Na Badrudin Yahaya
KLABU ya soka ya Simba imefunga usajili wake kwa kishindo baada ya kunasa saini ya mshambuliaji raia wa Ivory Coast, Fredy Michael Koublan akitokea timu ya Green Eagles inayoshiriki Ligi Kuu ya Zambia.
Mshambuliaji huyo hadi sasa ndio kinara wa mabao katika ligi hiyo akiwa amefunga mabao 14 katika mechi 16 alizocheza.
Kuingia kwa mshambuliaji huyo ni mapendekezo ya moja kwa moja ya Kocha, Abdelhak Benchikha ambaye mara nyingi alisisitiza uhitaji wa mshambuliaji imara kwenye timu yake.
Mbali na mshambuliaji huyo lakini pia mapema Simba walitangaza kumsajili mshambuliaji raia wa Gambia, Pa Omar Jobe.
Maingizo ya washambuliaji wawili kwenye kikosi cha Simba yanatoa mwanya wa tetesi za kuachwa kwa washambuliaji wao waliopo kikosini Jean Baleke na Moses Phiri ingawa uongozi bado haujathibitisha.
Simba pia kwenye dirisha hili waliwasajili wachezaji wawili wa Tanzania, Saleh Karabaka na Ladack Chasambi huku pia akiingia kikosini Babacar Sarr ambaye anatajwa kuchukuwa nafasi ya Aubin Kramo.
Kocha Benchikha ambaye aliingia kikosini mwezi Desemba yupo katika mikakati ya kukisuka kikosi chake ambacho bado kipo katika mchuano wa kuwania kuingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.