Na Badrudin Yahaya
TIMU ya Yanga SC, imetupwa nje ya michuano ya Mapinduzi Cup baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa APR ya Rwanda kwenye mchezo wa robo fainali.
Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar, Yanga ndio ilikuwa wa kwanza kufunga bao kupitia kwa Jesus Moloko ambaye alimalizia kazi nzuri ya Clement Mzize kipindi cha kwanza.
Wakati Yanga wakidhani kuwa wanakwenda mapumziko wakiwa kifua mbele, dakika za majeruhi walijikuta wakiwapa nafasi APR kusawazisha bao kupitia kwa Soulei Sanda baada ya makosa kwenye safu ya ulinzi.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na APR walipata mkwaju wa penalti ambayo ilifungwa na Mbaoma Victor.
Baada ya hapo, Yanga ilionekana kukatika hasa kwenye safu ya ulinzi na APR walijikuta wakipata nafasi nyingi nzuri za kufunga hata hivyo hazikutumika vizuri.
Bao la tatu katika mchezo huo, limefungwa na kiungo wa zamani wa Simba raia wa Sudan, Sharif Shaiboub na kuhitimisha safari ya Yanga kwenye michuano hiyo.
Yanga inarejea jijini Dar es salaam ikiwa ni msimu wa tatu mfululizo bila kushinda taji hilo tangu walipofanya hivyo mwaka 2021.
Kesho kutakuwa na mechi mbili ambapo awali kutakuwa na mechi kati ya Singida FG dhidi ya Azam FC na saa 2:15 usiku kutakuwa na mechi kati ya Simba SC dhidi ya Jamhuri katika robo fainali nyingine.