi duniani, huku viwango hivyo pia vikitarajiwa kupanda. 

Ripoti hiyo ya mtazamo wa chakula pia imetathmini matumizi ya kimataifa kwa bidhaa kama pembejeo za kilimo zinazoagizwa kutoka nje, ikiwa ni pamoja na mbolea. 

Gharama za kimataifa za uagizaji wa pembejeo zilitarajiwa kupanda hadi dola za Marekani bilioni 424 mwaka 2022, hadi kufikia asilimia 48 kutoka mwaka uliotangulia na kiasi cha asilimia 112 kutoka mwaka 2020.

Gharama za juu za nishati na mbolea zinazoagizwa kutoka nje ndiyo chachu ya ongezeko lililotarajiwa la bei ya chakula. 

Mahitaji ya chakula Afrika

Afrika inahangaika kutokana na uhaba wa chakula na gharama kubwa za uagizaji, wakati ambapo bara hilo lina 65% ya ardhi yenye rutuba ambayo haijalimwa duniani.

Ukanda wa Savannah wa Afrika una jumla ya hekta milioni 600, na hekta milioni 400 kati ya hizo zinafaa kwa kilimo, ingawa ni 10% tu ya ardhi inayolimwa sasa.

Kwahiyo, Afrika ndiyo yenye ufunguo wa kulisha watu bilioni 9 waliopo duniani ifikapo mwaka 2050.

Lakini kutokana na Afrika kukabiliwa na baa la njaa kila wakati, Tanzania imekuwa ikizalisha chakula cha ziada kila mwaka kulisha watu wake milioni 62 na kusafirisha nje ya nchi hasa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na maeneo mengine barani humo, ikiwemo Kusini mwa Afrika na kwenye Pembe ya Afrika.

Takwimu kutoka Wizara ya Kilimo na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonyesha kwamba Tanzania, ambayo inazungukwa na nchi nane, imekuwa ikisafirisha mazao ya chakula kama mchele, mahindi, mbogamboga, matunda, maharage na samaki.

Kama nilivyosema awali, katika msimu wa mavuno wa 2020/21, Tanzania ilizalisha zaidi ya meta za ujazo tani milioni 6.53 za mahindi, kulinganisha na mahitaji ya tani milioni 6, hivyo kuzalisha ziada ya tani 500,000 ya mahindi ya ziada.

Katika msimu huo huo, Tanzania ilivuna zaidi ya tani milioni 1.85 za mchele, ikivuka mahitaji halisi ya taifa ambayo ni tani milioni 1.065, hivyo kuzalisha ziada ya tani 800,000 za mchele.

Katika miaka mitano iliyopita (2018 hadi 2022), Tanzania iliingiza fedha za kigeni Dola za Marekani bilioni 3 kutokana na mauzo ya vyakula nje ya nchi, kama nafaka, mazao ya bustani, matunda na samaki.

Usafirishaji wa mbogamboga uliingizia nchi Dola za Marekani bilioni 1.01 katika kipindi cha miaka mitano, wakati nafaka, hasa mahindi na mchele, yaliingiza Dola milioni 999 katika kipindi hicho hicho.

Tanzania pia ilisafirisha nje mazao ya samaki yenye thamani ya Dola milioni 800 kati ya mwaka 2018 na 2022, na kuingiza jumla ya Dola milioni 71.4 kutokana na kusafirisha matunda nje, kwa mujibu wa takwimu za BoT za hivi karibuni.

Kwa takwimu hizo inaonyesha kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi chache za Afrika zinazozalisha kwa wingi chakula na inayo nafasi kubwa ya kuulisha ulimwengu.

Tangu kuingia madarakani Machi 2021, Rais Samia Suluhu Hassan amewekeza kwenye sekta ya kilimo katika kiwango ambacho hakijapata kutokea tangu nchi hiyo kupata Uhuru mwaka 1961.

Serikali yake imeongeza kwa kiasi kikubwa bajeti ya sekta ya kilimo kwa mwaka 2022/23 kufikia Dola milioni 411.2, ongezeko kubwa kutoka Dola miloni 126.7 zilizotengwa kwa mwaka 2021/22.

Mwaka 2003, wakuu wa nchi za Afrika walikubaliana kutumia 10% ya bajeti zao kwenye kilimo ili kuongeza uzalishaji kufikia mwaka 2008 kwa mujibu wa Azimio la Maputo lililozungumzia Kilimo na Usalama wa Chakula Afrika. Hata hivyo, miongo miwili baadaye, mataifa mengi ya Afrika hayajafikia lengo hilo.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alisema hatua za makusudi zimechukuliwa na Serikali ya Samia, ikiwemo kuzindua Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT-YIA) kwa vijana na wanawake, kuanzisha mkopo maalumu wa kilimo wa Shilingi trilioni 1, ruzuku ya mbegu na mbolea, kupanua eneo la umwagiliaji na miundombinu ya uzalishaji mbegu, mambo yatakayochochea Tanzania kusafirisha chakula barani Afrika.

“Tuna hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo nchini Tanzania, lakini kwa sasa tunalima kati ya hekta milioni 10 na 15. Kwahiyo tunazo hekta milioni 29 zenye rutuba zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, lakini kwa sasa zinazotumika ni chini ya 5%,” alisema Bashe.

“Kwa jitihada zinazochukuliwa na serikali kuingiza fedha kwenye miundombinu ya sekta ndogo ya umwagiliaji, tunadhani kwamba mojawapo ya matokeo ya Kongamano la Kilimo Afrika (AGRF 2023) baada ya kuuonyesha ulimwengu tulicho nacho ni kuwavutia sekta binafsi kuwekeza kwenye kilimo nchini.”

Serikali ya Tanzania imeweka malengo ya kuzalisha 20% ya mahitaji ya nafaka Afrika na ili kufikia malengo hayo serikali imeanza kuwekeza kwa kiwango kikubwa kwenye miundombinu ya umwagiliaji.

“Kama tunavyofahamu Afrika inahitaji wastani wa meta za ujazo tani milioni 45 za mchele kwa mwaka, lakini uzalishaji ni wastani wa 50% ya mahitaji ya mwaka. Afrika pia inahitaji wastani wa tani milioni 115 hadi 150 za mahindi kwa mwaka. Lengo la nchi yetu ni kuzalisha 20% ya mahitaji hayo ya Afrika kwa mwaka,” alisema Bashe.

“Hata hivyo, dira na mwelekeo wa serikali ni kwa miaka 2030 na 2050 ambapo idadi ya watu barani Afrika itakuwa karibu bilioni 2 na mahitaji ya chakula yatakuwa yameongezeka kwa 50%. Kwa idadi hiyo, Tanzania imeanza kujiandaa kuhudumia wakati ujao na ndiyo malengo ya serikali. Tunataka kusaidia sehemu nyingine ya Afrika kupunguza uagizaji wa chakula nje na kufikia malengo ya akiba ya chakula.”

Kwa upande wake, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeendeleza mkakati wa mabadiliko ya muda mrefu ya kilimo Afrika.

Mnamo Oktoba 2015, Benki hiyo iliandaa Mkutano wa Mawaziri kuhusu “Kuilisha Afrika – Mpango Kazi wa Kubadili Kilimo Afrika” uliofanyika mjini Dakar kuangalia namna ya kufungua fursa za kilimo barani humo na kuzalisha ajira ili kuweka kilimo mseto. Agenda ya Mabadiliko ya Kilimo inaunga mkono utekeleza wa Malengo Endelevu ya Dunia katika kuendelea uchumi shirikishi na sekta ya kilimo-biashara yenye ushindani Afrika.

Lengo kuu la kipaumbele cha Kuilisha Afrika ni kuifanya Afrika kuwa msafirishaji wa chakula nje ifikapo 2025. Mabadiliko yatahusisha kuunganisha rasilimali na mitaji, ikiwakilisha fursa muhimu kuchochea ushirikishwaji na ukuaji wa uchumi kwenye mnyororo wa thamani.

Kubadilisha seti ya awali ya minyororo ya thamani ya kilimo barani Afrika kutahitaji takriban Dola bilioni 280-340 kwa muongo ujao. Uwekezaji huo utazalisha masoko mapya yenye thamani ya Dola bilioni 55-65 kwa mwaka kufikia 2025.

AfDB ilisema uwekezaji wake katika kilimo (wa umma na binafsi) unatarajiwa kuongezeka mara nne kutoka wastani wa sasa wa dola milioni 612 hadi takriban dola bilioni 2.4.

Wachambuzi wanasema miongo kadhaa ya kutelekezwa imekatiza sekta ya kilimo barani Afrika, na kuziacha nchi nyingi barani humo zikiwa katika hatari ya kukumbwa na mzozo wa mara kwa mara wa chakula.

Mavuno ya chini au tija katika kilimo cha Kiafrika kwa muda mrefu imekuwa ikitajwa kama kikwazo kwa usalama wa chakula wa bara hilo.

Kulingana na Agnes Kalibata, Rais wa Muungano wa Mapinduzi ya Kijani barani Afrika (AGRA), iwapo uwiano wa wakulima wa Afrika wanaotumia mbegu bora utapanda kutoka asilimia 25 hadi 50, Afrika itaweza kuzalisha chakula cha kutosha kujilisha yenyewe. Kama idadi itapanda hadi 75%, wakulima wa Kiafrika wangezalisha chakula cha kutosha “kulisha dunia nzima”.

“Tuna faida nyingi: tuna ardhi nzuri, tuna maji na idadi ya watu ni vijana sana, lakini hatuwekezi katika sekta hiyo.

“Nadhani tatizo kubwa ni kutochukua hatua kwa wakati, matatizo madogo yameachwa kukaa kwa muda mrefu,” alibainisha Kalibata.

“Lazima ujiulize: kwa nini Afrika inakabiliana na mgogoro wa chakula? Tunaweza kuwa muuzaji chakula nje wa kimataifa, lakini badala yake sisi ni waagizaji wa jumla wa chakula, na biashara ndogo kati yetu wenyewe.”

Akaongeza: “Majibu yanajulikana. Teknolojia zipo. Mambo haya yalifanywa karne moja iliyopita. Tunachohitaji kufanya ni kuzipitisha na kuziingiza katika maisha yetu, lakini hatujafanya hivyo. Tulijua mabadiliko ya hali ya hewa yanakuja, lakini tulizika vichwa vyetu kwenye mchanga… Kwangu mimi, nasikitika kusema, tunaweza kushindwa kweli kwa uongozi wa kisiasa.”

Kwa uongozi wa mabadiliko wa Rais Samia, Tanzania inaelekea kuwa nchi ya mfano barani Afrika siyo tu ya kujitosheleza kwa chakula, bali pia kuwa muuzaji mkuu wa chakula nje ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *