Skudu apiga bao la ‘kideo’ Yanga ikiichapa Mtibwa 4-1

Na Badrudin Yahaya

TIMU ya Yanga SC, imeibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Stephane Aziz KI , ameibuka shujaa baada ya kufunga mabao mawili huku mengine yakifungwa na Kennedy Musonda na Mahtilase Skudu.

Mabao hayo ya Aziz KI, yamemfanya kufikisha mabao 9 na kuwa kinara katika upachikaji mabao hadi hivi sasa.

Wanaomfuatia kwa karibu ni Max Nzengeli wa Yanga, Feisali Salum wa Azam FC na Jean Baleke wa Simba SC wenye mabao 7 kila mmoja.

Ushindi huo, umeifanya Yanga kufikisha alama 27 nyuma ya Azam yenye alama 28 lakini ipo mbele kwa michezo miwili zaidi na Simba ikifuata ikiwa na alama 22.

Pamoja na kuibuka na ushindi huo mnono, Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, amefanya mabadiliko ya wachezaji wapya wanne katika kikosi chake cha kwanza ambacho huwa anakitumia mara kwa mara.

Wachezaji hao ni Kibwana Shomari, Skudu Makudubela, Salum Abubakari na Jesus Moloko ambao ndio wameanza katika kikosi cha kwanza kwa mara ya kwanza msimu huu.

Katika mchezo huo, ambao ulikuwa wa upande mmoja, hadi timu hizo zinakwenda mapumziko, Yanga ilikuwa ikiongoza kwa bao 1-0 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na Aziz KI.

Penalti hiyo ilitokea dakika ya 42 baada ya nahodha wa Mtibwa, Oscar Masai kumchezea faulo Clement Mzize ndani ya eneo la hatari na Mwamuzi, Sadi Mrope aliamuru ipigwe ambapo Aziz KI aliujaza wavuni.

Lakini kipindi cha pili, Kocha Gamondi aliwatoa
Mzize, Dickson Kibabage na Nzengeli na nafasi zao kuchukuliwa na Musonda, Farid Musa na Pacome Zouazou.

Mabadiliko hayo yalizaa matunda na dakika ya 65, Aziz Ki alifunga bao la pili akimpiga tobo beki Masai na kupiga shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni.

Yanga ikiendelea kutawala mchezo na dakika ya 76, Musonda alifunga bao la tatu kwa shuti kali ndani ya eneo la hatari akipokea pasi ya Moloko na mpira kujaa wavuni.

Dakika ya 82, Skudu alipiga shuti nje ya eneo la hatari na kujaa wavuni huku Kipa Makaka akiruka bila mafanikio.

Katika dakika 3 za nyongeza, Seif Karie aliyeingia badala ya Matteo Anthony, alifunga bao la kufutia machozi kwa Mtibwa Sugar na kufanya mchezo kumalizika kwa Yanga kushinda 4-1.

Yanga itashuka tena uwanjani Jumatano kuumana na Medeama SC katika mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *