Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Hospitali ya Kigamboni inatoa huduma za tiba mkoba ijulikanayo Dkt, Samia Suluhu Hassan Outtreach Services kwa kufanya upimaji, matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo jirani.
Upimaji huo utafanyika kwa watoto na watu wazima kuanzia Novemba 27, 2023 hadi Desemba 2,2023 kuanzia saa mbili asubuhi hadi 10 jioni katika viwanja vya Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano JKCI, Anna Nkinda, alisema katika utoaji wa huduma kutakua na Madaktari Bingwa wa moyo ambao wataambatana na wataalamu watakaotoa elimu ya lishe bora itakayowapa wananchi uelewa wa kufuata mtindo bora wa maisha.
Alisema mtindo huo utawasaidia kuepuka magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo ambayo yanaweza kuepukika kwa kufuata ushauri wa kitaalamu.
“Tutafanya uchunguzi wa matatizo ya moyo na wote ambao watagundulika watapatiwa matibabu hapo hapo au kupewa rufaa ya kuja kutibiwa katika taasisi ya JKCA iliyopo Upanga, Dar es Salaam,” alisema.
Aliongeza kuwa, wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi kupima afya zao, kujua kama wana matatizo ya moyo ili kuanza matibabu mapema.