Samia halisi sasa amesimama imara

Na Daniel Mbega, Dar es Salaam

“NITABAKI kiziwi, siwasikii! Ninachotaka ni mageuzi ya kiuchumi ndani ya nchi na si kingine.” Ni maneno mazito ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyatoa Jumanne, Juni 11, Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akipokea Gawio la Serikali kutoka kwa Mashirika ya Umma na Tasisi ambazo Serikali inamiliki hisa.

Na akasema hajawahi kusikia Waziri wa Fedha amesifiwa bali siku zote analalamikiwa, hivyo akamtaka Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, naye ategemee kupokea lawama hizi hizo anapotekeleza majukumu yake.

“Mimi kazi mliyonipa ninasimama na kuifanya, lakini mnashuhudia matusi ninayotukanwa. Mpuuzi, hana maana huyu bibi, eeeh! Ana hivi. Mambo tele, lakini ninajigeuza nani? Chura,” akasema.

Akaendelea: “Kulikuwa na mashindano ya chura, wamewekewa mlingoti wakaambiwa atakayefika juu ana zawadi. Vyura wakaanza kupanda mmoja mmoja. Sasa huku chini watazamaji wakawa wanawaambia ‘nyie mtaanguka shukeni, ninyi hatari hiyo, hamwezi kufika shuka mtashindwa tu.’ Kelele nyingi kama zinazopigwa humu ndani kwenu.

“Kwa hiyo vyura wakaanza kushuka mmoja mmoja akabakia mmoja tu. Akapanda mpaka juu, akaenda na akateremka. Kama kawaida wakaanza kumzonga ‘umewezaje kufika?’, kumbe yule chura hasikii.

“Kwa hivyo zile kelele zote alizopigiwa yeye kapanda juu na mlingoti wake, na mimi nimejigeuza vivyo hivyo chura. Kelele nyingi zinapigwa, wakiona hujibu wanasema tulitukane atajibu. Sijibu, nageuka chura sisikii kabisa. Ninachotaka ni mageuzi ya kiuchumi ndani ya nchi hii, sitaki kingine,” akasema.

Kauli hii ina mandiki kubwa hasa kutokana na jinsi Rais Samia anavyopambana kutekeleza miradi mingi ya maendeleo bila kujali kelele zinazopigwa na wapinzani ambao wengi wao malengo yao ni kukwamisha jitihada zinazofanywa.

Na Rais Samia akaenda mbali alipowaambia watendaji wa mashirika ya umma kwamba, kwenye mageuzi watakanyaga ‘Nguru wa Mshihiri’ huku akiwaonya anayetaka kumkera amkanyagie uchumi wake.

“Lakini katika mageuzi haya tutakanyaga wengi, wale ambao hawataki kwenda mbele na ndio watakaopiga kelele nyingi sana. Sasa ndugu yangu, mwanangu wewe kwenye shirika ambaye hutaki kukanyagiwa nguru wako, nenda kachape kazi. Leta mageuzi kwenye shirika lako, chapa kazi tuone tija. Hatutakanyaga nguru wako. Kama unanikanyagia mimi nguru wangu wa uchumi na mimi nitamkanyaga wako. “(Kwenye) kelele tujigeuze chura, tuzibe masikio, tupande mti mpaka tukishuka ndiyo tutasema hivi mlikuwa mnasemaje vile? Lakini letu limeshakuwa,” akasisitiza.

Kurejesha uwekezaji

Kasi aliyoingia nayo madarakani Rais Samia katika kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji kwa sekta binafsi, imetoa matunda bora kulingana na takwimu za Benki Kuu.

Taarifa za BoT za mwaka 2023 zinaonesha kuwa sasa sekta binafsi zinachangamkia mikopo katika benki za biashara, hali inayochochea uzalishaji, kukuza uchumi na kuongeza ajira, ambayo mara ya mwisho ilionekana mwishoni mwa 2015 na mwanzoni mwa 2016.

“Wastani wa ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi umefikia asilimia 22.2,” ilieleza Taarifa ya Fedha ya BoT.

Uchunguzi unaonyesha kwamba, mwanzoni mwa 2016 sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi yoyote ilianza kusinyaa hapa nchini, na hali hiyo ilijidhihirisha kwa sekta hiyo kususia mikopo iliyokuwa ikitolewa na benki na taasisi za fedha.

Kusinyaa huko, kulingana na taarifa ya 2017 kunakoashiria kupungua kwa shughuli za biashara, uwekezaji na hata kufungwa kwa baadhi ya biashara, kulisababisha utoaji wa mikopo kutoka juu ya asilimia 22 mwanzoni mwa 2016, hadi chini ya asilimia tatu mwaka 2017.

Wakati Dkt. Samia alinaingia madarakani Machi 19, 2021, alikuta kusinyaa kwa sekta binafsi kukiendelea, kwani uchukuaji mikopo ulikuwa chini ya asilimia tano.

Lakini mageuzi makubwa ya uchumi yaliyochukuliwa na uongozi wake, katikati ya mdororo wa uchumi uliosababisha na janga la Uviko-19, ilipofika Oktoba mwaka 2021, miezi nane baadaye, sekta binafsi ilianza kujikongoja kutoka ilikokuwa ikichungulia kaburi.

Takwimu za BoT zinaonesha kuwa, tangu sekta hiyo ilivyoanza kunyanyuka Oktoba 2021, ongezeko la mikopo linaloashiria ongezeko la uwekezaji, halikuwahi kushuka hadi kufikia juu ya asilimia 22 Aprili 2023, licha ya Dunia kuathiriwa na Vita ya Ukraine inayoendelea.

“Ongezeko kubwa la mikopo limetokana na mahitaji makubwa ya mikopo kwa sekta binafsi, ambayo ni ishara ya ubora wa sera za uwekezaji na mazingira mazuri ya kufanya biashara, yaliyowezeshwa na sera bora za fedha na kodi,” ikaeleza ripoti hiyo.

Katika uchambuzi wa kisekta, sekta ya biashara ndogo ndogo, biashara ndogo na za kati, ndiyo iliyoongoza kwa kuchukua asilimia 38.6 ya mikopo yote iliyotolewa kwa sekta binafsi.

Sekta iliyofuata ni kilimo, ambayo imechukua asilimia 36.1 ya mikopo yote iliyotolewa kwa sekta binafsi, hali iliyoashiria kwamba uamuzi wa Rais Samia, wa kutenga dirisha la maalumu la mikopo ya kilimo, lenye fedha zinazofikia Sh trilioni moja, umekubaliwa na sekta binafsi.

Ongezeko la utoaji mikopo linatarajiwa kuendelea kuimarika zaidi kutokana na hatua zinazoendelea kuchukuliwa za kuboresha mazingira ya biashara, huku zikiwezeshwa na sera ya fedha na sera ya kodi.

Mabadiliko yamekuja

Akiwa nahodha wa meli ya ‘MV Tanzania’, Samia aliamua jinsi ya kuvuka maji haya yanayoweza kuwa ya usaliti, na ndiyo maana ameeleza kwamba ameamua kuwa kimya bila kujibu lolote na badala yake yeye anaendelea kuchapa kazi ili kuwaletea Watanzania maendeleo.

Inafahamika kwamba, katika historia ya kisasa ya kisiasa, mwisho wa kipindi cha fungate ya rais mara nyingi hutoa fursa ya ukosoaji mkali, upinzani, na hata uhasama. Mambo haya yalijirudia mara baada ya kushika madaraka.

Katika siku zake 100 za kwanza za kuvutia ofisini, Samia alieleza agenda yake ya maendeleo ya “kuchanganya mabadiliko na mwendelezo”.

Ameendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika miradi mikuu ya miundombinu huku akifanya uboreshaji wa sera za kigeni, mazingira ya biashara, haki ya jinai, na uhuru wa viwango tofauti vya mafanikio.

Samia amesifiwa sana kwa kushirikisha tena washirika wa kikanda na kimataifa na kuanza kurejesha ahadi za kihistoria za Tanzania kwa ushirikiano wa kimataifa baada ya mtangulizi wake kwa ujumla kujiondoa duniani.

Walakini, ni kwa upande wa nyumbani ambapo amekuwa akikabiliwa na maumivu ya kichwa yanayomsumbua zaidi. Wakati Samia amedhamiria mabadiliko katika mwelekeo wa nchi kutoka katika siasa za chuki, ubaguzi, na kupungua kwa nafasi ya haki na uhuru, baadhi ya wanachama wa chama chake na serikali wamejiondoa kupinga mageuzi hayo.

Lakini sasa amesema hasumbuki na wanaopinga jitihada zake bali atawajibu kwa matokeo chanya.

Mapema katika urais wake, Rais Samia alitaja methali maarufu ya Kiafrika: “Ukitaka kwenda haraka nenda peke yako. Ikiwa unataka kwenda mbali, nenda na wenzako.”

Kwa maneno hayo machache, Samia alibadili vyema mwelekeo wa sera ya mambo ya nje ya Tanzania kutoka katika mtazamo wa ndani uliopitishwa tangu mwaka 2016, kurudi kwenye mtazamo wa nje, mtazamo wa kimataifa uliofuatwa na Tanzania tangu uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1961.

“Hatuwezi kujitenga kama kisiwa,” alisema Rais Samia.

Mafanikio yanaonekana

Katika kipindi cha miaka mitatu ya utawala wake, kuna mengi ambayo Rais Samia ameyafanya kwa mafanikio makubwa.

Kwa mfano, katika kipindi hicho, Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha miradi 25 ya barabara za lami zenye urefu wa kilometa 1,198.50.

Aidha, katika kipindi hicho, jumla ya barabara 57 zenye urefu wa kilometa 3,794.1 ziko hatua mbalimbali za utekelezaji.

Kadhalika, miradi ya ujenzi wa madaraja makubwa nane umekamilika huku miradi mitano ya ujenzi wa madaraja ikiendelea kutekelezwa na ipo katika hatua mbalimbali.

Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa kielelezo wa ujenzi wa Daraja la J. P. Magufuli (Kigongo – Busisi) mkoani Mwanza lenye urefu wa mita 3,200 kwenye Ziwa Victoria likiunganisha mji wa Mwanza na mikoa ya Geita na Kagera.

Kwa upande wa Sekta ya Madini, katika kipindi cha kuanzia Machi 2021 hadi Februari 2024, Wizara ya Madini imefanikiwa kuiendeleza sekta kwa namna mbalimbali ikiwemo kukusanya maduhuli yatokanayo na ada mbalimbali, mirabaha, faini na penati na kufikisha kiasi cha jumla cha Shs. trilioni 1.93.

Awali, mwaka 2021/22 ilikuwa Shs. bilioni 591.5 lakini hadi kufikia mwaka 2023/24 imefikia Shs. bilioni 690.4.

Katika kipindi cha Machi 2021 hadi Februari 2022 mauzo ya madini mbalimbali yalikuwa Shs. bilioni 157.34 lakini kufikia kipindi cha Machi 2023 hadi Februari 2024 mauzo yamefikia Shs. bilioni 476.8.

Kwenye Sekta ya Utalii ambayo ndiyo inaongoza kwa sasa kwa kuiletea nchi fedha za kigeni, mpaka sasa imeingiza Dola za Marekani bilioni 3.37 (zaidi ya Shs. trilioni 8).

Kimsingi, sekta hii imemrejeshea shukurani Rais Samia kwa juhudi zake binafsi za kutoka ofisini na kwenda kushiriki katika utengenezaji wa filamu ya “Tanzania: The Royal Tour”.

Ni wazi kwamba, sekta hiyo itakua zaidi baada ya kushiriki tena filamu nyingine ya Amazing Tanzania, ambayo kwa Kichina inaitwa ‘Mailii Tansaniya’, ilizinduliwa nchini China Mei 15, 2024 ambayo imemshirikisha tena Rais Samia pamoja na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi wa Zanzibar.

Katika kipindi cha miaka mitatu idadi ya watalii nchini imeongezeka kutoka 922,692 mwaka 2021 walioipatia nchi mapato Dola za Marekani bilioni 1.31 hadi watalii 1,808,205 mwaka 2023 walioingiza Dola bilioni 3.37.

Kwa kuongeza idadi ya watalii wengi baada ya mlipuko wa Uviko-19 Tanzania sasa inashika nafasi ya pili barani Afrika baada ya Ethiopia; na kwa kuongeza mapato makubwa inashika nafasi ya tatu baada ya Morocco na Mauritius.

Tanzania imeendelea kutambuliwa kimataifa na kupata tuzo mbalimbali ambazo ni pamoja na Hifadhi ya Taifa Serengeti kuwa hifadhi bora barani Afrika kwa miaka mitano mfululizo kuanzia mwaka 2019 hadi 2023; Tanzania kuwa nchi ya saba miongoni mwa nchi 18 duniani zilizo bora kutembelewa kiutalii kwa mwaka 2022, Hifadhi ya Taifa Serengeti kuorodheshwa kama eneo maridhawa la kutembelewa kwa mwaka 2023, na Hifadhi ya Taifa Serengeti kushika nafasi ya tatu ya vivutio bora vya asili duniani kwa mwaka 2023.

Kama hiyo haitoshi, Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro imeshinda tuzo mbili za Best of the Best Travelers’ Choice na Africa’s Leading Tourist Destination kwa mwaka 2023.

Kwa jitihada hizi, kwa uchache, Rais Samia anayo haki ya kukaa kimya na kuacha matokeo ndiyo yawajibu wapinzani wake.

Kijijini,

Msanga Ngongele,

Kisarawe.

+255-629 299688

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *