Ma Badrudin Yahaya
KOCHA wa timu ya Simba SC, Abdelhak Benchikha, ameahidi mabadiliko makubwa katika kipindi hiki ambacho timu itapata mapumziko ya zaidi ya mwezi mmoja.
Simba imekuwa na matokeo ya panda shuka ambapo katika mchezo wao mwisho wa kufunga mwaka wametoka sare ya 2-2 dhidi ya KMC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Sare hiyo ilionekana kumkera Kocha Benchikha ambaye alikiri kuwa timu hiyo inahitaji mabadiliko makubwa ya kimbinu na hata wachezaji.
Katika mapumziko hayo ya zaidi ya mwezi kupisha michuano ya Afcon na Kombe la Mapinduzi, pia kutakuwa na dirisha la usajili la Januari ambapo Simba wanatajwa kuingiza wachezaji wengine wapya huku baadhi wakitarajia kupewa ‘thank you’
“Tunahitaji mabadiliko makubwa, mabadiliko ya kimbinu jinsi tunavyocheza lakini pia na baadhi ya wachezaji,” amesema mara baada ya mchezo dhidi ya KMC.
Benchikha aliingia Simba takribani wiki tatu zilizopita akichukuwa nafasi ya Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ambaye alitimuliwa mwezi uliopita.
Katika mechi alizosimamia kama Kocha Mkuu, Benchikha ameshinda mechi moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika, akitoka sare moja na kufungwa moja. Katika ligi ameshinda mchezo mmoja na kutoa sare moja.