Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kimezindua utafiti kuhusu usalama wa wanahabari wanawake katika vyombo vya habari.
Utafiti huo ulifanywa kuanzia Julai-Septemba, 2023 ukihusisha vyombo vya habari katika mikoa 5 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumzia utafiti huo, Mkurugenzi wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben alisema uliangalia hali ya unyanyasaji wa kijinsia katika vyombo vya habari na unyanyasaji wa kingono, rushwa ya ngono katika vyombo vya habari.
“TAMWA kwa sauti kubwa tumekuwa tukikemea vitendo hivyo na ndiyo sababu kubwa ya kukosa waandishi wenye weledi, wanawake wa kutosha katika vyombo vya habari, na kukosa maudhui ya jinsia katika jamii,” alisema.
Alisema Tanzania imeridhia malengo endelevu ya dunia ambapo lengo la tano ndiyo mhimili wa malengo 17 linalohusu usawa wa jinsia.
Utafiti huo ulihusisha vyombo vya habari 22, wanahabari 137 kutoka mikoa mitano ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Mikoa hiyo ni Mwanza, Dodoma, Dar es Salaam, Morogoro na Arusha ambapo utafiti huo uliangalia unyanyansaji wa kijinsia unavyoathiri sekta ya habari.
Katika utafiti huo, asilimia 77 ya waliohojiwa walieleza unyanyasaji wa kijinsia katika vyombo vyao vya habari, asilimia 27 walitoa taarifa kupitia unyanyasaji kijinsia kutoka katika vyanzo vya habari.
Aasilimia 59 walitoa taarifa ya kupata unyanyasaji kutoka ndani ya vyombo vyao vya habari na kuthibitisha kutokea katika sekta ya habari.
“Unyanyasaji wa kijinsia na rushwa ya ngono huathiri sana mambo mbalimbali kwa viwango tofauti ikiwemo mienendo ya madaraka, maadili ya kitamaduni, shinikizo la uchumi na maslahi ya siasa,” alieleza.
Utafiti huo uligundua uwepo ya aina ya unyanyasaji wa kijinsia na rushwa ya ngono, unyanyasaji wa maneno hasa kwa wenye mamlaka ama katika vyombo vya habari wakihusishwa Mameneja, Wahariri, Wakurugenzi, wamiliki wa vyombo vya habari.
“Tulifikia mahali tunaona ni muhimu waandishi wa habari nao waangaliwe wanapoandika ya wengine ili wawe katika mazingira salama,” alisema.