Taifa Gas kuruhusiwa Kenya ni mwanzo wa uwekezaji baina yake na Tanzania?

Na Ezekiel Kamwaga

BBC Swahili

MIAKA miwili iliyopita, wakati wa ziara ya kwanza ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Kenya tangu awe Rais, mfanyabiashara mashuhuri wa Tanzania, Rostam Aziz, alilalamika hadharani kwenye mkutano wa wafanyabiashara kuhusu namna anavyofanyiwa urasimu asiwekeze kwenye mradi wa gesi nchini humo.

Hoja kubwa ya Rostam ilikuwa kwamba ingawa Tanzania na Kenya zilikuwa zinafanya biashara, ukweli ni kwamba hakukuwa na ulinganifu. Wakati huo, takwimu alizotoa Rostam zilionesha kwamba wakati Kenya ina kampuni zaidi ya 500 zinazofanya kazi Tanzania, kuna kampuni za Kitanzania zisizozidi 30 nchini Kenya.

Thamani ya biashara za Wakenya ilikuwa inazidi dola bilioni moja huku za Watanzania nchini hazikuwa zinazidi dola milioni 50.

Leo Rais William Ruto wa Kenya amezindua mradi wa kiwanda cha gesi ya kupikia wenye thamani ya zaidi ya dola milioni 130 wa kampuni ya Taifa Gas inayomilikiwa na Rostam. Baada ya vikwazo na urasimu mwingine uliodumu tangu mwaka 2017 – kwa mujibu wa maelezo ya mfanyabiashara huyo, ndoto yake ya kuhudumia soko la Kenya kwa gesi ya kupikia sasa inaelekea kutimia.

Nini kimebadilika kuhusu jambo hili tangu Rostam atoe kilio chake na je huu ni mwanzo mpya kwenye uhusiano wa kibiashara kati ya majirani hawa wawili?

Ziara ya Rais Samia mwaka 2021

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Octavian Mshiu, anaamini kwamba kilichotokea sasa kwa Taifa Gas kuruhusiwa kufanya uzalishaji wa gesi ya kupikia nchini Kenya ni matokeo ya ziara ya kwanza ya Rais Samia nchini Kenya.

Mshiu ambaye yuko Kenya kushuhudia uzinduzi wa mradi huo mkubwa kwenye eneo la Mombasa na ambaye alikuwepo Nairobi kwenye mkutano ambao Rostam alilalamika, amenieleza kwamba kuna ushahidi wa kutosha kwamba biashara imebadilika kati ya Kenya na Tanzania tangu ziara hiyo.

“Kulikuwa na changamoto nyingi za kibiashara kati ya Kenya na Tanzania wakati Rais Samia akiingia madarakani. Unakumbuka ilikuwa tumefikia wakati wa kufungiana mipaka, kuchomeana vifaranga na kutoaminiana. Rais Samia na Rais Uhuru Kenyatta kwanza na sasa Rais Ruto wamefanyia kazi vitu vingi.

“Ukitaka kujua tazama takwimu. Wakati Rais Samia akiingia madarakani mwaka 2021, thamani ya biashara za Tanzania kwenda Kenya ilikuwa wastani wa dola milioni 300 lakini sasa biashara imefikia zaidi ya dola bilioni 1.2 za Marekani. Hii ni takribani mara nne ya ilivyokuwa miaka miwili tu iliyopita,” alisema Mshiu.

Biashara ambazo Tanzania inafanya zaidi na Kenya kwa sasa ni za mazao ya chakula, makaa ya mawe, chai na madini. Kwa muda mrefu, wafanyabiashara wa Tanzania walikuwa na malalamiko kwamba walikuwa hawapewi vibali vya kuuza bidhaa zilizokamilika na badala yake wauze malighafi tu. Kwa hiyo, wakati kuuza mahindi Kenya ilikuwa rahisi, unga haikuwa rahisi.

Biashara na wafanyabiashara wa Kenya

Tanzania na Kenya ni nchi jirani zenye watu wanazoungumza lugha ya Kiswahili lakini wenye tabia na desturi tofauti kisiasa na kiuchumi. Baada ya Uhuru miaka 50 iliyopita, waasisi wa mataifa hayo waliamua kufuata njia tofauti kiutawala – Wakenya wakikumbatia siasa za kibepari huko Watanzania wakijikita kwenye ujamaa.

Matokeo yake ni kwamba kada ya watawala na wafanyabiashara nchini Kenya ina uhusiano wa karibu sana ilhali Tanzania kulikuwa na jitihada kubwa za kutofautisha siasa na biashara. Kwa maana hiyo, wanasiasa wa Kenya pia ni wafanyabiashara wakubwa au wana ushawishi mkubwa kwa wafanyabiashara.

Ni mahusiano hayo ya karibu baina ya biashara na siasa za Kenya ndiyo yaliyoelezwa kuwa kikwazo kikubwa kwa wafanyabiashara kutoka nchi nyingine za Afrika Mashariki kuweka mguu nchini humo. Kenya pia ndiyo taifa lenye uchumi mkubwa pia na matajiri wengi kuzidi jirani zake na hivyo ni vigumu kwa mfanyabiashara mwingine mkubwa kupenya kutoka kwenye mtandao huo.

Hata wakati Rostam akitoa malalamiko yake hadharani nchini Kenya, kulikuwa na hisia kwamba huenda alikuwa akipata taabu kukubaliwa kufanya biashara ya gesi ya kupikia kwa sababu ni biashara ambayo inashikiliwa na mmoja wa wafanyabiashara wenye ushawishi mkubwa kwenye siasa za Kenya. Hivyo, tatizo kubwa la wageni kushamiri kibiashara nchini humo halikuwa sheria na taratibu bali watu na maslahi yao ya kibiashara na kisiasa.

Ndiyo sababu, kuboreka kwa uhusiano baina ya Rais Samia na marais Uhuru kwanza na sasa Ruto kumeweza kufanikisha jambo hili pasipo kubadili sheria yoyote ya Kenya. Kuna uwezekano pia kwamba huenda Ruto anaweza kuwa Rais wa tofauti Kenya kwa sababu hatoki katika mojawapo ya familia maarufu za kisiasa na kibiashara ambazo zimeshikilia uchumi wa Kenya kwa takribani nusu karne sasa.

Mwanzo mpya?

Pasi na shaka, hatua hii ni mwanzo mzuri kwenye masuala ya uwekezaji baina ya nchi hizi mbili na eneo zima la Afrika Mashariki kwa ujumla. Rostam ana bahati pia kwamba uwekezaji wake huu unaendana na ahadi alizotoa Rais Ruto wakati akiomba kura kwa Wakenya.

Mojawapo ya ahadi kubwa za Ruto ilikuwa ni kupunguza gharama za maisha kwa Wakenya na uwepo wa Taifa Gas nchini Kenya unatarajiwa kupunguza gharama za gesi ya kupikia. Hii ni habari njema kwa Mama Lishe na majumbani ambako ina maana gharama za nishati hiyo muhimu itashuka. Hili ni kundi ambalo Ruto alilizungumzia zaidi kwenye kampeni zake.

Hatua inayofuata sasa ni kwa Tanzania nayo kuonyesha nia njema kwa kuruhusu uwekezaji kutoka Kenya katika eneo ambalo lilikuwa vigumu huko nyuma. Kuna taarifa za mazungumzo ya kuruhusu shirika la ndege la JamboJet la Kenya kuruhusiwa kufanya kazi zake Tanzania na labda hili liko mezani kwa sasa.

Katika malalamiko aliyotoa Rostam, ujumbe mkubwa zaidi ulikuwa kwamba ili kuleta maendeleo na mtangamano miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki, jambo kubwa zaidi ni kuruhusu biashara na uwekezaji miongoni mwa wananchi na wafanyabiashara. Pasipo biashara, muungano wa Afrika Mashariki utakuwa ndoto.

Kukubaliwa kwa mradi huu wa gesi ya kupikia ni hatua kubwa na inafungua mwanzo mpya kwa biashara baina ya nchi hizi mbili kwa sababu mbili kubwa; mosi ni ukubwa wa mwekezaji mwenyewe ambaye anatajwa kama mmoja wa matajiri wakubwa wa Tanzania na hivyo jambo lake litajulikana kwa wengi.

Pili ni ukweli kwamba kwa kukubaliwa Taifa Gas, watendaji wa Kenya na Tanzania sasa watapata ujumbe kwamba vikwazo kwa wawekezaji wageni havina maana tena katika Afrika Mashariki inayoanza kujengwa na viongozi wa sasa.

Ni uwekezaji wa mwekezaji mmoja lakini mwangwi wake utakuwa mkubwa na utafunua njia nyingi zaidi kwa wawekezaji wengine katika maeneo tofauti ya kiuchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *