Na Mary Mashina
MAMLAKA ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), imatarajia kutangaza vitalu vipya vya uchimbaji mafuta na gesi katika Ukanda wa Pwani hivi karibuni.
Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni, amesema hayo leo wakati alipotembelea Banda la mamlaka hiyo katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba) yanayofikia tamati kesho Julai 13, 2024.
Amesema wamefanya utafiti katika maeneo tofauti nchini na kubaini asilimia 50 ya eneo lote nchini lina miamba tabaka yenye mafuta.
Amesema katika maeneo hayo mengi yako Ukanda wa Pwani, Kati na Nyanda za Juu maeneo ya Mbeya.
“PURA iko mbioni kutangaza maeneo mapya ya uwekezaji nchini kwenye vitalu vya mafuta na gesi na tunashirikiana na wenzetu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),” amesema Sangweni.
Sangweni amesema katika kutangaza fursa hizo wataanza na Ukanda wa Pwani na kisha kuendelea maeneo mengine ukiwamo Singida na eneo la Kyela mkoani Mbeya.
Sangweni amesema katika maonesho hayo wameendelea kuwaelimisha wananchi na washiriki kuhusu kazi na fursa zilizopo kwenye mkondo wa juu wa petroli nchini.