Twiga Stars yafuzu WAFCON 2024 nchini Morocco

Na Badrudin Yahaya

HATIMAYE timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’, imefuzu kucheza fainali zijazo za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake ‘WAFCON’ 2024 zitakazofanyika nchini Morocco.

Twiga Stars imekata tiketi hiyo kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2 dhidi ya Togo na kufikia rekodi iliyowekwa miaka 13 iliyopita ambapo ndio ilicheza fainali hizo kwa mara ya mwisho.

Katika mchezo wa marudiano uliomalizika saa chache zilizopita uwanjani Keegue nchini Togo, Stars ililala kwa mabao 2-0.

Hata hivyo, Stars imesonga mbele kutokana na mchezo wa awali uliopigwa jijini Dar es Salaam, kushinda mabao 3-0.

Ushindi huo, umepokelewa kwa hisia tofauti katika mitandao ya kijamii, kwa wadau mbalimbali wa soka kutoa pongezi zao.

Baadhi ya wadau hao ni Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kwa nyakati tofauti wakitoa pongezi zao.

Twiga Stars inaungana na timu ya soka ya Taifa ya Wanaume ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ambayo imefuzu kucheza fainali za AFCON 2024 ambazo zitafanyika nchini Ivory Coast.

Kikosi cha Twiga kiliundwa na baadhi ya nyota ambao wanacheza soka la kulipwa akiwemo Oppa Clement anayecheza Uturuki katika Klabu ya Besiktas na ambaye ndio alifunga mabao mawili katika mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam.

Wengine ni Diana Lucas anayecheza katika Klabu ya Ausfaz Assa Zag ya nchini Morocco, Enekia Kasonga anayecheza nchini Saudi Arabia katika Klabu ya Eastern Flames na Aisha Masaka anayecheza nchini Sweden katika Klabu ya BK Hacken.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *