Samia alivyoiwezesha ATCL kurejea angani kwa kishindo

Na Samson Sombi

UHUSIANO mwema wa nchi na mataifa mengine duniani kukuza nakuimarisha sekta ya biashara, utalii na uwekezaji ambazo ni mihimili muhimu sana katika ujenzi wa uchumi wa nchi na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Hakuna nchi duniani inayoweza kujitosheleza kwa kila kitu hasa katika nyanja ya uchumi. Hivyo uhusiano wa nchi moja na mataifa mengine ni muhimu sana katika maendeleo ya pande zote mbili. Ukuaji wa sayansi na teknolojia unatoa wigo mpana wa nchi moja kushirikiana na nchi nyingine katika nyanja mbalimali za maendeleo.

Machi 19, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alikula kiapo cha kuongoza Jamuhuri ya Muungano waTanzania na kuwahakikishia watanania kwamba hakuna litakaloharibika katika uongozi wake huku akihimiza kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa katika harakati za kuleta maendeleo katika nchi yetu.

Katika hatua nyingine, Aprili 22, 2021, Rais Samia alihutubia Bunge la 12 kwa mara ya kwanza na kueleza kwa kina azma ya serikali ya wamu ya sita katika kuimarisha na kudumisha uhusiano mwema na mataifa mengine huku akitoa kipaumbele katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Katika hotuba hiyo Rais Samia alieleza pia mikakati ya serikali kuboresha miundobinu ya usafiri wa anga ikiwa ni pamoja na maboresho ya viwanja vikubwa vya ndege hapa nchini.

“Kuhusu usafiri wa anga serikali itaendelea na maboresho ya viwanja vya ndege kwa kusoma mwenendo wa biashara hii ulimwenguni na kuepukana na mambo yote yasiyo na tija,” alisema Rais Samia.

Ndani ya miaka mitatu serkali imetenga na kutoa fedha za kugharamia kazi kubwa inayoendelea ya upanuzi, ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege katika maeneo mbalimbli hapa nchini.

Aidha kumekuwa na ongezeko kubwa sana la wataalam katika sekta ya usafiri wa anga hatua inayopelekea kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma ndani na nje ya nchi.

Idadi ya watumiaji wa usafiri wa huduma za anga imeongezeka katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Dkt. Samia, huku idadi ya watalii ikielezwa kupaa juu. Idadi ya ndege mpya za kisasa imeongezeka.

Mchango mkubwa wa Rais Samia katika nyanja za maendeleo ya kijamii umeendelea kutambuliwa na mataifa makubwa duniani ikiwamo Korea Kusini ambako Mei 30 hadi Juni 5, 2024 alifanya ziara katika nchi hiyo na kutunukiwa shahada ya udaktari wa heshima (PHD) na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga cha Korea (KAU) kutokana na mchango wake katika sekta ya usafiri wa anga.

Amepata shahada hiyo ya udaktari wa heshima ndani ya kipindi kifupi cha miaka mitatu kutokana na mchango wake katika sekta ya usafiri wa anga nchini,kwa hatua alizochukua hasa wakati na kabla ya mlipuko wa Uviko-19 kama vile kuongeza safari za ndege katika Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL).

Akizungumza baada ya kupewa udaktari huo wa heshima Dkt. Samia alishukuru na kupokea heshima hiyo na kueleza kwamba sekta ya usafiri wa anga imekuwa na umuhimu mkubwa sana katika maendeleo ya nchi.

Alisema ilikuwa ni muhimu kulihusisha Shirika la Ndege na tangu hatua hiyo ilipoanza kuchukuliwa mapato ya ATCL yameongezeka kutoka Shs. 33 bilioni mwaka 2026/17 hadi kufikia Dola 308.4 milioni za Marekani mwaka 2023.

Alisema safari za ndege za kimataifa pia zimeongezeka kutoka 26 mwaka 2016/17 hadi kufikia 33 mwaka 2021, hivyo kuongezeka kwa idadi ya watalii nchini hadi kufikia karibu watalii million mbili wanaotembelea Tanzania.

‘’Ni muhimu kutambua kwamba waendeshaji wa ndani na wasafiri wamekuwa sehemu ya sekta hii kwani takwimu zinaonyesha pia idadi ya wasafiri imeongezeka kwa asilimia 25.6 kutoka abiria milioni tatu kabla ya mlipuko wa Uviko -19 hadi abiria milioni 3.8 kufikia mwaka 2023.’’Alisema Rais Samia.

Rais Samia alisema mwaka 2006 Tanzania ilikuwa na ndege moja lakini hadi sasa ina ndege 14 za abiria, pamoja na ndege moja ya mizigo,Aliongeza kwamba ndege hiyo imeweza  kupanua masafa yake  kutoka mataifa manne  hadi kufikia mataifa 24.

Rais wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga cha Korea, Hee Young Hurr, alisema chuo hicho kina histioria ya miaka 72 na kwamba wamekuwa na ushirikiano na Tanzania hasa kwenye udhamini wa masomo ya shahada ya umahiri.

“Utayari wa Rais Samia kushirikiana katika sekta ya anga hapa kwetu ni mwanzo mzuri wa ushirikiano kati ya Tanzania na Korea. Uongozi wake unavutia na tumeamua kumkutunukia shahada ya udaktari katika usimamizi wa usafiri wa anga,” alisema Hurr.

Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi ya KAU Amidi wa shule kuu Soo Chang Hwang, alisema uogozi wa Rais Samia katika sekta ya anga ni wakipekee na umekuwa na manufaa makubwa ikiwamo kuongezeka kwa idadi ya ndege zinazotua nchini na Kuongezeka kwa idadi ya ndege za ATCL pamoja na mapato.

“Kwa niaba ya bodi ya KAU tunakupongeza na shahada hii ni ishara ya heshima kwako kwa kile unachokifanya na tunatarajia utaendelea kuwa na ushirikiano na chuo chetu.” alisema Hwang.

Rais Samia amepata heshima hiyo huku upanuzi na ukarabati wa viwamja vya ndege ukiendelea kwa kasi kubwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Viwanja hivyo ni pamoja na uwanja wa ndege Kigoma, Mwanza, Pemba, Shinyanga, Songea, Songwe, Sumbawanga na Tabora.

Ujenzi wa kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Msalato,Dodoma utakaogharimu zaidi ya sh 600 bilioni, kazi inaendelea na tayari zaidi ya sh 15.2 bilioni zimeshatumika kulipa fidia wananchi waliopisha maeneo kwa ajili ya mradi huo.

Ni chini ya uongozi wa Rais Samia kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) kimekabidhiwa rasmi kwa mamlaka ya viwanja vya ndege (TAA) kutoka kwa kampuni ya uendelezaji na uendeshaji wa kiwanja cha ndege cha Kilimanjaro (KADCO) ikiwa ni utekelezaji wa azimio la Bunge la Novemba 4, 2022.

Katika hotuba yake ya kwanza kwa Bunge Rais Samia alikwenda mbali zaidi na kusema serikali yake itawekeza katika upatikanaji wa raslimali watu wenye uwezo na weledi wa kutoa huduma bora kwa watumiaji wa huduma za anga.

Tangu wakati huo kwa mujibu wa mamlaka ya usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kumekuwa na ongezeko la wataalamu, mathalani marubani kutoka 234 hadi 603, wakaguzi wa ndege kutoka 28 hadi 44, waongoza ndege kwenye minara kutoka 70 hadi 154 na wataalamu wa taarifa za kianga kutoka 50 hadi 83.

Katika hatua nyingine mashirika ya ndege ya kimataifa kama Air France, Saudi Airline, Elderweis, na Eurowing ambayo yalianza kufanya safari za moja kwa moja nchini katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia ni uthibitisho wa uwepo wa mazingira bora ya uwekeszaji katika sekta ya anga na jitihada mbalimbali za kidiplomasia zinazofanywa na serikali kuvutia wawekezaji nchini.

Agosti 2023 Bunge la Tanzania liliridhia Azimio la Katiba ya Tume ya Usafiri wa Anga Afrika (AFCAC), hatua ambayo itafanya Tanzania kuwa mwanachama wake na kuimarisha mahusiano mazuri ya kidiplomasia na nchi za Afrika katika kukuza uchumi wa nchi yetu.

Machi 25, 2024 Tanzania ilipokea Ndege mpya aina ya Boeing 737-9MAX na kufanya jumla ya ndege mpya 14 huku ndege aina ya Dreamliner na Bombardier Q300 zikiwa mbio kuingia nchini. Ununuzi wa ndege mpya hivi karibuni umeiweka Tanzania katika ramani ya nchi zenye mashirika ya ndege ya umma duniani, yanayotumia ndege za kisasa ikiwemo hiyo ya MAX9 na ndege ya mizigo ya Boeing 737-300E.

Kwa ujumla, sekta ya anga ni muhimu sana katika ulimengu wa sayansi na teknolojia, nampongeza Rais Samia kwa jitihada za kukuza sekta hii kwa maeneleo ya nchi yetu, Watanzania hatuna budi kumuunga mkono.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *