Kundi la Yanga SC kimataifa ‘halina mwenyewe’

Na Badrudin Yahaya

Mabingwa wa soka nchini Tanzania, timu ya Yanga SC, imevuna alama moja ugenini baada ya kupata matokeo ya 1-1 dhidi ya Medeama kutoka Ghana.

Kwa matokeo hayo, Yanga wameendelea kubaki na rekodi yao ya kutopata ushindi katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Huu ulikuwa ni mchezo wa tatu kwa kila timu kwenye Kundi D ambapo Al Ahly na CR Beluizdad, pia zimetoka 0-0 kwenye mchezo mwengine wa kundi hilo.

Mshambuliaji Jonathan Sowah, amewatanguliza wenyeji kwa kufunga bao kwa njia ya mkwaju wa penalti baada ya mlinzi Dickson Job, kumuangusha Derick Fordjour ndani ya eneo la hatari.

Mbali na bao hilo lakini Sowah alionekana kuwa mwiba kwa walinzi wa Yanga kwani muda mwingi wa mchezo huo, alikuwa akiwasumbua.

Hata hivyo, Yanga walirejea mchezoni kwa kusawazisha bao dakika ya 37 kupitia kwa Kiungo, Pacome Zouzoua ambaye kwa bao hilo anakuwa ameiokoa timu yake kwa mechi ya pili mfululizo baada ya kusawazisha bao pia kwenye mechi dhidi ya Al Ahly wiki iliyopita.

Yanga wanaendelea kubaki mkiani mwa kundi hilo wakiwa na alama 2 lakini matokeo ya suluhu katika mchezo mwengine wa kundi hilo umefanya nafasi kuwa wazi kwa kila timu.

Katika dakika ya 77 ya mchezo, mlinzi wa kushoto wa Yanga, Nickson Kibabage alifunga bao baada ya kupokea pasi kutoka kwa Stephane Aziz Ki lakini lilikataliwa kwa madai ya kuotea.

Kibabage kwenye mchezo huo amepata bahati ya kumalizia dakika 90 baada ya kunusurika kuumia kwenye kipindi cha kwanza baada ya kufanyiwa madhambi hatari na mlinzi wa kulia wa Medeama, Kwadwo Amoako.

Ukiachilia nafasi hiyo lakini pia mshambuliaji wa Yanga raia wa Ghana, Hafiz Konkoni, alipoteza nafasi nzuri kwenye dakika za majeruhi baada ya kuingia akichukuwa nafasi ya Kennedy Musonda.

Timu hizo zinatarajia kurudiana tena katika mchezo ujao ambayo utapigwa Desemba 20 uwanjani Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kabla ya mchezo huo kuanza, timu ya Yanga, imetangaza Kiungo wa kimataifa wa Ivory Coast, Zouzoua, ameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa klabu hiyo Novemba.

Pacome amenyakua tuzo hiyo kwa kuwapiku kiungo Mganda, Khalid Aucho na mshambuliaji chipukizi mzawa, Clement Mzize alioingia nao Fainali.

Kwa ushindi huo, Pacome atazawadiwa fedha sh. milioni 4 kutoka kwa wadhamini NIC mara tu atakaporejea kutoka Ghana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *