Na Badrudin Yahaya
KIKOSI cha timu ya Simba SC, chini ya Kocha, Abdelhak Benchikha, kinatarajia kuuingia kambini Januari 25 kwa ajili ya maandalizi ya kuendelea michezo iliyobaki ndani ya msimu huu.
Simba wanakabiliwa na mashindano ya Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo kwasasa ipo katika hatua ya makundi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kupitia kurasa zao rasmi za mitandao ya kijamii, Simba itaingia kambini na wachezaji wao wote wa zamani na wapya.
“Kikosi cheti kwa sasa kipo mapumziko, Mungu akipenda tutarejea tena mazoezini Januari 25,” ilisomeka taarifa rasmi ya Simba.
Wachezaji wa Simba walipewa mapumziko hayo mara baada ya kumaliza michuano ya Mapinduzi Cup kwa kufungwa 1-0 na Mlandege katika mchezo wa fainali.
Kikosi hicho kinaporejea mazoezini, kinatarajia kuwa na sura mpya za wachezaji ambao wamesajiliwa katika dirisha la usajili lililofungwa hivi karibuni.
Wachezaji hao ni Edwin Balua, Ladack Chasambi, Saleh Karabaka, Babacar Sarr, Freddy Michael Koublan na Pa Omar Jobe.Pia kwenye dirisha hili Simba, waliwaacha Jean Baleke, Moses Phiri, Shaban Chilunda, Jimmyson Mwanuke, Nassor Kapama na Mohamed Mussa.