GCLA yajivunia miaka miwili ya Rais Samia

  • Yapata jengo jipya la bilioni 8.14/-, mitambo ya bilioni 9.3/-
  • Yapima jumla ya sampuli na vielelezo 368,123

Na Daniel Mbega, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imeupongeza uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambayo ndani ya miaka miwili imeiwezesha Mamlaka hiyo kukamilisha ujenzi wa jengo lake la makao makuu jijini Dodoma.

Jengo hilo jipya limegharimu takriban Shs. bilioni 8.14 na ujenzi wake umechukua miezi 13 tu kukamilika.

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mbarouk Simbagungile Mafumiko, ametoa shukrani hizo Alhamisi, Novemba 30, 2023 wakati alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam katika mojawapo ya vikao kazi vya taasisi za umma vinavyoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Mbali ya mafanikio ya kupata jengo jipya, lakini katika kipindi hicho cha miaka miwili ya utawala wa Rais Samia mamlaka hiyo imefanikiwa kununua mitambo mipya ya kisasa, mikubwa kwa midogo, yenye thamani ya Shs. bilioni 9.3.

“Mheshimiwa Rais Samia ameiwezesha Mamlaka katika suala zima la uwekezaji kwenye Miundombinu ya Uchunguzi wa Kimaabara. Tumefanikiwa kupata jengo la Makao Makuu ya Mamlaka jijini Dodoma, lakini ujenzi wa majengo unaendelea,” anasema Dkt. Mafumiko.

Anaitaja miradi ya ujenzi inayoendelea kuwa ni ujenzi wa Ofisi na Maabara kwa ajili ya Ofisi ya Kanda ya Kusini mjini Mtwara, ambao ukikamilika utawezesha kusogeza huduma za Mamlaka kwa mikoa ya Kanda ya Kusini inayohusisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, sanjari na kuondoa gharama za pango kwa Mamlaka.

Mradi mwingine ni ujenzi wa Jengo la Ofisi Kanda ya Mashariki jijini Dar es Salaam ambao ukikamilika utaboresha mazingira ya kufanyia kazi na utoaji huduma kwa wananchi.

“Tunayo ofisi ambayo tumekuwa tukifanyia kazi kwa miaka mingi kabla ya kuhamia Dodoma, lakini eneo lile ni dogo kulinganisha na huduma tunazozitoa, hivyo tunahitaji kupata jengo kubwa hasa kwa kuzingatia kwamba ofisi ya Dar es Salaam ndiyo inayopokea kazi nyingi zikiwemo za kupitia Bandri ya Dar es Salaam,” anafafanua.

Anautaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa Ofisi na Maabara katika Ofisi ya Kanda ya Ziwa jijini Mwanza, ambayo inahudumia takriban mikoa saba ya Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Simiyu, Shinyanga na Kigoma.

Mradi huo, anasema, ukikamilika utawezesha kusogeza huduma za Mamlaka kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa na utaboresha mazingira ya kufanyia kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kuhusu mitambo na vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa kimaabara ambavyo Serikali ya Rais Samia imewezesha kupatikana, Dkt. Mafumiko anasema Mamlaka hiyo imenunua mitambo mikubwa nane (8) na midogo 134 yenye thamani ya Shs. bilioni 9.3, ambayo ilinunuliwa katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2021/2022 na 2022/2023.

Baadhi ya mitambo hiyo ni Gas Chromatography – Mass Spectrometer (GC-MS/MS) unaotumika kwa uchunguzi wa sampuli za mkojo na damu kubaini viwango vya viambata vya dawa za kulevya na sumu kwa wagonjwa walioathirika na dawa za kulevya, uchunguzi wa usalama na ubora wa dawa asili, virutubisho (Food Supplements), na tafiti mbalimbali.

Kuna mtambo wa kisasa ujulikanao kama Liquid Chromatography – Mass Spectrometer (LC-MS/MS) ambao unatumika kuchunguza sampuli za jinai, tiba asili, vyakula, virutubisho, tafiti za magonjwa, na usalama wa chanjo.

Mitambo mingine ni Inductively Coupled Plasma – Optical Emission Spectrometer (ICP-OES) na Atomic Absorption Spectrometer (AAS) ambayo inatumika kwa ajili ya uchunguzi wa maji tiba (dialysis water) yanayotumiwa kutibu wagonjwa wa figo pamoja na uchunguzi wa damu n mkojo kwa wafanyakazi wa migodini u viwandani kubaini viwango vya madini tembo (elephant ore) kwa wagonjwa walioathirika kutokana na mzingira ya kazi zao.

Aidha, mitambo mingine ni mashine ya Genetic Analyser 3500XL inayotumika katika uchunguzi wa sampuli za vinasaba vya binadamu (Deoxyribonucleic acid – DNA) kuhusiana na mashauri ya jinai, kijamii (Paternity) na wagonjwa wanaohitaji upndikizaji wa figo na utambuzi wa Jinsi iliyotawala (Sex identification) ilikuwezesha matibabu yakiwemo ya upasuaji.

Mtambo mwingine ni Cyanide Analyser unatumika kuchunguza sampuli za damu na mkojo kubaini uwepo wa sumu ya Cyanide kwa wagonjwa au wafanyakazi migodini walioathirika kutokana na mazingira ya kazi za migodini, pamoja na mtambo wa Mercury Analyser unaotumika katikauchunguzi wa sampuni za damu na mkojo kubaini viwango vya madini ya zebaki (Mercury) kwa wagonjwa au wafanyakazi wa migodini.

“Uwekezaji huu wa mitambo umesaidia kuimarisha shughuli za uchunguzi wa kimabara na udhibiti kwa lengo la kulinda afya za binadamu na mazingira,” anasema Dkt. Mafumiko.

Anaongeza kwamba, katika karne ya 21 ambayo Dunia inashuhudia ukuaji wa kasi katika sayansi na teknolojia, taasisi za kisayansi hazina budu kufanya uwekezaji wa mitambo ya kisasa kukidhi mahitaji hayo na akamshukuru Rais Samia kwa kuiwezesha Mamlaka kupata mitambo ya kisasa.

Uchunguzi wa umahiri hauwezi kuwa bora ikiwa hakutakuwa na rasilimali watu, tena wenye ujuzi na maarifa, hivyo, pamoja na uwekezaji huo wa majengo na mitambo ya kisasa, Mamlaka imewekeza katika mafunzo ya wataalamu ilikuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Dkt. Mafumiko anasema, katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, jumla ya watalaamu 28 walihudhuria mafunzo ya muda mrefu na watumishi 147 walihudhuria mafunzo ya muda mfupi ndani na nje ya nchi.

Aidha, watumishi 56 waliwezeshwa kuhudhuria mikutano ya kitaaluma na wengine 23 waliwezeshwa kupata mafunzo ya awali ya Utumishi ya Umma (Induction course).

“Kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023, watumishi 50, sawa na asilimia 114 ya lengo la kutoa mafunzo kwa watumishi 44, walihudhuria mafunzo ya muda mrefu ndani na nje ya nchi. Lakini watumishi 247, sawa na asilimia 123 ya lengo, walihudhuria mafunzo ya muda mfupi ndani na nje ya nchi,” anasema.

Huduma za Uchunguzi wa Kimaabara 

Dkt. Mafumiko anasema kwamba, Mamlaka imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutekeleza majukumu yake ya kisheria, hususan katika upimaji wa sampuli na vielelezo mbalimbali, ambapo ndani ya miaka miwili ya utawala wa Rais Samia, wamefanikiwa kupokea na kupima sampuli na vielelezo 368,123.

Anasema, kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 wastani wa sampuli na vielelezo 155,817 vilipokelewa na kufanyiwa uchunguzi, sawa na asilimia 139.94 ya lengo la wastani wa kuchunguza sampuli na vielelezo 111,349 kwa mwaka huo.

Aidha, kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023, sampuli 212,306 sawa na asilimia 133.9 ya lengo la kuchunguza sampuli 158,600 zilifanyiwa uchunguzi wa kimabaara.

“Haya ni mafanikio makubwa kwa Mamlaka na yote imefanikiwa kutokana na miundombinu wezeshi iliyopo, ambayo ni ya kisasa kabisa,” anasema.

Anasema, miundombinu bora iliyopo imefanya utekelezaji wa Mkataba wa Huduma kwa Mteja uwe na mafanikio hasa katika utoaji wa matokeo ya uchunguzi, ambayo yanatolewa kwa wakati.

Anafafanua kwamba, katika upimaji wa kubaini sumu kwenye sampuli wanatumia wastani wa siku 11 za kazi na katika uchunguzi wa kimaabara kwa sampuli za dawa za kulevya, mioto na milipuko, wanatumia siku 6.5 za kazi kukamilisha.

“Kwa uchunguzi wa kimaabara kwa sampuli za vinasaba vya binadamu tunatumia wastani wa siku 27 za kazi kutegemeana na aina ya sampuli, ingawa sampuli za mifupa ndizo huchukua siku nyingi, japokuwa haziwezi kuzidi siku 35 za kazi,” anasema.

Huduma za uchunguzi wa kimaabara zina umuhimu mkubwa kwa jamii kwa sababu matokeo yake ynaleta haki, Amani na utulivu wa nchi kwa kutoa ushahidi mahakamani kwenye mashauri yanayotokana na uchunguzi wake.

Lakini pia uchunguzi huo unasaidia kutatua migogoro kwenye jamii hususan uhalali wa wazazi kwa motto pamoja na masuala ya mirathi, unawezesha kupandikiza figo kwa wagonjwa kwa ushirikiano na Madaktari Bingwa, na unatambua ubora na usalama wa bidhaa za viwandani na kilimo kwa ajili ya kulinda afya ya jamii.

Usajili wa Wadau

Kwa mujibu wa Sheria, wadau wote wanaojishughulisha na biashara ya kemikali wanatakiwa wasajiliwe na Mamlaka.

Dkt. Mafumiko anasema, ndani ya kipindi cha miaka miwili wadau wanaojihusisha na biashara hiyo ya kemikali wameongezeka kutoka 2,125 mwaka 2020/2021 hadi 3,371 mwaka 2022/2023.

Aidha, kwa kuwa Mamlaka hiyo ndiyo yenye wajibu pia wa kusimamia na kudhibiti kemikali zinazoingia na kusafirishwa nchini, katika kipindi cha miaka mitatu jumla ya vibali 161,482 vilitolewa kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na kemikali.

Takwimu zinaonyesha kwamba, mwaka 2020/21 jumla ya vibali 40,270 vilitolewa, mwaka 2021/22 jumla ya vibali 55,780 vilitolewa na mwaka 2022/23 vibali 65,432 vilitolewa.

Dkt. Mafumiko anasema, Mamlaka imekuwa ikiwezesha ukuaji wa biashara ya kemikali za kimkakati ambazo ni Ammonium Nitrate inayotumika katika mambo mbalimbali ikiwemo vilipuzi kwenye migodi, Salfa inayotumika pia kuchenjulia shaba, na Sodium Cyanide inayotumika kuchenjulia dhahabu.

Kwa mwaka 2020/21 Ammonium Nitrate ilikuwa tani 65,526, Salfa ilikuwa tani 99,594, na Sodium Cyanide ilikuwa tani 23,533.

Katika mwaka 2021/22, Ammonium Nitrate ilikuwa tani 135,445, Salfa tani 396,982 na Sodium Cyanide ilikuwa tani 41,461.

Aidha, kwa mwaka 2022/23, Ammonium Nitrate ilikuwa tani 310,299.50, Salfa tani 1,018,136, na Sodium Cyanade ilikuwa tani 37,331.

Ongezeko la Mapato ya Ndani

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali inategemea mapato kutoka vyanzo mbalimbali ambavyo ni pamoja na Tozo na Faini mbalimbali, Mapato ya Usimamizi wa Sheria ya Kemikali, Mapato ya gharama za Uchunguzi wa Kimaabara, pamoja na Ruzuku kutoka Serikali Kuu (Revenue Grants) ambayo hutumika kwa ajili ya mishahara ya watumishi.

Mapato hayo yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na ufanisi wa utendaji kazi wa Mamlaka, ambapo kwa mwaka 2021/22 jumla ya mapato hayo yalikuwa Shs. 44,464,110,270 ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Kati ya hayo, Shs. 7,507,464,284.00 zilitokana na Tozo na Faini mbalimbali, Shs. 20,720,258,871.00 ni Mapato ya Usimamizi wa Sheria ya Kemikali, Shs. 11,110,620,466.00 ni Mapato ya gharama za Uchunguzi wa Kimaabara, na Ruzuku kutoka Serikali Kuu ilikuwa Shs. 5,125,766,649.00.

Kwa mwaka 2020/21 jumla ya mapato yalikuwa Shs. 31,126,776,216 ambapo Shs. 6,836,368,764.00 kati ya hizo ni Tozo na Faini mbalimbali, Shs. 13,728,918,689.00 zikiwa ni Mapato ya Usimamizi wa Sheria ya Kemikali, Shs. 5,737,012,796.00 ni Mapato ya gharama za Uchunguzi wa Kimaabara, na Shs. 4,824,475,967.00 ni Ruzuku kutoka Serikali Kuu.

Aidha, kwa mwaka 2019/20 mapato yalikuwa Shs. 26,059,314,506 kutokana na Mapato ya Usimamizi wa Sheria ya Kemikali (Shs. 17,177,811,852.57), Mapato ya gharama za Uchunguzi wa Kimaabara (Shs. 4,161,854,789.38) na Shs. 4,719,647,864 ni Ruzuku kutoka Serikali Kuu.

Ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia, Mamlaka hiyo imechangia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali jumla ya Shs. 2,289,500,000, ambapo kwa mwaka 2021/2022 ilishangia Shs. 1,374,500,000 na mwaka 2022/2023 ilichangia Shs. 915,000,000.00.

GCLA ilikotokea

Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ilianzishwa mwaka 1895 na utawala wa Wajerumani kwa lengo la kufanya utafiti wa magonjwa ya Ukanda wa Joto (Tropical Diseases).

Baada ya Uhuru, Maabara ilikuwa Idara ya Mkemia Mkuu wa Serikali chini ya Wizara ya Afya ikihusika na masuala mbalimbali yaliyohitaji uchunguzi wa kimaabara.

Mwaka 1999 ilibadilishwa na kuwa mojawapo ya Wakala za Serikali, ikiwa chini ya Katibu Mkuu Kiongozi – Ikulu.

Hata hivyo, mwaka 2017, Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Gazeti la Serikali 248 la tarehe 21/07/2017, ilitangazwa kuwa Mamlaka chini ya Sheria Namba 8 ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali iliyopitishwa na Bunge mwaka 2016.

Majukumu yake ni pamoja na uchunguzi wa kimaabara wa sampuli au vielelezo vya jinai, uchunguzi wa kimaabara wa sampuli zinazotokana na majanga, na utoaji wa ushahidi wa kitaalamu unaohusu uchunguzi wa kimaabara mahakamani.

Sampuli na vielelezo vingi vinavyoshulikiwa na Mamlaka hiyo vinahusu mashauri ya jinai kama dawa za kulevya, mauaji, ubakaji, ulawiti na ujangili wa wanyama pori.

Pia Mamlaka hiyo inahusika na sampuli na vielelezo vya mashauri ya madai kama vile uhalali wa wazazi kwa mtoto, utatuzi wa migogoro inayohusiana na mirathi.

Mipango ya baadaye

Dkt. Mafumiko anasema, mipango ya baadaye ni ujenzi wa miundombinu wezeshi ya utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka kwa kuendelea kusogeza huduma za Mamlaka kwa wananchi katika kanda na mikoa kulingana na uhitaji na uwezo, na kuendelea kununua mitambo na vifaa vya Maabara kwa ajili ya Maabara za Makao Makuu ya Mamlaka Dodoma pamoja na Ofisi za Kanda.

“Mpango mingine ni kuendelea kujenga na kutumia mifumo ya kielektroniki (Tehama) ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za Mamlaka, pamoja na kuimarisha huduma za uchunguzi wa kimaabara kwa kuendelea kununua mitambo ya kisasa inayoendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia za uchunguzi wa Maabara,” anasema Dkt. Mafumilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *