Ripoti za kidemographia na kiuchumi kutatua changamoto za kijamii nchini

Na Mary Mashina, Dar es Salaam

WIKI iliyopita serikali imezindua Ripoti za Kidemografia, Kijamii, Kiuchumi na Mazingira zilizotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 Chapisho Namba Nne pamoja na ripoti ya kina iliyotokana na taarifa zilizokusanywa katika Sensa ya Majengo nchini mwaka 2022.

Ripoti inayohusu majengo yote ni ya kwanza kutolewa nchini tangu kuasisiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.

Akizindua ripoti hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, anawataka watendaji wote wanaohusika na sera na mipango katika Serikali Kuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wahakikishe kuwa mipango na maamuzi yote yanayohusu maendeleo ikiwamo utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi yanazingatia matokeo hayo ya sensa.

Anaagiza pia sensa kutumika kikamilifu katika kubaini na kutatua changamoto zinazoikabili jamii yetu kwa namna ambayo ni endelevu.

Nirudie kusisitiza kuhusu umuhimu wa matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi katika ngazi zote za utawala wakati tunapopanga mipango na programu za maendeleo ya wananchi.

Matumizi ya matokeo hayo ni ya kila Mtanzania kwa kuwa ni mali ya umma. Hivyo, mkakati wa uelimishaji umma katika maeneo mbalimbali uendelezwe.

Aidha, anawataka maofisa masuuli wote kuhakikisha utekelezaji wa vipaumbele vilivyoanishwa kwenye bajeti uzingatie uhalisia wa takwimu zilizobainishwa katika sensa. “Ninatambua bajeti imezingatia sensa hivyo ninasisitiza utekelezaji wake pia ujikite katika uhalisia wa takwimu zilizopo.”

Majaliwa pia anatoa wito kwa asasi za kiraia, mashirika ya kimataifa, mashirika yasiyo ya serikali na sekta binafsi kwa ujumla kutumia taarifa za matokeo ya sensa katika upangaji wa mikakati yao. “Hii itawezesha kuongeza kasi ya usambazaji huduma kwa wananchi badala ya kurundika afua zote katika eneo moja kuzingatia idadi ya wahitaji.”

Kadhalika anawataka wanazuoni, wanataaluma na watafiti kutimia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 katika kufanya shughuli zao za kitaaluma.

Anaeleza kuwa, taarifa zilizopo zimegusa maeneo muhimu ambayo yatakuwa na mchango mkubwa katika uandishi wa makala, ufundishaji na ujifunzaji na uthibitishaji wa nadharia za kitaaluma.

Elimu

Majaliwa anasema baadhi ya matokeo muhimu katika ripoti za takwimu za msingi alizozitaja zimedhihirisha matokeo chanya ya utekelezaji wa mipango ya kimkakati inayofanywa na serikali mbili katika sekta mbalimbali.

“Matokeo yameonesha kuwa tumepiga hatua kubwa katika sekta ya elimu. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, kiwango cha kujua kusoma na kuandika kwa watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kimeongezeka hadi asilimia 83.0 mwaka 2022 kutoka asilimia 78.1 ilivyokuwa mwaka 2012,” anaeleza.

Nishati safi

Majaliwa anasema matumizi ya nishati safi kwaajili ya kupikia yameongezeka nchini ambapo, kaya zinazotumia umeme kwaajili ya kupikia zimeongezeka kutoka asilimia 1.6 mwaka 2012 hadi asilimia 4.3 mwaka 2022 na gesi kutoka asilimia 0.9 mwaka 2012 hadi asilimia 9.4 mwaka 2022.

Anasema kwa upande mwingine, idadi ya kaya zinazotumia kuni kwaajili ya kupikia zimepungua kutoka asilimia 68.5 mwaka 2012 hadi asilimia 55.5 mwaka 2022.

“Haya ni mafanikio makubwa katika uhifadhi na utunzaji wa mazingira. Sote tunafahamu kuhusu madhara yanayosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa ambayo ni pamoja na kuchangia ongezeko la athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, athari kwa afya za watumiaji pamoja na kuleta athari nyingine za kiuchumi katika jamii,” anaeleza Majaliwa.

Maji, Mazingira

Anasema katika hatua nyingine, sekta ya maji na mazingira imeendelea kufanya vizuri ambapo matokeo ya sensa yanaonesha kuwa asilimia 70.1 ya kaya zote zinatumia maji kutoka katika vyanzo vilivyoboreshwa.

Kadhalika anasema asilimia 60.2 zinatumia vyoo vilivyoboreshwa. “Hili ni jambo la kujivunia saa.”

“Nimetaarifiwa kuwa ripoti zimesheheni taarifa za kina zaidi na zimebainisha kwa kina ya hali ya nchi yetu katika nyanja za kijamii, kiuchumi na mazingira ikiwa ni pamoja na hali ya majengo ya makazi na yasiyo ya makazi,” anasema Majaliwa.

Faida za matokeo ya sensa

Anatoa pongezi nyingi kwa watendaji wote kwa kuwa, ripoti hizo zimekamilika kwa wakati muafaka kwa kuwa nchi yetu imo katika kipindi cha mpito cha mipango ya maendeleo.

“Kama mnavyofahamu, hivi sasa nchi yetu inaendelea na mchakato wa kutathmini utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050.

“Matokeo haya na mengine ya Sensa ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo na Sensa ya Anwani za Makazi ya Mwaka 2022 yana nafasi ya kipekee katika kusaidia tathmini na kufanya maandalizi thabiti ya dira hizo kwa manufaa mapana ya Watanzania wote.

“Kama mnavyofahamu serikali katika pande zote mbili za muungano imekuwa ikisisitiza kuhusu kuimarisha masuala ya ufuatiliaji na tathmini. Hivyo basi, matokeo ya Sensa yataendelea kutumika katika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya nchi yetu ya muda mfupi, muda wa kati, na muda mrefu kama vile Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Mwaka 2021/22 -2025/26 na Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar wa Mwaka 2021/22-2025/26,”anasisitiza Majaliwa.

Anasema matokeo hayo yametumika kikamilifu katika kutayarisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/25, hivyo anaamini bajeti imegusa uhalisia wa mahitaji ya wananchi katika nyanja zote.

Waziri Mkuu Majaliwa, anasema matokeo ya takwimu za sensa yaliwezesha serikali kuchukua hatua za haraka na madhubuti katika kubainisha kiwango cha madhara yaliyotokana na majanga ya maporomoko ya udongo yaliyotokea katika Wilaya ya Hanang, Mkoani Manyara na mafuriko katika Wilaya ya Rufiji iliyoko Mkoani Pwani.

“Taarifa ziliwezesha kuandaa mikakati ya kuwafariji wananchi walioathirika. Mafanikio hayo yote yametokana na uwapo wa matokeo ya takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ambazo zimeunganishwa na takwimu za Sensa ya Majengo na Anwani za Makazi.

Kwa maneno mengine, ripoti hizi zina mchango mkubwa katika kutunga na kuhuisha sera mbalimbali zinazohusiana na masuala ya ustawi wa wananchi ikiwamo uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.

Anasema matarajio ya serikali kuona mipango yote katika ngazi zote za utawala ikiwamo ya kibajeti inazingatia uhalisia unaotokana na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi na Sensa ya Majengo ya Mwaka 2022.

“Nasisitiza jambo hili kwa kuwa tukifanya hivyo sio tu itatuwezesha kutumia rasilimali tulizonazo kwa ufanisi itatuwezesha kuona au kupata thamani halisi ya takwimu zitokanazo na sensa ambazo ni hazina kubwa kwetu kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali,” anasema. 

Sensa ya majengo

Majaliwa anasema kwa mara ya kwanza, mwaka 2022 serikali ilifanya Sensa ya Majengo sambamba na Sensa ya Watu na Makazi na Sensa ya Anwani za Makazi.  Sensa hiyo, imeifanya Tanzania kuwa moja ya nchi chache Barani Afrika ambazo zimeweza kufanya mazoezi hayo makubwa ya Kitaifa kwa pamoja.

Anasema viongozi na wageni waalikwa, sina shaka mtakubaliana nami kuwa matokeo yaliyobainishwa katika Ripoti ya Takwimu za Msingi za Sensa ya Majengo ni muhimu sana kutokana na sababu zifuatazo:

Anasema sensa ya majengo itasaidia kuongeza ufanisi katika maeneo mbalimbali ya sekta ya nyumba ikiwa ni pamoja na kukusanya maduhuli ya serikali hasa kodi za majengo kupitia mita namba za umeme zilizokusanywa wakati wa zoezi la Sensa ya Majengo.

Anasema uhuishaji wa kanuni za mipango miji Tanzania Bara hususani viwango vya kupanga ukubwa wa maeneo kwa matumizi ya ardhi na makundi ya matumizi na madaraja ya matumizi ya ardhi zote za mwaka 2024,

Anasema pia kuhuisha taarifa za umiliki, matumizi ya jengo, namba za simu za wamiliki na majira nukta ya majengo husika.

Vilevile, kanzidata ya sensa ya majengo itatumika kuhuisha mfumo wa ‘Integrated Land Management Information System’ (ILMIS) kwa ajili ya kuimarisha ufuatiliaji na utekelezaji wa sera mbalimbali za sekta ya nyumba.

Anasema pia matokeo hayo, yatachagiza juhudi kubwa zinazofanywa na serikali katika kuboresha maisha ya wananchi.

“Kama mtakumbuka nchi yetu haikuwa na takwimu za uhakika za majengo, lakini kupitia Sensa ya Majengo tumeweza kubaini idadi ya majengo yote nchini. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo nchi yetu ina majengo milioni 14.3,” anasema Majaliwa.

Anaeleza zaidi kuwa, kati ya majengo hayo milioni 13.9 yapo Tanzania Bara na takribani majengo 400,000 yapo Zanzibar.

Aidha, anasema asilimia 94.4 ya majengo yote siyo ya ghorofa. Isitoshe, majengo tisa kati ya kumi ni kwa ajili ya makazi na asilimia 3.4 ya majengo ni ya makazi na biashara.

Anwani za makazi

Majaliwa anasema matokeo ya sensa zote tatu, yaani Sensa ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo na Sensa ya Anwani za Makazi yamewezesha Mfumo wa Anwani za Makazi.

Anasema mfumo huo umeweza kutoa barua za utambulisho wa mkazi kidijitali, kurahisisha utoaji wa anwani za makazi katika majengo mapya yanayoendelea kujengwa nchini; kuwezesha taasisi za serikali kutumia taarifa za Anwani za Makazi, kufanya uhakiki na kuboresha taarifa zilizokusanywa wakati wa operesheni Anwani za Makazi pamoja na kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa kidijitali.

“Kutokana na maelezo hayo yote, sina shaka nyote mtakubaliana nami kuwa matokeo ya sensa zote tatu, yamekuwa na tija sana katika kupanga, kupima na kutathmini utekelezaji wa sera na mipango mbalimbali ya maendeleo ya nchi yetu tuliyojiwekea,” anasisitiza.

Mataifa mengine yajifunza

Majaliwa anasema kupitia utekelezaji wa Sensa ya kidijitali ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo na Sensa ya Anwani za Makazi ya Mwaka 2022, Tanzania imetoa mchango wa uzoefu wake katika kufanikisha sensa za nchi nyingine Kikanda na Kimataifa.

“Ninawapongeza sana wataalamu wetu kwa kuwa ninafahamu, jirani zetu wakiwamo Uganda walifika nchini kwetu kujifunza namna tulivyofanikisha sensa kwa weledi na wakatualika kwenda kushauri namna bora ya utekelezaji wa sensa yao ya kidijitali iliyofanyika mwezi Mei, 2024. Ninawapongeza sana kwa utaratibu huo mzuri wa kubadilishana uzoefu kwa wataalamu kutoka nchi za jirani,” anasema.

Anasema Tanzania imeshaalikwa mara kadhaa na Umoja wa Mataifa kutoa uzoefu wake katika utekelezaji wa Sensa ya kidijitali katika kuzisaidia nchi nyingine ambazo zilikuwa zinajiandaa kufanya sensa zao katika mzunguko wa miaka ya 2020 ya Umoja wa Mataifa wa Kufanya Sensa, ambao ulianza mwaka 2015 na utaisha mwaka 2024.

Aidha, anasema Tanzania ni miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Kitaalamu ya Umoja wa Mataifa inayohuisha Kanuni na Mapendekezo ya Umoja wa Mataifa wa kufanya Sensa.

“Kanuni na Mapendekezo hayo yatawasilishwa kwenye Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Takwimu na baadaye kwenye Kikao cha Umoja wa Mataifa cha Wakuu wa Nchi na Serikali kwaajili ya kuridhiwa,” anasema Majaliwa.

Anasema licha ya hayo, sensa hiyo imetoa fursa ya ajira kwa wataalamu wetu wa teknolojia ya habari katika Bara la Afrika kwa nchi ambazo zinaendelea na utekelezaji wa sensa zao za kidijitali kama vile Namibia, Nigeria, Zambia na Uganda.

“Mambo yote hayo yamewezekana kutokana na utashi mkubwa wa siasa wa viongozi wetu wakuu katika masuala ya takwimu. Viongozi wetu wamekuwa tayari wakati wote kutuwezesha upande wa rasilimali, pamoja na kutoa miongozo makini ambayo imetufikisha katika hatua hii ya mafanikio makubwa tunayojivunia ndani ya nchi yetu, kikanda na kimataifa,” anasema Majaliwa.

Mwongozo wa matumizi yake

Majaliwa anasema kazi zinazoendelea zimeelezwa kwa ufasaha ikiwamo utekelezaji wa Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.

“Sina shaka sote tumeshuhudia namna ambavyo serikali inatekeleza Mwongozo huo ambao ni maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa wakati alipokuwa akizindua matokeo ya mwanzo ya Sensa mwezi Oktoba, 2022.

“Kama mtakumbuka, Rais Samia alisisitiza kuhusu usambazaji, uhamasishaji na mafunzo ya matumizi ya matokeo ya sensa ili kuhakikisha yanatumika kikamilifu katika mipango ya maendeleo katika ngazi zote za utawala,” anasema.

Aliwapongeza na kuwashukuru “makamisaa wa sensa kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha mwongozo unatekelezwa kikamilifu kulingana na mpangokazi wake.

Nimetaarifiwa kuwa makundi mbalimbali katika jamii zetu tayari yamefikishiwa matokeo ya sensa na kupewa mafunzo ya namna ya kuyatumia katika shughuli zao za kila siku.

Makundi hayo ni pamoja na viongozi na watendaji wa serikali katika ngazi mbalimbali za utawala. Nimefarijika sana kusikia kuwa matokeo hayo yamekuwa chachu katika mijadala na hoja zenye tija zaidi katika maendeleo ya nchi yetu.

Uzinduzi huo, ulihudhuriwa na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar na Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa; Hemed Suleiman Abdulla, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu; Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Hamza Hassan Juma.

Wengine ni Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Zanzibar, Saada Mkuya Salum, wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Mliopo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *