Wanawake hutoa mimba kwenye kliniki zisizo rasmi kukwepa sheria

UTATA wa kisheria kuhusu utoaji mimba nchini Kenya unasukuma maelfu ya wanawake kurejea kwenye kliniki zisizo rasmi, BBC Africa Eye inachunguza jinsi utoaji mimba unavyogubikwa na unyanyapaa na habari potofu.

Edith amelazwa kwenye kitanda kilichofunikwa na gazeti la zamani katika zahanati ya mtaani Nairobi.

Miguu yake imeshikiliwa juu na vyuma huku mwanamume aliyevalia koti jeupe akieleza kuwa anakaribia kuweka dawa ndani ya mfuko wake wa uzazi. Ndoo nyekundu ya blichi iliyo na vyombo vya matibabu imewekwa sakafuni.

Mama huyo wa watoto watatu, ambaye jina lake limebadilishwa ili kulinda utambulisho wake, ana ujauzito wa miezi minne na anakaribia kutoa mimba.

“Nililazimika kuacha kazi kwasababu nililazimika kurejea kazini, na nina mtoto mwingine mdogo,” baadaye aliambia BBC Africa Eye.

Utoaji mimba ni suala gumu nchini Kenya.

Sheria ya adhabu, ambayo chimbuko lake ni enzi la ukoloni, inapinga utoaji mimba, kuhmtia hatiani mwanamke, na mtu anayetoa mimba na mtu anayetoa nyenzo zinazohitajika kutoa mimba.

Hata hivyo, katiba ya 2010, pamoja na chombo kikubwa cha sheria, huruhusu utoaji mimba wakati “maisha au afya ya mama viko hatarini” au wakati ujauzito umetokana na ubakaji.

Edith aligundua alikuwa na birusi vya HIV miaka michache iliyopita. Baada ya Mpenzi wake kukataa kupima, alimuacha.

Wakili mmoja aliiambia BBC kuwa kupata mtoto huku akiishi na virusi vya ukimwi kunamaanisha “hali yake ya kimwili huenda imo hatarini”. Hii, pamoja na mambo mengine, ilimaanisha kuwa Edith anaweza kuwa haki ya kutoa mimba kisheria.

Lakini alihisi kliniki ya mtaani ilikuwa chaguo lake pekee.

Ni madaktari wachache wanaotoa mimba kisheria ambao wako tayari kuzungumzia suala hilo kwa uwazi.

Kukamatwa kwa watu mashuhuri kwa miaka mingi kumefanya hali kuwa “hatari kwa wafanyakazi wa afya”, kulingana na Prof Joachim Osur, mtaala jijini wa afya ya uzazi na jinsia katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Amref huko Nairobi. Ni kuhusu jinsi sheria inavyoeleweka.

“Inategemea na jinsi jaji anavyotafsiri uhalali wa utaratibu ambao mtu ameufanya, hukumu inaweza kutolewa kwa njia moja au nyingine,” anasema.

Mnamo 2004, Dk John Nyamu, pamoja na wauguzi wawili, walikamatwa kwa mauaji ya watoto wawili wachanga, uhalifu ambao hukumu yake ilikuwa ni kifo.

Alizuiliwa katika Gereza leye ulinzi mkali la Kamiti jijini Nairobi kwa miezi 12 kabla ya kupatikana bila hatia.

Hisia za vyombo vya habari nchini Kenya kuhusu kesi yake hatimaye zilisababisha kuundwa kwa Muungano wa Haki za Afya ya Uzazi na Haki. Kundi hili ndilo lililoongoza mjadala wa kusaidia kutunga katiba ya 2010, ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo ilitoa njia halali, licha ya kwamba ina ukomo, ya kutoa mimba.

Hata hivyo, Dk Nyamu, ambaye kwa sasa anatoa utoaji huduma ya mimba kwa njia salama na halali, anaamini kuwa utata wa kisheria juu ya utoaji mimba hufanya iwe vigumu kwa wanawake kupata huduma hizi, hata pale wanapostahili kuruhusiwa na hasa katika vituo vya afya vya umma.

“Utoaji mimba usio salama umekithiri nchini Kenya,” anasema, akihoji kuwa wanawake masikini wanateseka zaidi kwani utoaji wa mimba salama haupatikani katika hospitali za umma kwa sababu ya kutokuwa na uhakika na ukosefu wa miongozo. utoaji mimba usio salama wanaoupata unaweza kusababisha matatizo ya kiafya.

“Wanaokuja na matatizo ya baada ya kutoa mimba, wengi wao ni vijana…. Wanawake hasa huanza [utaratibu] wenyewe, au wanafanya kwa usaidizi wa mtu ambaye hajapata mafunzo,” Dk Nyamu anaongeza.

Kulingana na shirika la kimataifa la haki za binadamu, Kituo cha Haki za Uzazi, karibu wanawake na wasichana saba hufariki kila siku nchini Kenya kwa sababu ya utoaji mimba usio salama. Maelfu zaidi wamelazwa hospitalini.

Katika kliniki isiyodhibitiwa viungani mwa jiji la Nairobi, mwanamume anayesimamia hutoa mimba kwa wanawake kwa shilingi 2,500 za Kenya.

“Tuna wasichana ambao bado wanasoma shule unapata wengine wanabakwa.

“Unapata mtu ambaye hayuko tayari, kupata mtoto. Sisi tunawasaidia kwa sababu wanakuja kuomba msaada. Wanahitaji msaada huo kutoka kwetu,” anasema, akizungumza kwa sharti la kutotajwa.

Anatoza ziada kwa ajili ya utupati salama wa kijusi. Ikiwa mwanamke hawezi kumudu hilo, hulipa mtu wa kukitupa kijusi mtoni.

Wanaharakati wa kupinga utoaji mimba na mashirika ya kidini nchini Kenya, wengi wao wakiungwa mkono na wanaharakati wa kupinga utoaji mimba nchini Marekani, wanasisitiza kuwa sheria iko wazi: utoaji mimba ni kinyume cha sheria.

Charles Kanjama, mwenyekiti wa Jukwaa la Wanataaluma wa Kikristo nchini Kenya, mara kwa mara huzungumza dhidi ya utoaji mimba na kuandaa mikutano jijini Nairobi.

“Kwetu sisi, hatufikirii kuwa kuna mkanganyiko wowote. Tunadhani [kanuni ya adhabu na katiba] zinalingana. Siungi mkono marekebisho ya sheria zetu ili kuondoa uhalifu wa kutoa mimba,” anasema.

Mnamo 2012, serikali ilichapisha miongozo kwa wafanyakazi wa afya kuhusu utoaji mimba halali. Mwaka mmoja baadaye waliondolewa, na mafunzo juu ya huduma salama wa utoaji mimba yalisitishwa.

Hiyo inasalia kuwa kesi na kundi la Bw Kanjama linataka ibaki hivyo.

“Msimamo wetu ni kwamba ikiwa utoaji mimba ni salama au si salama, kwanza mtoto hufa kila mara. Kwa hiyo, siku zote si salama kwa mtoto. Na la pili huwezi kuwafundisha watu kufanya jambo ambalo ni kinyume cha sheria nchini.”

Kuna sauti nyingi nchini Kenya ambazo hazikubaliani na utoaji mimba.

Mbunge Esther Passaris haungi mkono tu utoaji mimba lakini pia anashinikiza kuboreshwa kwa afya ya ngono na elimu ya upangaji uzazi.

“Katiba yetu inaruhusu utoaji mimba tu wakati usalama wa mama umo hatarini, na usalama sio tu wa kimwili na wa kibaolojia, ni wa kihisia na kiuchumi.

“Nadhani ni wakati muafaka kwamba tuelewe mzigo wa kihisia wa kutoweza kupata uzazi wa mpango, kutomuwezesha mwanamke kujua kwamba si lazima awe mashine ya kuzalisha watoto.”

Bi Passaris anasema huku katiba ya 2010 ilihalalisha utoaji mimba katika hali fulani, anasema kuwa hofu inayoizunguka kitendo hicho inazuia upatikanaji wa huduma za afya kwa wanawake, hasa kwa wale wanaotoka katika jamii maskini.

“Matajiri wana fursa ya kuwapeleka watoto wao katika hospitali za hadhi ya nyota tano na kutoa mimba kwa njia salama, kimya kimya, bila mtu kujua au kuzungumza. Lakini maskini wanapaswa kuhangaika,” anasema.

Mnamo Machi 2022, Mahakama Kuu ya Kenya ilithibitisha utoaji mimba kama haki ya kimsingi chini ya masharti ya katiba na iliamua kuwa kukamatwa kiholela ni kinyume cha sheria, lakini imefanya machache kuondoa hofu kwa baadhi ya wanawake, kama Edith.

Tukirejea katika kliniki ambapo anatafuta huduma ya kutolewa mimba mwanamume, ambaye anasema alifunzwa kama daktari na kutoa mimba takriban 150 kwa mwezi, amemaliza kumuwekea dawa ndani yake ili kutoa mimba.

“Tuna, kama, saa nne hadi tano kabla ya dawa kuanza kufanya kazi. Lakini baadaye, wakati dawa itakapoanza kufanya kazi , atapata uzoefu sawa na ule ambao mwanamke hupata wakati wa kujifungua,” anasema.

Edith alihifadhi shilingi 4,000 za Kenya kwa ajili ya kutoa mimba. Hazikutosha lakini zahanati ilikubali kufanya utaratibu huo kwa sharti kwamba angelipa pesa zilizosalia.

Wiki moja baada ya kutoa mimba, Edith anazungumza na BBC tena, akielezea uzoefu wake wa kutoa mimba kwa siri.

“Nilikuwa peke yangu na nikiwa na uchungu mwingi kiasi kwamba nilikuwa nikipiga kuta. Nilikuwa nikijiuliza ni nini kilikuwa kikiendelea, ikiwa hii ilikuwa ni kuzaliwa. Nilikuwa nikifikiria: ‘Sitaki kufa katika nyumba hii peke yangu.’

“Unafanya kwa uchungu, kwa sababu hukutarajia kitu kama hicho. Unawapenda watoto lakini ukizingatia maisha unayoishi, lazima ufanye hivyo.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *