Na Eckland Mwaffisi, Dar es Salaam
UKIMYA wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan juu ya hatua alizoahidi kuzichukua dhidi ya vigogo ambao wametajwa kuhusika na ubadhirifu, uzembe katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Heabu za Serikali (CAG), umeendelea kuwatesa baadhi ya vigogo.
Sababu kubwa inayowatesa vigogo hao ni aina ya utendaji kazi wa Rais Dkt. Samia na mfumo wake wa kuchukua hatua dhidi ya viongozi na watendaji wanaoshindwa kuendana na kasi yake.
Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, Rais Dkt. Samia amekuwa akifanya maamuzi kwa mfumo usiotabirika.
Hali hiyo inawafanya wateule wake kutoelewa ni wakati gani Rais Dkt. Samia atafanya maamuzi magumu.
Mara kadhaa, Rais Dkt. Samia amewataka wasaidizi wake wafanye kazi kwa weledi, kuzingatia misingi ya utawala bora na sheria, kutanguliza uzalendo.
Rais Dkt. Samea amekuwa akiwataka viongozi kufanya kazi kwa kuzingatia mipango, sheria, miongozo na Dira ya Maendeleo ya nchi ili kukuza ustawi wa Taifa.
Pia kusimamia na kutekeleza majukumu waliyopangiwa kikamilifu kwa kushirikiana, kuheshimiana, kuzingatia viapo vyao lakini baadhi ya viongozi wanaonekana kwenda kinyume na maagizo ya Rais Dkt. Samia.
Pamoja na wito wake kwa baadhi ya watendaji kuacha kugombana wenyewe kwa wenyewe, taarifa za ndani zinasema baadhi yao wanaendeleza malumbano hayo kimyakimya hivyo kukwamisha maendeleo.
Changamoto nyingine ni baadhi ya watendaji kuendelea kufanya kazi kwa mazoea jambo ambalo linamkera Rais Dkt. Samia, huenda akafanya maamuzi magumu ili kuboresha safu ya uongozi katika serikali yake.
Msisitizo mkubwa wa Rais Dkt. Samia kwa viongozi ni kutambua kuwa, Serikali anayoiongoza imedhamiria kukuza uchumi wa nchi na ustawi wa jamii.
Ili kufikia azma hiyo ni wajibu kila kiongozi kwenye kila sekta kutekeleza wajibu na majukumu yake ipasavyo.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Leo, umebaini wapo baadhi ya watendaji ambao uwajibikaji wao umepungua wakihofia kutubuliwa katika nafasi zao kutokana na tuhuma mbalimbali zinazowakabili katika taasisi zao.
Agizo la Kamati Kuu ya CCM kuitaka serikali ichukue hatua dhidi ya vigogo waliotajwa kuhusika na ubadhirifu wa fedha za umma limeongeza joto kwa watendaji walioguswa katika ripoti hiyo.
Kamati Kuu iliielekeza Serikali kuchukua hatua dhidi ya wote waliohusika na ukiukwaji wa sheria, kusababisha ubadhilifu wa mali, rasilimali za nchi.
Joto hilo linapanda kutokana na kauli ya Rais Dkt. Samia kuwa kuna watendaji serikalini hawaendani na kasi yake hivyo kauli hiyo ni mwanzo wa mabadiliko makubwa ya viongozi serikalini ambayo Rais Dkt. Samia anatarajiwa kuyafanya wakati wowote.
Mbali ya vigogo waliotajwa katika ripoti hiyo wakiwemo wakuu wa taasisi na mashirika, wachambuzi wa masuala ya Siasa wanasema mabadiliko hayo pia yatawagusa viongozi ambao hawakutajwa katika ripoti hiyo lakini wameshindwa kwenda na kasi ya Rais Dkt. Samia.
Kwa mujibu wa wachambuzi hao, Rais Dkt. Samia anapoanza kuchukua hatua za kuwatumbua viongozi wasioendana na kasi yake, atakuwa amefungua njia kwa wateule wake hasa Mawaziri kuchukua hatua dhidi ya watendaji walioshindwa kuwajibika katika nafasi walizoaminiwa kuziongoza.
“Mabadiliko makubwa yanayotarajiwa kufanywa na Rais Dkt. Samia hayatawaacha baadhi ya watendaji wa taasisi za umma zilizo chini ya Wizara zinazoongozwa na Mawaziri.
Katika ripoti ya CAG, taasisi 14 za umma zimetajwa kuiingizia Serikali hasara jambo lililomfanya Rais Dkt. Samia kutaka ifanyike tathmini kama kuna haja ya mashirika hayo kuendelea kuwepo .
“Ipo changamoto kubwa ya baadhi ya viongozi ambao wameaminiwa na Rais kutotekeleza majukumu yao kwa kutanguliza maslahi yao badala ya nchi na uzalendo.
“Rais Dkt. Samia hawezi kukubali viongozi hao wamchafue yeye binafsi na chama anachokiongoza kama Mwenyekiti wao, ukimya wake una kishindo kikubwa, yajayo yanafurahisha.
“Naamini Rais Dkt. Samia anakamilisha mchakato wa kuwafuatilia watu wote wanaotumia dhamana zao za uongozi vibaya, kutotanguliza maslahi ya nchi, uzalendo mbele katika nafasi wanazotumikia,” alisema mchambuzi wa masuala ya Siasa ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alipozungumza na Tanzania Leo.
Alifafanua kuwa, maagizo ya CCM yanampa nguvu Rais Dkt. Samia, wakati akipokea ripoti alionyesha kukerwa na viongozi wanaofanya ‘madudu’ hasa upitishwaji mikataba mibovu inayoendelea kuigharimu nchi, kucheleweshwa malipo kunakozalisha riba kubwa kwa Serikali.
Alisema vyama vyote vya siasa kikiwemo CCM tayari vimeanza maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 hivyo Rais Dkt. Samia anataka kufanya kazi na watu ambao watakisaidia chama na serikali kutekeleza ahadi zote zilizopo kwenye Ilani kabla ya uchaguzi.
Aliongeza kuwa, anaamini mabadiliko makubwa ya viongozi yanayotarajiwa kufanywa na Rais Dkt. Samia yatazingatia viongozi wenye uwezo.
“Kuwajibishwa kwa viongozi kutokana na matokeo ya ripoti ya CAG ndicho kinachopaswa kufanywa ili kukomesha vitendo hivyo.
“Kama hatua hazitachukuliwa, ubadhirifu utaendelea kujirudia, wahusika wawajibishwe na kushtakiwa ili iwe fundisho kwa wengine,” aliongeza.