Wafanyakazi wachunguzwe kubaini makosa yanayosababishwa na afya ya akili, uzembe

Na Kija Elias, Kilimanjaro

HIVI karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la watu wanaojidhuru kwa kujitoa uhai kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kimapenzi, msongo wa mawazo, ugumu wa maisha, malezi na makuzi.

Matukio kama hayo yamekuwa yakihusisha vifo vya kujiua au kujinyonga, mwanaume au mwanamke kuua mwenzi wake na wakati mwingine mzazi kuua watoto wake.

Mara kadhaa sababu za kufanya hivyo zimeelezwa ni wivu wa kimapenzi, ugumu wa maisha na msongo wa mawazo, ambapo mhusika huona hana suluhisho zaidi ya kujiua au kuua ama kuingia kwenye ulevi kupindukia akiamini ndilo suluhisho la tatizo linalomkabili.

Wataalamu wa magonjwa ya akili wanasema, hatua ya mtu kujidhuru au kumdhuru mwenzake kwa sababu yoyote ile, hutokana na tatizo la afya ya akili.

Hayo yamejiri Novemba 27, 2023 kwenye kikao cha Utekelezaji cha Baraza la Wafanyakazi, Idara ya Uhamaiaji (TUGHE) kilichofanyika katika Chuo cha Kikanda cha Uhamiaji Tanzania (TRITA) mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro, ambapo mtoa mada Dkt. Garvin Kweka kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, amesema Afya ya Akili ni tatizo linalomfanya mtu kuwa na hisia na hatua ya kufanya matendo tofauti yasiyotarajiwa kwenye jamii.

Dkt. Kweka amesema, unapomuona mtu anakunywa sumu, kujinyonga, kuwa mlevi kupindukia hiyo yote husababishwa na hisia zinazotokana na tatizo la afya ya akili.

“Asilimia kubwa kwa sasa ya wanaopatwa na tatizo la afya ya akili ni vijana na ikiwa hawatachukua hatua, huendelea kuteseka mpaka wanapokuwa watu wazima,” amesema Dkt. Kweka.

Takwimu za Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi zilizofanyika nchini mwaka 2022 zinaonesha Tanzania ina idadi ya watu 61,741,120, huku asilimia zaidi ya 40 ni vijana, huku Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema matatizo ya afya ya akili mara nyingi husababisha msongo wa mawazo, kujiua, unywaji pombe kupita kiasi na matumizi ya mihadarati.

Hayo yote husababisha vifo kwani ulevi kupindukia hufanya wakati mwingine mtu kuendesha gari hovyo na kupata ajali, lakini pia ulevi husababisha kufanya ngono isiyo salama hali inayoweza kuleta magonjwa ya kuambukiza na baadaye vifo.

Akizungumza katika Kikao cha Utekelezaji cha Baraza la Wafanyakazi, Idara ya Uhamiaji Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Miriam Mmbaga, amewataka wasimamizi wa wafanyakazi mahali pa kazi, kufanya uchunguzi wa kina kwa wafanyakazi wao wanapokiuka Kanuni, Taratibu na Sheria za Kazi kabla ya kutoa adhabu stahiki ili kubaini makosa yaliyofanyika kwani mengine husababishwa na Afya ya Akili au Uzembe.

“Lengo kuu la kikao hiki ni kujadili Robo ya pili ya bajeti ya mwaka 2023-2024, lakini katika mada ambazo zitakwenda kutolewa ni pamoja na changamoto ya afya ya akili ambapo pamekuwa na mienendo mbalimbali kwenye jamii na sehemu zetu za kazi, unakuta waasimamizi wa rasilimali watu huwa tunaenda moja kwa moja kwenye kuchukua hatua za kinidhamu,” amesema Mmbaga.

Amesema kutokana na tafiti ambazo zimefanywa na Wataalamu wa afya, wamegundua kuna mambo ambayo yamekuwa yakiwasumbua watumishi wa umma na watu wa kawaida ikiwemo afya ya akili, hivyo ni vizuri watu wakafahamu kwamba kwa sasa kuna shida kubwa ya afya ya akili kwenye jamii zetu hususani kwa watumishi wa umma.

“Tafiti zilizofanyika tumepata kusikia afya ya akili inasababishwa na msongo wa mawazo, malezi na makuzi na namna tunavyofanya mambo yetu na kusababisha watu kwenda kujiua ama kujinyonga,” amesema.

Mmbaga amesema unamkuta mfanyakazi anakuja kazini hakuna ambaye aliwaza kumshauri au kumsikiliza unamwagiza kufanya kazi hafanyi, lakini hakuna mtu ambaye amewahi kukaa na mtu huyo na kuzungumza naye, unamkuta pengine sio kawaida yake kuchelewa bila ya kukaa naye na kumsikikiza ni changamoto gani anayopitia msimamizi wa rasilimali watu anachkua hatua ya kumfukuza kazi au anamwandikia barua ya onyo kali.

Ameongeza kuwa mtu kama huyo anapatwa na msongo wa mawazo na anapofika nyumbani anakwenda kujinyonga anapoteza maisha na taifa linapoteza nguvu kazi kwa jambo ambalo lingeweza kufanyiwa kazi.

“Kupitia kikao hiki tumeona watumishi wetu kupitia Baraza hili wapate mada hiyo ya afya ya akili, ili watakapotoka hapa waende kuweka utaratibu wa kuwafikia watumishi wetu walioko mikoani ili waelewe tatizo hili lipo na namna ambayo wanaweza kujiepusha na matatizo kama haya.

Amesema Sekta ya Meneja ya Rasilimali Watu ni muhimu sana kwani ni sehemu za kazi, mtu huyu ni kiunganishi kati ya wafanyakazi na uongozi, karibu matukio mengi kwenye maofisi huwahusisha watu hawa kwa namna moja ama nyingine, jambo linalowalazimu kuwa karibu sana na wafanyakazi.

“Msongo wa mawazo, unywaji pombe kupindukia ni moja ya masuala yanayomhusu meneja rasilimali watu moja kwa moja endapo mmoja wa wafanyakazi wa taasisi yake atakuwa na tatizo hilo, ili kunusuru nguvu kazi ya kampuni,” amefafanua Mmbaga.

Ameongeza kuwa kumekuwa na utoaji wa adhabu kali kwa wafanyakazi pindi wanapokiuka Kanuni, Taratibu na Sheria za kazi pasipo kuchunguza kama ni  matatizo ya Afya ya Akili au ni kosa la uzembe, hatua ambayo imekuwa ikileta majanga mengi kwa baadhi ya wafanyakazi ikiwemo kujiua.

Mbali na hilo Mmbaga amewataka Wafanyakazi nchini kuanza maandalizi ya Kustaafu ikiwamo kuishi na jamii vizuri wangali bado makazini ili muda utakapofika wa kurudi uraiani wawe na mahusiano mazuri na jamii zao.

Kwa upande wake, Kamishna wa Uhamiaji wa Uraia na Hati za Kusafiria, Gerald Kihinga, amesema katika dunia inavyokwenda kuna ugumu wa maisha  ambao umekuwa ukichangia watu kuwa na afya ya akili, hivyo ni muhimu sana kwa Watumishi wa Umma kupata semina kama hii ili kuweza kujitambua na kuweza kuchukua hatua mapema kabla ya mambo hayajaharika.

“Kupitia semina hii watu wataweza wameanza kumbe inawezekana na mimi ninatatizo la afya ya akili, ninachukua hatua mapema kabla madhara hayajanikuta.

Kihinga amesema wamekuwa wakiona watu wanakuwa walevi kupita kiasi, wanafanya kazi chini ya kiwango, hata kazi hafanyi vizuri na wengine hufikia kiwango cha kujiua au kujinyonga.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres anashauri serikali kuona umuhimu wa kuwekeza katika afya, elimu na jamii katika kudhibiti janga hilo ili kuhakikisha ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo haimuachi mtu nyuma ikiwemo vijana wenye matatizo ya afya ya akili ambao wakati mwingine hunyanyapaliwa na kukosa msaada kutokana na hali yao.

Kikao cha Baraza la Wafanyakazi, Idara ya Uhamiaji kinawajumuisha Menejimenti ya Idara ya Uhamiaji Makao Makuu, ngazi za mikoa, watumishi wasio watumishi wa umma kutoka Tanzania Bara na Vizsiwani kwa lengo la kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Idara ya Uhamiaji kwa bajeti ya mwaka 2023-2024, pamoja na kupokea changamoto kwenye sekta ya uhamiaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *