Na Eckland Mwaffisi, Dar es Salaam
KATIKA kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali ya Awamu ya Sita imetoa sh. trilioni 2.39 ili kutekeleza miradi ya usambazaji umeme vijijini.
Fedha hizo zimeongeza kasi ya maendeleo na ukuaji uchumi kwa wananchi wa vijijini, kuboresha huduma za kijamii, gharama ya kuunganisha umeme ni sh. 27,000.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mhandisi Jones Olotu (pichani), aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika kikao kazi kati ya taasisi hiyo na Wahariri wa vyombo vya habari nchini.
Kikao hicho ni mwendelezo wa vikao vinavyoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kuyapa nafasi Mashirika na taasisi za umma zilizopo chini ya ofisi hiyo kuelezea majukumu yao, changamoto na mafanikio.
Alisema Rais Dkt. Samia ni shujaa wa mafanikio makubwa ambayo REA imeyapata kupitia majukumu waliyonayo ya usambazaji nishati ya umeme vijijini katika mikoa mbalimbali Tanzania Bara.
“Kuna miradi mingi ya usambazaji umeme vijijini ambayo inaendelea kutekelezwa, ifikapo Juni, 2024, vijiji vyote Tanzania Bara vitakuwa na umeme na ifikapo 2030 vitongoji vyote vitakuwa na umeme,” alisema.
Alieleza kuwa, umeme unaosambazwa vijijini utasaidia kuhamasisha shughuli za uzalishaji, uanzishwaji viwanda vidogo, vya kati, biashara ili kuchochea uchumi wa vijiji.
Mhandisi Olotu alifafanua kuwa, walengwa wa miradi ya REA ni wananchi waishio vijijini ambao ni asilimia 75 ya wananchi wote Tanzania Bara wanaofikia 59,851,347.
Miradi inayotekelezwa na REA ni kuongeza wigo wa Gridi ya Taifa katika vijiji, vitongoji vyote nchini ili kufikisha huduma kwa wananchi wengi vijijini.
Pia kuna miradi ya nje ya gridi inayojumuisha mifumo midogo ya kuzalisha na kusambaza umeme katika maeneo yenye vyanzo vya nishati Jadidifu.
Alitoa ufafanuzi wa miradi hiyo ni pamoja na kufunga mifumo ya umeme jua katika taasisi za serikali, maeneo ya huduma za jamii zilizopo vijijini.
Pia kusambaza nishati safi na salama ya kupitia, REA imewezesha ujenzi wa mitambo ya biogesi majumbani, kwenye taasisi za elimu, kambi za jeshi, magereza.
Mradi wa Kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa pili, unahusisha kupeleka umeme kwenye vijiji 4,071 vilivyobaki kati ya vijiji vyote 12,318.
Pia kujenga njia za umeme wa msongo wa kati zenye urefu wa kilomita 23,526, kujenga njia za umeme wa msongo mdogo urefu wa kilomita 12,159, kufunga mashineumba 4,071, kuunganisha wateja wa awali wapatao 258,660.
Mradi huo unafadhiliwa na serikali ya Tanzania ikishirikiana na Benki ya Dunia kwa gharama ya sh. trilioni 1.58, unatarajiwa kukamilika Desemba, 2023.