Hamasa ya teknolojia bunifu ya Rais Samia yawezesha DIT kuja na kifaa cha kuua mbu

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

JITIHADA kubwa zinazofanywa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya 2020-2025 zinaendelea kuzaa matunda.

Hii ni baada ya Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kubuni na kutengeneza kifaa cha kutumia mwanga wa Ultraviolet (UV) kinachojulikana kama ‘Mosquito killer for killing harmful insects’ ili kuua mbu na kupunguza mzigo wa magonjwa yanayosababishwa na mbu nchini.

Wengi tunafahamu kwamba mbu ni mdudu hatari kwa uenezaji wa vijidudu vinavyosababisha ugonjwa wa Malaria, lakini pia wataalamu wanasema anahusika na kueneza magonjwa kama Homa ya Dengue na Virusi vya Zika.

Taasisi ya DIT imefanya kitu muhimu katika kuunga mkono jitihada za Rais Samia, ambaye amekuwa akihamasisha suala la teknolojia bunifu kama sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Na jitihada hizi zitasaidia sana kupunguza maambukizi ya Malaria nchini, ambayo kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, maambukizi hayo yameshuka na kufikia 8.1% mwaka 2023 kutoka 15% mwaka 2015.

Kupungua kwa kiwango hicho cha maambukizi ya Malaria kumetokana na jitihada za dhati za Serikali katika kuhakikisha kiwango cha Malaria nchini kinafikia sufuri kwa kuweka mikakati ya kutokomeza mazalia ya mbu sambamba na kuhakikisha upatikanaji wa Vitendanishi na dawa za kutibu Malaria katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini.

Na tunaambiwa mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Songwe, Manyara, Kilimanjaro, Singida na Mwanza ndiyo inayofanya vizuri kupunguza kiwango cha maambukizi ya Malaria kufikia 1% ingawa katika mikoa ya Katavi, Tabora na Kagera bado kiwango ni kikubwa cha maambukizi kutokana na hali ya kimazingira ya mikoa hiyo.

Ilani ya CCM

Wakati CCM inaomba ridhaa ya wananchi ya kuendelea kuongoza mwaka 2020, iliahidi katika Ibara ya 9(E)(i) na (iv) kwamba itaimarisha na kuhuisha taasisi za utafiti, sayansi, teknolojia na ufundi ili ziweze kubuni nyenzo za kuongeza tija katika sekta za uzalishaji na uhuduma na kwamba itachochea na kuendeleza ubunifu, uvumbuzi na ugunduzi nchini kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Na katika Ibara ya 102(a), (d) na (f), CCM iliahidi kwamba itaimarisha mfumo wa uratibu wa shughuli za sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa uchumi imara na endelevu huku ikiweka kipaumbele katika kujenga na kuendeleza uwezo wetu na kuimarisha matumizi salama ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika maeneo ya kimkakati ikiwemo matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia na maendeleo ya teknolojia ya kidijitali (digital technology), na kuratibu uwekezaji katika maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu, hususan tafiti zinazochochea ugunduzi (invention) na zitakazowezesha nchi kupunguza utegemezi wa teknolojia kutoka nje.

Fauka ya hayo, ikaahidi kujenga mfumo shirikishi na endelevu wa ubunifu (national innovation system) kwa kusimamia kila hatua ya ubunifu ili kuhakikisha ubunifu unakuwa fursa ya kiuchumi na unaongeza tija katika shughuli za uzalishaji na hivyo kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi, na kuibua, kutambua na kuendeleza ubunifu na ugunduzi unaozalishwa nchini kwa ajili ya kutatua changamoto zinazoikabili jamii ya Watanzania.

Haya na mengine mengi ndiyo ambayo Rais Samia amekuwa akiyatekeleza kwa dhati kama CCM yenyewe ilivyoahidi kwenye Ibara ya 10 ya Ilani yake kwamba, itahakikisha serikali zake (ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) zinatekeleza mambo yote yaliyoahidiwa

katika Ilani hiyo kwa manufaa na ustawi wa Taifa, utekelezaji ambao unaongozwa na kauli mbiu ya: “Tumetekeleza kwa Kishindo; Tunasonga Mbele Pamoja” kabla ya Rais Samia kuongezea “Kazi Iendelee”.

Umuhimu wa kifaa hiki

Kifaa hiki kinaelezwa kwamba kimeundwa kuvutia na kuua mbu kwa kutumia njia mbalimbali na kinatumia mwanga na joto kuvutia mbu, kina uwezo wa kuvutia mbu umbali wa mita 90 kwa kutumia mwanga wa urujuani (violet).

Kwamba, kifaa hiki kinaweza kuwekwa ndani ya nyumba, kwenye maeneo ya wazi kama vile hospitali, maeneo ya mapumziko ya wazi nje, kwenye vyuo, shule za bweni au maeneo mengi ambayo yana uwazi ili kuua mbu na kuzuia watu kupata maambukizi ya malaria na magonjwa mengineyo yaenezwayo na wadudu hao.

Wakati wa Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ‘Saba Saba’, Joel Ngushwai, Mratibu kutoka Studio ya Taasisi ya DIT, alisema kifaa hicho kinatumia teknolojia ambayo imekuwa maarufu kwa kudhibiti mbu katika maeneo mbalimbali na aliomba wananchi kukitumia.

Hicho ni kifaa cha kwanza kutengenezwa baada ya kuona kinafanya kazi na tayari walifanya majaribio katika maeneo ya taasisi ya DIT kwa muda wa mwezi mmoja na wamegundua kina uwezo wa kuua wadudu wengi warukao kwa asilimia 95.

“Kwa mtu, chuo au hospitali anayetaka kutumia kifaa hiki kupambana na mbu, kuna njia mbili, njia ya kwanza anaweza kutumia solar na njia ya pili anaweza kutumia umeme wa Tanesco kwa ajili ya kukichaji,” akasema.

Akasema, wameamua kutengeneza kifaa hicho baada ya kuona uwepo wa mbu wengi katika baadhi ya hospitali na vyuo ambapo wagonjwa na wanafunzi wanahangaika kupambana na mbu.

Mbali na Malaria, Homa ya Dengue na virusi vya Zika vimesababisha milipuko kadhaa nchini na kufanya kudhibiti mbu kuwa jambo la kipaumbele.

Homa ya Dengue, inayosababishwa na mbu aina ya Aedes, inaweza kusababisha dalili kali kama vile homa ya ghafla, maumivu ya kichwa na maumivu ya viungo.

Virusi vya Zika, ambavyo pia vinasambazwa na mbu wa Aedes, vinaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya, hasa kwa wanawake wajawazito kwani vinaweza kusababisha kasoro za kuzaliwa kwa watoto.

Ngushwai anasema, kifaa hicho kimekuwa maarufu zaidi kama suluhisho bora la kupambana na wadudu hao kwa sababu hutoa njia rahisi na rafiki wa mazingira katika kupunguza idadi ya mbu katika maeneo ya mijini na vijijini.

Faida kwa jamii

Umuhimu wa kupunguza idadi ya mbu katika jamii unaweza kusaidia kupunguza mzigo wa magonjwa yanayosababishwa na mbu katika jamii na hii itawezesha kupungua kwa idadi ya watu wanaougua magonjwa hayo.

Uwepo wa kifaa hicho utasaidia wananchi na wagonjwa hospitalini kulala kwa utulivu na kupunguza kelele za kuumwa na mbu wakati wa usiku, jambo ambalo ni muhimu kwa watoto na watu wazima wanaohitaji usingizi bora kwa afya bora.

Aidha, kuwepo kwa kifaa hicho kunakupa amani ya akili, kujua kama una kinga dhidi ya mbu na magonjwa wanayoambukiza inaweza kukupa amani ya akili, hasa wakati wa msimu wa mvua ambapo mbu huzaliana kwa wingi zaidi. Lakini pia inakusaidia kuboresha maisha.

“Kuwa na uwezo wa kufurahia wakati wako wa nje bila kusumbuliwa na mbu kunaweza kuboresha ubora wa maisha yako. Hii ni muhimu sana kwa familia zinazopenda kutumia wakati mwingi nje, kama vile bustani, shamba, au kwenye veranda,” anasema Ngushwai.

Kwa muktadha huo, maeneo yenye kiwango kidogo cha mbu yanaweza kuvutia watalii Zaidi na hivyo kusaidia kukuza uchumi wa maeneo hayo na kuboresha maisha ya wenyeji.

“Mtu anayetaka kutumia kifaa hiki kwa ajili ya kuua mbu lazima ahakikishe anakiweka kwenye maeneo yasifikiwa kwa urahisi na watoto wadogo na wanyama vipenzi wa binadamu ili kuepuka ajali zinazoweza kutokea kama vile kugusana na gridi ya umeme au kuangusha kifaa,” anasema Ngushwai.

Jinsi kinavyofanya kazi

Ngushwai anasema, kifaa hicho hutumia mwanga wa urujuani iliyokolea (Ultraviolet – UV) kuvutia mbu, wakati mbu wanaporuka kuelekea kwenye mwanga, wanagusana na gridi iliyo na umeme ambayo inawaua papo hapo.

Njia hii ni bora kwa matumizi ya ndani na nje, lakini mwanga wa UV unaweza pia kuvutia wadudu wengine, hivyo kusaidia jamii kuwaua wale ambao siyo rafiki.

Teknolojia ya kuua mbu kwa kutumia mwanga wa Ultraviolet imekuwa maarufu kwa sababu ya ufanisi wake na faida nyingi zinazohusiana nayo.

Ngushwai anataja sababu kuu za kuchagua kutumia teknolojia ya mwanga wa UV kwa kudhibiti mbu zikiwemo Ufanisi wa Kuvutia na Kuua Mbu, kwani kifaa hiki ni maarufu kwa uwezo wa kuvutia mbu kwa ufanisi mkubwa. Mwanga wa UV huvutia mbu na wadudu wengine wa kuruka kwa nguvu, na wanapokaribia chanzo cha mwanga, wanagusana na gridi ya umeme inayowaua papo hapo.

Hii inamaanisha kuwa unaweza kuona matokeo haraka na kudumu katika kupunguza idadi ya mbu.

Lakini pia kutumia kifaa hiki kunatoa faida nyingi muhimu kwa afya, mazingira na uchumi wa jamii. Miongoni mwa faida hizo ni:

Kupunguza Magonjwa Yanayosababishwa na Mbu: Tanzania ni mojawapo mwa nchi zilizoathirika zaidi na malaria, na pia kuna magonjwa mengine kama Homa ya Dengue na Virusi vya Zika. Kupunguza idadi ya mbu kwa kutumia kifaa hiki kunaweza kupunguza hatari ya maambukizi ya magonjwa haya.

Kuhifadhi Afya ya Watoto: Watoto wako katika hatari kubwa zaidi ya kuathirika na malaria na magonjwa mengine yanayosababishwa na mbu. Kutumia kifaa hiki kuua mbu nyumbani kunaweza kusaidia kulinda afya ya watoto wako.

Kupunguza Matumizi ya Kemikali: Badala ya kutumia viuadudu vya kemikali, ambavyo vinaweza kuwa na madhara kwa afya, kifaa hiki hutoa njia salama na bora ya kudhibiti mbu.

Ukiacha faida hizo za kiafya, kuna faida pia za kimazingira. Vifaa vingi vya kuua mbu vimeundwa kuwa rafiki wa mazingira. Mitego ya asili na mitego ya CO2, kwa mfano, hutumia kivutio kisicho na sumu na kuepuka kemikali hatari, na kuifanya kuwa salama kwa mazingira.

Pia vifaa vinavyotumia nishati ya jua (solar) vinapunguza matumizi ya umeme na kusaidia kuokoa nishati.

Kupunguza matumizi ya dawa za kuua wadudu kutasaidia kupunguza utegemezi wa dawa zenye kemikali ambazo zinaweza kuwa na athari mbaya kwa mazingira na viumbe hai vingine.

Kwa kuepuka matumizi ya kemikali na sumu, kifaa hiki kitasaidia kuhifadhi viumbe hai vingine, kama vile wadudu muhimu wa bustani, ndege, na wanyama wengine wa porini.

Ufanisi wa Gharama

Gharama za Muda Mrefu: Ingawa uwekezaji wa awali katika kifaa cha kuua mbu unaweza kuwa juu kuliko viuadudu vya kawaida, akiba ya muda mrefu ni kubwa.

Kupungua kwa gharama za matibabu kutokana na magonjwa yanayosababishwa na mbu na muda wa maisha marefu wa vifaa hivi huchangia akiba ya jumla.

Kuokoa Gharama za Umeme: Mashine nyingi za hivi karibuni zinatumia nishati ya jua (solar) kama chanzo cha umeme, na hivyo kupunguza gharama za umeme na kuwa rafiki kwa mazingira.

Kupunguza Matumizi ya Vizuia na Viuadudu: Kifaa hiki kinapunguza hitaji la kununua na kutumia vizuia au viuadudu mara kwa mara, na hivyo kuokoa gharama kwa muda.

Urahisi wa matumizi

Kifaa hiki kwa ujumla ni rahisi kusanidi na kinahitaji matengenezo kidogo na kinatoa suluhisho lisilo na matatizo kwa udhibiti wa mbu unaoendelea, na kukuruhusu kufurahia maeneo yako ya ndani na nje bila kero ya mbu.

Matengenezo Rahisi: kifaa hiki kinahitaji matengenezo mengi. Kwa mfano, vianzishi vya umeme vinahitaji kusafishwa mara kwa mara ili kuondoa mabaki ya mbu waliouawa, wakati mitego ya CO2 inahitaji kujazwa tena kwa mitungi ya CO2 mara kwa mara.

Kifaa Kisicho na Harufu: Tofauti na baadhi ya vizuia wadudu vya kemikali ambavyo vinaweza kuwa na harufu mbaya, vifaa vingi vya kuua mbu haviitoi harufu yoyote, na hivyo kuifanya iwe rahisi kutumia ndani ya nyumba na maeneo ya nje.

Utatuzi kama ikitokea changamoto kwenye kifaa hiki

Ikiwa kifaa chako hakifanyi kazi, angalia kama kimeunganishwa vizuri kwenye chanzo cha umeme. Hakikisha nyaya zote ziko salama na kwamba kuna umeme wa kutosha. Ikiwa kifaa chako kinatumia betri, angalia kama betri zina nguvu ya kutosha.

Kama kifaa hakitoi mwanga wa UV, balbu inaweza kuwa imeharibika au kuna tatizo na mfumo wa umeme. Badilisha balbu na uone kama tatizo linaendelea. Ikiwa bado haitoi mwanga, angalia nyaya na vyanzo vya umeme kwa matatizo yoyote.

Ikiwa kifaa chako kinatoa harufu mbaya, inaweza kuwa kuna mabaki ya mbu waliokufa ambao hawajaondolewa kwa muda mrefu. Safisha kifaa vizuri na uhakikishe hakuna mabaki yoyote yaliyobaki kwenye gridi ya umeme.

Kwa kufuata vidokezo hivi vya uwekaji na matengenezo, unaweza kuhakikisha kifaa chako cha kuua mbu kinafanya kazi kwa ufanisi zaidi na kudumu kwa muda mrefu. Kifaa hiki ni uwekezaji muhimu kwa afya yako na faraja yako, na matengenezo sahihi yanaweza kusaidia kupata matokeo bora zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *