Na Rashid Abdallah
BBC Swahili
Baada ya uvumi wa hapa na pale, hatimaye jioni ya Jumatano, Novemba 29, 2023 ukweli ulibainishwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Godfrey Chongolo amejiuzulu nafasi yake baada ya kuitumikia kwa takribani miaka miwili na miezi kadhaa.
Katika siasa za chama cha CCM kujiuzulu kwa Katibu Mkuu sio jambo jipya. Aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho kwa miaka mingi Abdulrahman Kinana aliwasilisha barua ya kujiuzulu mwaka 2018 kwa mwenyekiti wa chama wa wakati huo Rais John Pombe Magufuli.
Ingawa kile ambacho hakifanani – ni zile sababu zinazomsukuma Katibu Mkuu mmoja na mwingine kuondoka katika nafasi yake. Lakini leo si siku ya kumjadili mkongwe wa siasa za Tanzania, Abdulrahman Kinana. Turudi kwa Chongolo.
Mazingira ya kujiuzulu kwake
Taarifa za kujiuzulu zilianza kusambaa kupitia barua iliyokuwa ikitembea katika mitandao ya kijamii siku kadhaa kabla ya Mwenyekiti wa CCM kuthibitisha kupokea barua ya Chongolo.
Gazeti la kila siku la Mwananchi limeripoti katika tovuti yake kwamba – barua hiyo imetaja kuchafuliwa katika mitandao ya kijamii kuwa ndiyo sababu ya yeye kujiuzulu. Na kuamua kuwajibika kama kiongozi kwa maslahi ya chama.
Katika taarifa iliyotolewa na chama chake jioni ya Novemba 29, 2023 inaeleza Chongolo aliwasilisha kweli barua ya kujiuzulu kwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Katika kikao cha kawaida cha Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kilichofanyika jijini Dar es Salaam siku ya Jumatano, Rais Samia alithibitisha kupokea barua ya kujiuzulu kwake, na aliridhia ombi hilo.
Majukumu ya Katibu Mkuu ni Yapi?
Nafasi ya Katibu Mkuu ni ya tatu kwa ukubwa katika mtiririko wa kiuongozi wa chama hicho chini ya Mwenyekiti wa CCM na Makamu wawili wa mwenyekiti. Kwa mujibu wa Katiba ya Chama chama Mapinduzi, kazi na majukumu ya Katibu Mkuu ni pamoja na:
Kuratibu kazi zote za chama, kusimamia kazi za utawala na uendeshaji katika chama, kuratibu na kufuatilia masuala ya usalama na maadili katika chama na kusimamia udhibiti wa fedha na mali za chama.
Chongolo aliteuliwa wakati ambapo Rais Samia akijaribu kufanya mabadiliko ya polepole ya sera katika siasa za Tanzania. Akitafuta kuziondoa baadhi ya sera za mtangulizi wake na kuweka za kwake kuhusu namna shughuli za kisiasa zinapaswa kuendeshwa.
Kwa kuzingatia hilo majukumu ya Chongolo pengine yalikuwa mepesi zaidi ukilinganisha na wakati wa mtangulizi wake Dkt. Bashiru Ally ambaye mbali na kazi zilizo ainishwa katika katiba ya chama – pia alikuwa na kazi ya kujibu tuhuma za mara kwa mara dhidi ya Mwenyekiti hayati Magufuli kuhusu kubana uhuru wa kisiasa, kuandamwa watu wa vyama vya upinzani, kuzuiwa mikutano na maandamano.
Safari yake Katika Siasa
Daniel Godfrey Chongolo alichukua nafasi hiyo April 2021 – baada ya kuachwa wazi na Dkt. Bashiru Ally, aliyeteuliwa na hayati John Pombe Magufuli Mei 2018 – alipomrithi Abdulrahman Kinana aliyehudumu kwa miaka saba.
Chongolo ni mtoto wa CCM kwa muda mrefu. Ni tofauti kidogo na Dkt. Bashiru Ally aliteuliwa wakati akiwa mhadhiri wa masuala ya siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hakuwa na mizizi ndani ya chama hicho.
Kabla ya nafasi ya ukatibu mkuu, Chongolo alikuwa mkuu wa Wilaya ya Kinondoni iliyopo katika mkoa wa Dar es salaam na kabla ya hapo, aliwahi kuhudumu kama mkuu wa Wilaya ya Longido mkoani Manyara.
Nafasi nyingine alizoshika ni ofisa wa CCM katika idara ya uenezi makao makuu ya chama Dodoma, wakati huo Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi akiwa Nappe Nauye ambaye kwa sasa ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Vilevile Chongolo amewahi kuwa mhariri wa Redio Uhuru inayorusha matangazo yake kutokea jiji la Dar es Salaam – ikimilikiwa na chama tawala. Pia kuhudumu katika bodi ya shirika la magazeti ya chama hicho ya Uhuru na Mzalendo.
Aliwekwa katika nafasi ya Katibu Mkuu baada ya Rais Samia kuamua kubadilisha safu ya uongozi wa juu wa chama hicho – kwani naibu katibu mkuu pia alibadilishwa kwa upande wa Tanzania bara na Katibu wa itikadi na uenezi vilevile alichaguliwa mtu mwingine.
Kipi kifuatacho?
Uamuzi wa kung’atuka unakuja nyuma ya miezi kadhaa kabla ya Tanzania kuingia katika chaguzi za serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025. CCM itahitaji Katibu Mkuu mwingine kabla ya chaguzi hizo kuanza
Alipoulizwa na BBC mchambuzi wa siasa kutoka Tanzania Mohammed Issa – kuhusu CCM inahitaji kuwa na Katibu Mkuu wa aina gani kuelekea uchaguzi wa 2024 na 2025. Anasema:
“Mabadiliko yanatoa nafasi kwa chama cha Mapinduzi kujipanga upya katika nafasi ya Katibu Mkuu. CCM ije na mtu ambaye atakiunganisha zaidi chama na kuwepo kwake kusiwe sababu ya kukigawa chama. Kumpata mtu wa namna hii manake umakini mkubwa unahitajika.”
Angalau kwa sasa yaonekana kuna uhuru wa kisiasa unaondelea, hivyo Katibu Mkuu ajaye atakuwa anaelewa kwamba majukwaa ya kisiasa ndio njia pekee ya kuzidisha ushawishi wa chama chake. Kwani zile zama za chama tawala kufanya shughuli za kisiasa kwa kujinafasi wakati vyama vyama upinzani havipati fursa hiyo zaonekana zimekwisha.