Na Daniel Mbega, Dar es Salaam
KUIMARIKA kwa miundombinu bora, hasa ya barabara, ni mojawapo ya vipaumbele vikuu vya Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa na dhamira ya kuitekeleza kwa bidi Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) yam waka 2020-2025 kabla ya Oktoba 2025.
Kwenye upande wa Reli ya Kisasa (SGR) amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuendeleza mradi huo wa kimkakati na sasa usafiri wa treni iendayo haraka kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro tayari umekwishaanza huku ule wa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ukitarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa.
Aidha, kwa upande wa nishati, dunia imeona ongezeko la zaidi ya megawati 470 kwenye Gridi ya Taifa zilizozalishwa kwenye mradi wa kimkakati wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, hususan kutoka Mtambo Namba 8 na 9.
Sekta ya Afya amefanikiwa kwa asilimia kubwa kukamilisha ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali, zikiwemo za wilaya, mikoa na rufaa, huku vitendanishi vikiongezwa pamoja na dawa, na hivi karibu Serikali yake ikatoa nafasi takriban 9,800 kwenye kada mbalimbali.
Kwa upande wa elimu, Rais Samia aliendeleza pale mtangulizi wake alipoishia, baada ya kutangaza kwamba, elimu bila malipo sasa ni mpaka Kidato cha Sita na siyo Kidato cha Nne pekee, huku akiwafuta machozi mabinti waliokatishwa masomo kwa kupata ujauzito baada ya kuruhusu warejee shuleni kutimiza ndoto zao.
Sasa kama Serikali ya Awamu ya Tano, ambayo yeye alikuwa Makamu wa Rais wakati huo, ilifanikiwa kuongeza mtandao wa barabara za lami kwa kujenga barabara zenye urefu wa kilometa 2,023.34 na madaraja 10, yeye amepania kuongeza mtandao huo kwa kujenga barabara za lami zenye urefu wa kilometa 9,317 kama ilivyoahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi.
Ukiacha ujenzi wa miradi mbalimbali ya barabara unaoendelea, lakini upembuzi yakinifu wa barabara zenye urefu wa kilometa 5,974.2 na daraja moja umekamilika huku upembuzi yakinifu ukiendelea kwa barabara zenye urefu wa kilometa 3,342.6.
Miradi inayoendelea
Kama CCM ilivyoahidi kwenye Ilani yake, Rais Samia anaendelea kukamilisha ujenzi na ukarabati wa km 1,716.75 za barabara kwa kiwango cha lami katika barabara kuu na barabara za mikoa.
Miradi hiyo inayohusisha pia barabara za kuondoa msongamano kwenye majiji na miji mbalimbali nchini, ikiwemo barabara za mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam, zinatajwa kwamba zinagharimu takriban Shs. trilioni 4.493.
Hizi ni fedha nyingi sana ambazo hata kama nyingine zinatoka kwa wahisani pamoja na mikopo yenye masharti nafuu, lakini mwisho wa siku zitalipwa kutokana na kodi za wananchi.
Ni kutokana na ukweli huo, ndiyo maana Rais Samia amekuwa akisisitiza ubora wa miradi unaoendana na gharama halisi ya fedha, ili Watanzania wafurahie matunda ya uhuru wao.
Ukitazama kwa haraka, miradi mingi kati ya hii ni ile ambayo ilikuwa imesimama kwa muda mrefu kutokana na sababu mbalimbali huko nyuma, mingine mikataba yake ikiwa imesainiwa tangu Awamu ya Nne lakini ikashindwa kuendelea kwa wakati huo.
Rais Samia ameona ni vyema aisimamie kwa bidi ili kuharakisha maendeleo ya wananchi ambao bado wana Imani kubwa na Serikali ya CCM.
CCM katika Ilani ya Uchaguzi iliahidi kuanza ujenzi mpya (km 6,006.04) na ukarabati wa barabara kwa kiwango cha lami, ambao Rais Samia ameutekeleza kwa kiwango kikubwa mpaka sasa.
Serikali yake imeweka mikakati mbalimbali ya kuanza ujenzi mpya kwenye barabara ambazo zitaiunganisha Tanzania katika maeneo mengi.
Kwa mfano, kuna mradi wa upanuzi wa Barabara ya Kibaha – Chalinze kuwa njia nane (km 75), ambao ukikamilika utatokomeza kabisa foleni kwenye barabara hiyo, kwani itaungana na ile ya Ubungo – Kibaha yenye njia nane pia.
Kuna mradi wa barabara ya Handeni – Kiberashi – Kondoa mpaka Singida ambapo Serikali imepanga kuanza na km 50 za sehemu ya Handeni – Kiberashi.
Siyo siri kwamba, ikiwa barabara hii itajengwa mpaka Singida, itarahisisha mawasiliano kwa sababu mtu anayetoka Tanga au Dar es Salaam hatalazimika tena kupita Moshi-Arusha na Manyara, bali atakatiza katikati hadi Singida, na ikiwa anataka kuendelea, atachagua mwenyewe.
Serikali pia ina mpango wa kujenga barabara za Arusha – Kibaya – Kongwa yenye urefu wa km 430), na Kongwa – Mbuyuni NARCO Junction – Kibaya – Orkesmet yenye km 340), ambazo zitaunganisha maeneo ya katikati kwenye mikoa ya Arusha, Dodoma na Manyara, ambako shughuli za uchumi ni nyingi lakini wanakosa usafiri wa uhakika kupeleka bidhaa zao kwenye masoko.
Kuna barabara ya Makongolosi – Rungwa – Mkiwa yenye km 412, ambayo kwa hakika itachochea maendeleo kwenye mikoa Nyanda za Juu Kusini, hususan wilayani Chunya ambako kuna shughuli nyingi za uchimbaji wa dhahabu ikiwa inazalisha kilo 300 kila mwezi, na uwepo wa madini adimu (Rare Earth) ambayo yanatumika kutengenezea vifaa vya elektroniki.
Kuna pia barabara ya km 148 ya Makofia – Mlandizi – Vikumburu, ambayo ikiwa itajengwa na kuwekwa lami itachochea maendeleo ya uchumi wa wananchi wa Wilaya ya Kisarawe, na kutengeneza fursa za uwekezaji na ajira kwenye kilimo.
Kujengwa kwa barabara za Mbamba Bay – Liuli – Lituhi (km 112.5) na Kitahi – Lituhi (km 93) kutaleta manufaa makubwa hasa kutokana na maeneo hayo katika wilaya za Mbinga na Nyasa kuwa na utajiri mkubwa wa madini, hususan makaa ya mawe.
Zinazofanyiwa upembuzi yakinifu
Kuna barabara takriban 23 ambazo zimefanyiwa au zinaendelea kufanyiwa upembuzi yakinifu zikiwa na urefu wa jumla ya kilometa 3,342.6, zikiwemo zile ambazo zinahitaji kukarabatiwa kutokana na ‘kuchakaa’.
Miongoni mwa barabara hizo ni Kibaoni – Majimoto – Inyonga (km 162), Mpanda – Ugala – Kaliua – Ulyankulu – Kahama (km 428), Murushaka – Murongo (km 125), Kilindoni – Ras Mkumbi (km 55), Morogoro – Dodoma (km 263), Mwanza – Mwanza/Shinyanga (km 102), Kibaoni – Majimoto – Kasansa – Muze – Kilyamatundu (km 200), Nyehunge – Sengerema (km 68), na Mvuha – Kisaki (km 73).
Nyingine ni Bigwa – Kisaki (km 151), Geita – Nzera – Nkome (km 54), Murugarama – Rulenge – Nyakahura (km 85), Karatu – Mbulu – Haydom – Singida (km 190), Bariadi-Kisesa-Mwandoya-Ngoboko-Mwanhuzi-Sibiti-Mkalama-Iguguno (km 289), Mika – Utegi – Shirati (km 44), Chimala – Matamba – Kitulo (km 51), Upanuzi wa Kitonga Escarpment (km 10), Mbulu – Magugu (Mbuyu wa Mjerumani) (km 63), Mafinga – Mgololo (km 77.6), Babati (Dareda) – Dongobesh (km 60), Liwale – Nachingwea – Ruangwa (185), na Likuyufusi – Mkenda (km 124).
lakini kuna barabara ya Kongwa Ranch – Kiteto – Simanjiro hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa KIA yenye urefu wa kilometa 483, ambayo inaweza kuwa njia ya mkato kwa wasafiri kutoka Dodoma kwenda moja kwa moja Moshi bila kupitia Arusha Mjini wala Babati.
Hii inaonyesha ni kwa namna gani Serikali ya Rais Samia ilivyojipanga kuhakikisha inawarahisishia Maisha Watanzania kwa kuwatengenezea miundombinu rafiki.
Ujenzi wa Madaraja
Tangu ameingia madarakani, Rais Samia amefanikiwa kukamilisha miradi kadhaa ya ujenzi wa madaraja huku akiendelea na ujenzi wa mengine, yote yakiwa ni mapya.
Madaraja ambayo yamekamilika wakati wa utawala wa Rais Samia ni Tanzanite (Salender – Dar es Salaam), Wami mkoani Pwani, na Kitengule mkoani Kagera ambalo linaunganisha linaunganisha barabara kuu ya Kyaka-Bugene-Benako na barabara ya Kagera Sugar Junction-Kakunyu, katika Wilaya za Misenyi, Karagwe na Ngara mkoani Kagera.
Mengine ni Daraja la Msingi (Singida) lenye urefu wa meta 100 lililopo Barabara ya Mkoa ya Kitukutu – Gumanga – Nyahala (Sibiti) inayounganisha Mkoa wa Singida, Mwanza na Mara kupitia Daraja la Sibiti lenye urefu wa mita 82, Daraja la Gerezani (Dar es Salaam), na Daraja la Malagarasi katika barabara ya Kabingo – Kasulu – Manyovu (Kigoma) lenye urefu wa meta 77.
Ujenzi wa Daraja la Kigongo – Busisi maarufu kama Daraja la JP Magufuli linalounganisha wilaya za Misungwi na Sengerema mkoani Mwanza bado unaendelea na kwa sasa umefikia takriban asilimia 90.
Kukamilika kwa daraja hilo lenye urefu wa kilometa 3.2 kutawezesha watu kutumia dakika nne tu kuvuka kutoka upande mmoja hadi wa pili kwa gari, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo wakati mwingine kivuko kilikuwa kinashindwa kusafiri kutokana na uwepo wa magugu maji.
Kukarabati madaraja
Serikali imeanza ujenzi na ukarabati wa madaraja 14 yakiwemo ya Kirumi katika Mto Mara, Pangani (Tanga), Wami Chini (Pwani), Simiyu (Mwanza), Mzinga (Dar es Salaam), Malagarasi Juu katika Barabara ya Buhigwe – Kitanga – Kumsenga (Kigoma), Mkenda (Ruvuma), Mtera Dam (Iringa), Mitomoni (Ruvuma), Ugalla (Katavi), Bujonde (100m) – Mbeya – Sanza (Singida), Upanuzi wa Daraja la Ipyana (Mbeya), na Daraja la Kalebe (Kagera).
Aidha, Serikali pia inakamilisha usanifu wa madaraja ya Malagarasi Chini (Kigoma), Mkundi (Morogoro), Godegode (Dodoma) na Mirumba (Katavi) huku ikiwa tayari imetenga Shs. bilioni 58.288 kwa ajili ya kujenga daraja la Simiyu na daraja la Sukuma mkoani Mwanza. Jitihada hizi za Rais Samia zinaashiria mafanikio makubwa ya kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla, kwa sababu kukamilika kwa miradi hii ya barabara kutawezesha mawasiliano