Na Badrudin Yahaya
TIMU ya Yanga SC, imeondoka alfajiri ya leo jijini Dar es Salaam kwenda Ghana kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Medeama FC ya nchini humo wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mchezo huo wa hatua ya makundi, unatarajiwa kuchezwa Ijumaa kuanzia saa 1 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.
Yanga hadi sasa haijaonja ladha ya ushindi katika michuano hiyo kwani inashika mkia katika Kundi D ikiwa na alama 1 baada ya kutoka sare na Al Ahly na kufungwa ma CR Belouizdad.
Kinara wa kundi hilo ni Ahly yenye alama 4 ikifuatiwa na Medeama na Belouizdad zenye alama 3 kila moja.
Akizungumza kabla ya kuanza safari, Meneja Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Ally Kamwe, amesema ni mchezo mgumu kwao kutokana na uimara wa wapinzani wao.
” Ukiangalia kundi letu kila timu ilishinda mechi ya nyumbani kwake isipokuwa sisi tu ndio tulipata sare na Ahly ila tutakwenda kucheza mchezo huo kwa tahadhari kubwa ili tusije kupoteza na kujiweka katika mazingira magumu,” amesema Kamwe.
Hata hivyo, Kamwe amesema kutokana na maandalizi waliyofanya na morali iliyokuwepo kikosini wana imani watafanya vizuri katika mchezo huo.
Baada ya mchezo huo, Yanga itashuka tena uwanjani Desemba 16 kuumana na Mtibwa Sugar katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara.
Pia itarudiana na Medeama Desemba 20 katika mchezo utakaoanza kuchezwa saa 10 jioni uwanjani kwa Mkapa, Dar es Salaam.