Na Badrudin Yahaya
KLABU ya Azam FC, imetangaza kukamilisha usajili wa kipa raia wa Sudan, Mohamed Mustapha kutoka Klabu ya El Merreikh.
Kipa huyo amejiunga na Azam kwa mkataba wa mkopo ambao utatamatika mwisho wa msimu huu.
Mustapha alikuwa langoni wakati El Merreikh inacheza na Yanga kwenye mchezo wa mtoano Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo timu yake ilipoteza michezo yote miwili.
Huyu anakuwa ni mchezaji wa pili kusajiliwa na Azam tangu dirisha la usajili lilipofunguliwa.
Mchezaji wa kwanza alikuwa ni mshambuliaji raia wa Colombia, Franklin Navarro na kwa pamoja wachezaji hao wote wapo Zanzibar kwenye michuano ya Mapinduzi Cup.
Katika idara ya makipa hili linakuwa ni ingizo la tatu kwa makipa wa kigeni, kumbuka Azam wanao makipa wawili Idrisu Abdulah (Ghana) na Ali Ahmada wa (Comoro).
Pia Azam wanae kipa mzawa ambaye walimkuza katika timu yao ya vijana, Zuber Masoud Foba.
Hadi sasa wanafikisha idadi ya wachezaji 14 wa kigeni ukiachilia mbali Issa Ndala ambaye walimtoa kwa mkopo KMC mwanzoni wa msimu hivyo watalazimika kuwapunguza watatu ili kubaki na 12 kuendana na matakwa ya kikanuni za Ligi Kuu Bara.