Samia alivyowatengenezea fursa Bongo Movie nchini Korea Kusini

Na Daniel Mbega, Dar es Salaam

JULAI 10, 2024, kundi la wasanii wa filamu na tamthilia nchini Tanzania lilirejea kutoka Korea Kusini ambako wasanii hao walikwenda kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya Sanaa ya filamu na tamthilia duniani.

Mwenyekiti wa wasanii hao, Steve Mengele, maarufu kama ‘Steve Nyerere’, kwa niaba ya wenzake, akampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kugharamia safari yao ya siku 10.

Safari ya wasanii hao imekuja baada ya Rais Samia kutangaza neema kubwa kwa wasanii ya kugharamia safari zao pindi atakapokuwa na ziara za kikazi nje ya nchi.

Na itakumbukwa kwamba, Mei 31, 2024, wakati Rais aliposafiri umbali wa kilomita 10,200 kutoka Dar es Salaam hadi Seoul kwa ziara ya siku sita, kwa mara ya kwanza aliandamana na wasanii, lengo likiwa kwenda kubadilishana uzoefu na kuwapa fursa ya kujifunza masuala ya sanaa kwa mataifa yaliyoendelea ili waboreshe kazi zao ziwe za viwango vya kimataifa.

Licha ya kwamba ziara hiyo ilikuwa na mambo mengi yenye fursa kubwa za kiuchumi hasa kwa Tanzania, ambayo pia imeendelea kuimarisha uhusiano wake na Korea Kusini uliodumua kwa miaka 32, lakini kuambatana na wasanii wa filamu lilikuwa ni jambo jema.

Na limekuwa jambo jema zaidi baada ya kugharamia ziara ya mafunzo ya wasanii kadhaa, mwezi mmoja tu baada ya ziara yake ya kiserikali. Miongoni mwa wasanii waliopata fursa hiyo, mbali ya Steve Nyerere, ni makamu wake Idris Sultan, Wema Sepetu, Irene Uwoya, Yvonne Cheryl au Monalisa, Irene Paul, Gertrude Mwita na Godliver Gordian.

Wakiwa huko, rais wa Filamu Korea Kusini, Yang Jongkon, alisema Tanzania imechaguliwa kuwa nchi ya kwanza Afrika kufanya filamu na nchi hiyo ya Mashariki ya Mbali huku akiahidi kuja nchini kuonana na waigizaj wa filamu.

Akizungumza jijini Busan, Jongkon alisema Rais Samia amefanya kazi kubwa ya kuunganisha soko la filamu la Tanzania na Korea.

“Hivyo basi nami sina budi kueleza kuwa Tanzania ndiyo nchi ya kwanza tutakayoshirikiana nayo tutakapoingia Afrika. Kwa sasa tunamalizia kuimarisha bara la Asia kwenye tasnia hii ya filamu,” akasema na kuahidi makubwa kwa wasanii wa Bongo Movie huku pia akisema katika ziara yake ataongozana na baadhi ya watengeneza filamu wa Korea.

Fursa waliyoipata wasanii hao ni kubwa sana, hasa kwa kuzingatia kwamba, Korea Kusini ni ni kiwanda cha tasnia ya filamu tajiri zaidi duniani, ikiwa inashika nafasi ya tano nyuma ya Hollywood ya Marekani na Canada, Bollywood ya India, Chinese Cinema ya China na Uingereza, huku ikifuatiwa na Nihon Eiga ya Japan, Ufaransa, Ujerumani, Australia na Mexico.

Biashara ya filamu ya Korea Kusini ina mapato ya jumla ya takriban dola bilioni 1.7, na kuifanya kuwa tasnia ya filamu ya tano kwa ukubwa duniani. Ilianzishwa mnamo 1945 na tangu wakati huo imekua na kuwa moja ya kampuni maarufu zaidi za filamu ulimwenguni, ikitambulisha ulimwengu kwa aina kama vile K-pop na filamu za kutisha za Kikorea. Sekta ya filamu ya Korea Kusini imekwenda mbali sana tangu kuanzishwa kwake.

Siyo siri kwamba, Korea Kusini ndilo soko la sinema lenye watu wengi zaidi duniani kwa kuzingatia mahudhurio ya kila mtu. Hadi sasa, sekta hiyo imepiga hatua kubwa. Kulikuwa na takribani kumbi 500 za skrini moja katika mwaka 1998, na mauzo ya tikiti ya karibu milioni 50. Lakini kufikia mwaka 2016, mauzo ya tikiti yalikuwa yamepanda hadi milioni 217, na zaidi ya filamu 2,400 zilionyeshwa kwenye kumbi za sinema. Mwaka huo wa 2016, tasnia ya filamu ya Korea Kusini ilileta mapato ya dola bilioni 1.5, na kuiweka nafasi ya saba duniani.

Kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1950 hadi miaka ya 1960, sekta ya filamu ya Korea Kusini ilinufaika kutokana na msisimko wa “kipindi cha Zama za Dhahabu.” Ilizingatiwa sana kuwa ya ubora duni kufikia miaka ya 1970. Ujio wa sheria inayozuia idadi ya filamu za kigeni zinazoonyeshwa katika kumbi za sinema kila mwaka uliinufaisha sana sekta hiyo na Korea Kusini ikawa mojawapo ya mataifa machache mwaka 2005 kuonyesha filamu nyingi za ndani katika majumba ya sinema kuliko filamu za kigeni (zilizoagizwa kutoka nje).

Ukiangalia historia ya filamu hata hapa Tanzania, mbali ya filamu za Hollywood zinazoendelea kutamba, lakini katika miaka ya 1960 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990, filamu zilizokuwa zikitamba kwenye majumba ya sinema ya wakati huo ni za Kihindi au za Kichina.

Wakati huo ukienda Drive-Inn (ulipo Ubalozi wa Marekani), New Chox, Cameo, Avalon, Empire na Empress lazima ukutane na filamu za kibabe kama Bombai Ka Babu iliyochezwa na Dev Anand, Suchitra Sen, Nazir Hussain, Achala Sachdev na Manohar Deepak, na filamu ya Kanoon (Sheria) ya Rajendra Kumar, Nanda, Ashok Kumar, Mehmood, Shashikala, Jeevan na Om Prakash, basi ungekutana na filamu za kimahaba za Usne Kaha Tha (yaani ‘Alisema Hivyo’) ya Sunil Dutt, Nanda, Indrani Mukherjee, Rajendra Nath na Durga Khote, au Dil Apna Aur Preet Parai (yaani ‘Moyo ni wetu na upendo ni wa mtu mwingine’) chini ya uongozaji wa gwiji Kishore Sahu ikiwa imechezwa na Raaj Kumar, Meena Kumari, Nadira, Tun Tun, Helen na Om Prakash.

Zikafuata filamu kali kama Deewaar (Ukuta) ya Amitabh Bachchan, Shashi Kapoor na Nirupa Roy, Muqaddar Ka Sikandar (Mshindi wa Hatima) ya Amitabh Bachchan, Vinod Khanna na Rakhee Gulzar, filamu ya Disco Dancer ya Mithun Chakraborty, Kim na Kalpana Iyer, filamu ya Chameli Ki Shaadi (Harusi ya Jasmine), hadi enzi za Kuch Kuch Hota Hai (yaani ‘Kitu Kinatokea’) ya nyota kama Shah Rukh Khan, Kajol na Rani Mukerji, kutaja kwa uchache tu.

Miaka ya 2000, 2010 na 2020 imeshuhudia ujio wa tamthiliya kutoka Mexico, Ufilipino, Korea Kusini, India, Russia na Uturuki, ambazo zimewateka mashabiki wa Sanaa kote nchini na kuwafikirisha sana wasanii wetu.

Kwa maana hiyo, ziara ya Rais Samia Korea Kusini imefungua fursa nyingi za wasanii wa filamu na tamthiliya nchini Tanzania, ambao sasa baada ya kipindi kifupi cha kuzuru huko wanaweza wakafanya jambo tofauti na mazowea.

Ukiacha kundi la tasnia ya filamu zenye utajiri mkubwa duniani, Korea Kusini inashika nafasi ya sita katika kundi la viwanda vikubwa vya filamu duniani, yaani vinavyozalisha filamu nyingi.

Korea Kusini inatajwa kwa ubora wake katika usimulizi wa hadithi bunifu na nyimbo maarufu za kimataifa.

Kwenye kundi linaloongozwa na Hollywood, kiwanda cha filamu cha Nigeria (Nollywood) kinashika nafasi ya tatu nyuma ya Bollywood kwa kuzalisha filamu nyingi mno.

Sekta ya filamu ya Korea Kusini imevutia hadhira ya kimataifa kwa ubunifu wake wa hadithi za kusimulia, kazi bora za kuchanganya aina na viwango vya juu vya uzalishaji. Filamu kama vile “Parasite” zimepata tuzo za kimataifa, zikiangazia uwezo wa tasnia ya kutoa simulizi za kipekee na za kushawishi.

Inatambulika kwa vichekesho vya kisaikolojia na simulizi za kuvutia za mapenzi, ikiwa inapigwa ‘tafu’ na Serikali ambayo uendelezaji wa tasnia hiyo ni mojawapo ya mipango yake endelevu.

Tamasha la Kimataifa la Filamu la Busan ni jukwaa kuu kwa watengenezaji filamu wa Asia. Waongoza filamu na waigizaji wa Korea wanazidi kupata umaarufu wa kimataifa.

Kwa maana nyingine, ziara ya wasanii hawa wa Bongo Movie kama itatumiwa vyema, au wasanii wenyewe kama watajitambua, wakajikosoa na kuwa na mawazo ya kimataifa, wanaweza kutengeneza filamu na tamthiliya za viwango vya kimataifa, huku pia wakipata jukwaa la kwenda kuonyesha kazi zao huko Korea.

“Tumejifunza namna ya kufanya kazi zetu za kisanii kama njia ya kujiletea maendeleo na kukuza sekta hii nchini Tanzania. Kwa kweli tunampongeza sana Rais Samia kwa kutupa fursa kwenda kujifunza zaidi kuhusu sanaa na tunaamini tulichojifunza huko kitatusaidia katika shughuli zetu,” alisema wasanii hao walipozungumza na wanahabari mwishoni mwa wiki.

Kwa upande wa maboresho ya sekta hiyo, waliiomba serikali kuweka mikakati zaidi kugharamia utendaji kazi wa Sanaa wa Tanzania kama walivyofanya Korea kwa kuweka bajeti ya uandaaji wa filamu zao hali iliyoibua na kuendeleza sekta hiyo.

“Ili kuwa wakubwa na kutangaza makampuni na viwanda vyetu, watumike wasanii wa ndani kutangaza shughuli zao,” alisema Steve.

Matunda ziara ya Rais Samia

Tunafahamu kwamba, katika ziara ya Rais Samia kumekuwepo na faida kubwa, ambapo yeye mwenyewe alishuhudia utiwaji saini wa mkataba mmoja wa mkopo wa masharti nafuu wa dola za Marekani 2.5 bilioni sawa na shilingi 6.5 trilioni, kwa ajili ya miradi ya mendeleo, ikiwemo sekta ya madini, ukilenga ushirikiano kwenye utafiti, uwekezaji na kujenga uwezo wa kuongeza thamani ya madini ya kimkakati hasa ya nickel, lithium na kinywe.

Kama alivyosema Balozi wa Tanzania nchini Korea, Togolani Mavura, nchi 59 zilizoko barani Afrika, Asia na Ulaya zinafaidika na mkopo wa aina hii kutoka EDCF.

Mkopo huo wa dola bilioni 2.5 ni wa masharti nafuu una riba ya asilimia 0.01, unalipwa kwa miaka 40, na una fungate (grace period) ya miaka 25, yaani unaanza kulipa baada ya mwaka wa 26.

Mikopo ya aina hii inaungwa mkono na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu ambaye anasema kwa upande wao wawakilishi wa vyama vya upinzani, hawapingi ukopaji, ila wanapinga mikopo yenye masharti ya kibiashara. Lakini kwa upande wa mikopo hiyo yenye masharti nafuu wanaiunga mkono.

Kwa maana hiyo, ushirikiano kati ya Tanzania na Korea Kusini umeendelea kuiletea maendeleo Tanzania katika nyanja mbalimbali. Kwa sababu Korea imeshiriki katika miradi mingine ya maendeleo nchini ikiwamo ujenzi wa mradi wa maji safi na maji taka Iringa na ujenzi wa daraja la Malagarasi na daraja la Tanzanite.

Kwa upande wa biashara kati ya nchi hizi mbili, pia imeendelea kukua. Kwa mujibu wa Mtandao wa Takwimu za Kiuchumi Duniani (OEC), katika kipindi cha miaka 27 iliyopita, biashara kati ya Tanzania na Korea imekua kutoka dola milioni 17.4 mwaka 1995 hadi dola milioni 344 mwaka 2022.

Mbali na mkataba huo, Rais Samia alishuhudia utiwaji saini wa Hati ya Makubaliano (Memorandum of Understanding-MOU) katika sekta za Uchumi wa Bluu na Madini ya Kimkakati.

Lakini pia alishuhudia kusainiwa kwa Tamko la Utayari wa Kuanza Majadiliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi (Joint Statement on the launch of Negotiation on Economic Partnership Agreement-EPA).

Fedha hizo kwa ajili ya miundombinu ya maendeleo zitatolewa chini ya Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Serikali ya Korea (EDCF) kwa masharti nafuu.

Hii ni mara ya tatu mfuko huo wa EDCF unatoa mkopo wenye masharti nafuu kwa Serikali ya Tanzania kwani mara ya kwanza ilikuwa katika kipindi cha mwaka 2014 hadi 2020 ambapo ilitoa kwanza dola za Marekani milioni 733 ambazo zilitumika kwenye mradi ya ujenzi wa Hospitali ya Taifa ya Mloganzila Muhimbili, Daraja la Maragarasi, Mradi wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA), mradi wa umwagiliaji Zanzibar.

Mara ya pili ni mwaka 2021 hadi 2025 ambapo Korea ilitoa dola bilioni moja kwa ajili ya mradi wa upimaji ardhi kidijitali ambao utawekeza data za viwanja kidijitali kupitia Chuo cha Tekonolojia Kijiditali (DTI) na Ujenzi wa Hospitali ya Miguni Zanzibar ya vitanda 600.

Pia kuna mradi wa dola milioni 230 wa kuijenga upya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambayo itakuwa ni maghorofa. Ujenzi huo unaendelea hadi 2030.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *