Na Badrudin Yahaya
KLABU ya soka ya Yanga, imeanza michuano ya Mapinduzi Cup kwa kishindo baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Jamhuri katika mchezo wa Kundi C.
Katika mchezo huo, uongozi wa Yanga pia ulichukuwa nafasi ya kumtambulisha mchezaji wao mpya, Augustine Okra raia wa Ghana ambaye amesajiliwa akitokea Klabu ya Bechem United ya nchini kwao.
Yanga ilifunga mabao yote matano kwenye kipindi cha kwanza kupitia kwa Crispin Ngushi aliyefunga mawili, Kibwana Shomari, Clement Mzize na Mahlatse Makudubela ‘Skudu’.
Mchezaji wa Yanga, Ngushi alitajwa kuwa nyota wa mchezo huo na alikabidhiwa kitita cha sh. 500,000 na wadhamini wa tuzo hiyo Shirika la Bima la Taifa (NIC).
Mchezo mwengine wa kundi hilo, ulichezwa saa 10 alasiri ambapo KVZ walitoka sare ya 1-1 na Jamus ambao ni wageni waalikwa kutoka Sudan Kusini.
Msimamo wa kundi hilo, sasa unaonesha KVZ ambao wamecheza mechi mbili wanaongoza wakiwa na alama nne huku Yanga wakifuatia na alama 3, Jamus ipo nafasi ya tatu na alama 1 huku Jamhuri ikishika mkiani bila alama yoyote.
Kesho michuano hiyo itaendelea kwa mechi mbili ambapo saa 10 alasiri Singida FG itacheza na APR huku saa 2 usiku Simba wakishuka dimbani dhidi ya JKU.