Kweli ya Kaisari anapewa Kaisari hapa Tanzania?

Na Mwandishi Wetu

WIKI hii tumeamka na mjadala wa mgomo wa wafanyabiashara wa Kariakoo, ambapo taarifa zinaonesha tangu Jumamosi iliyopita, kulisambazwa vipeperushi, vikieleza uwepo wa mgomo huo kuanzia Jumatatu, Juni 24, 2024.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Hamisi Livembe, alipohojiwa alisema jumuiya hiyo haijatoa baraka, lakini kwa kuwa taarifa zipo, aliulizia viongozi wa Kariakoo, kwa kuwa hakutoa baraka, jibu likawa hawakuwa na taarifa.

Hata vyombo vya habari katika kupata maoni ya wafanyabiashara Kariakoo bila kuwa na mlengwa mahususi, vilibaini wako wafanyabiashara waliokiri kuwa na taarifa na wako ambao hawakuwa na taarifa.

Imeelezwa pia vipeperushi hivyo vya kuhamasisha mgomo vilisambazwa katika eneo hilo muhimu kwa uchumi wa nchi, vikihamasisha mgomo huo baada ya Kariakoo, usambae mikoani.

Jana kweli athari ya mgomo ikaonekana, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alikwenda na ujumbe wa kukutana nao mezani.

Ujumbe huo ulikuwa muhimu, maana hata kipeperushi cha kushawishi mgomo, hakikuwa na madai mahususi, zaidi ya kuandika kwa ujumla ‘changamoto zetu zote zipatiwe ufumbuzi’.

Maudhui ya kipeperushi hicho, yanamlazimisha Mkuu wa Mkoa kusisitiza kukaa mezani na wafanyabiashara hao maana hayaeleweki, japo kwa baadhi ya vyombo vya habari, wamedodosa na kudai kuna watumishi ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wamerejesha kero kwa wafanyabiashara.

Madai ya kero yanayotajwa ni pamoja na manyanyaso kwa maana ya kukamatwa kwa wateja, faini kwa wasiotoa risiti zimeongezeka na kubambikiwa kodi ama kulipishwa kodi mara mbili kinyume na taratibu.

Lakini imeelezwa kuwa katika msafara wa mamba, kenge nao wapo, kwamba kuna baadhi kweli wana kero, lakini ndani ya mgomo huo huo, kuna wafanyabiashara wanataka kuutumia kukwepa kodi.

Hilo ni jambo ambalo halipingiki, kwani ni tabia ya wafanyabiashara kutafuta upenyo wa kukwepa kodi. Hata waliouliza swali kwa Bwana Yesu kuhusu kodi, aliwajibu ya Kaisari mpe Kaisari na ya Mungu mpe Mungu.

Jibu lile la Bwana Yesu, pamoja na mambo mengine, liliwaumiza wakwepa kodi, maana walikuwepo, kwa kuwa halikuwapa fursa ya kukwepa kodi.

Pamoja na kuwepo baadhi ya wenye nia ya kukwepa kodi, hakuna Mtanzania ambaye hakumsikia Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alivyosema mapema kabisa alipoingia madarakani, kwamba ‘kodi anazitaka, lakini si za dhuluma.’

Kwa kauli ile, ni wazi Dkt. Samia alifungua milango kwa wafanyabiashara ambao wana kero za kweli, kuzifikisha mezani, ndio maana Mkuu wa Mkoa, amefika na ujumbe wa kukutana mezani.

Sasa kuwepo kwa milango hiyo wazi halafu wenye kero wakashindwa kuingia, ni suala linalotia ushawishi wa kuwepo kwa zaidi ya kero, ambalo ni siasa. Hili kimsingi halikubaliki popote ndio maana pia ya lile neno la Bwana Yesu, ‘ya Kaisari mpe Kaisari’.

Dunia nzima hakuna Taifa linaloongozwa bila kodi, hivyo kuwepo kwa wakwepa kodi na au wanaotumia siasa, ili kudhoofisha ukusanyaji wa kodi, hakukubaliki duniani na hata Mbunguni.

Nasema hivyo kwa kuwa, huko duniani wakitangazwa watu wanaolipa kodi, Watanzania hatupo na kwa kweli hata Afrika Mashariki, hatuonekani.

Tasnia ya kodi inatumia vipimo ambavyo vinatambulika na kukubalika duniani, ikiwemo kiwango kinacholipwa na wafanyabiashara, wazalishaji na wananchi kuwa kodi, katika mapato yote wanayoyapata katika biashara au uzalishaji au ajira (Pato la Taifa au GDP).

Katika Kipengele cha 7, Kipengele Kidogo cha (IV) cha Makadirio ya Bajeti ya 2024/2025 yanayojadiliwa bungeni hivi sasa, kipimo hicho kimetajwa na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba.

Kipengele hicho chenye kichwa cha habari, ‘Shabaha ya Uchumi Jumla’, kinasema “Mapato ya kodi kufikia asilimia 12.9 ya Pato la Taifa mwaka 2024/25 kutoka matarajio ya asilimia 12.6 mwaka 2023/24.”

Tafsiri yake ni kwamba kiwango kinacholipwa na wafanyabiashara, wazalishaji, wafanyakazi na wananchi kuwa kodi mwaka jana, ni asilimia 12.6 ya mapato yao yote, yaani GDP, ambapo Serikali inapendekeza kifikie asilimia 12.9 katika mwaka wa fedha unaoanza Julai Mosi mwaka huu.

Sasa tujilinganishe duniani, ili tujiridhishe kama kweli agizo la ‘Ya Kaisari apewe Kaisari’ linatimizwa katika nchi hii.

Kwa mujibu wa Mtandao wa Wikipedia kwa takwimu za 2020, nchi iliyoongoza kwa kupata asilimia kubwa ya kodi kutoka katika GDP ni Ufaransa, ambako ni asilimia 46.2; inafuata Denmark (46.0%) na Ubelgiji (44.6%).

Kwa nchi za Afrika anayeongoza ni Ushelisheli (31.7%) ikifuatiwa na Djibouti (30.8%) na Namibia (30.1%).

Kwa Afrika Mashariki, Kenya ndiye anayeongoza (18.1) wa pili Rwanda (16.6) na Uganda (13.1). Tanzania japo ni uchumi wa pili kwa ukubwa, lakini hatupo katika nchi tatu za Afrika Mashariki zinazolipa kodi. Tumuogope Mungu!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *