Na Daniel Mbega, Dar es Salaam
LEO Ijumaa, Novemba 24, 2023, wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanatarajiwa kuridhia kwa pamoja kukabidhiwa kwa kijiti cha uenyekiti kwa Rais wa Sudan Kusini, Salvatory Kiir Mayardit, akimrithi Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye.
Mkutano huo wa wakuu wa EAC unaofanyika kwenye makao makuu ya jumuiya hiyo jijini Arusha na ambao unahudhuriwa pia na Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, umekuwa na mafanikio makubwa katika nyanja nyingi, hususan kiuchumi, kidiplomasia, kijamii na kisiasa.
Na kwa hakika uamuzi wa kumpatia Rais Kiir uenyekiti, ambao ni kwa mujibu wa Katiba ya EAC inayoelekeza kijiti hicho kiwe kinazunguka, unaonyesha ukomavu wa demokrasia katika ukanda huo, licha ya kuwepo kwa migogoro ya ndani katika baadhi ya nchi wanachama.
Mkutano huo wa siku mbili unaofikia tamati leo, ulijadili pia suala la usalama wa chakula ndani ya jumuiya hiyo.
Lakini hii ni mara ya kwanza kwa Sudan Kusini kukabidhiwa uenyekiti wa EAC tangu ‘kuzaliwa’ kwa taifa hilo na miaka saba bada ya kujiunga ndani ya jumuiya.
Sudan Kusini ilijiunga na EAC mwaka 2016, ikiwa mwanachama wa sita baada ya Kenya, Tanzania, Uganda, Burundi na Rwanda, na mwaka 2022 EAC ikapokea mwanachama wa saba, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Sudan Kusini ni taifa ambalo lilizaliwa mwaka 2011 kutoka ubavuni mwa Sudan, kufuatia migogoro ya muda mrefu pamoja na awamu mbili kuu za vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyochangia kuzaliwa kwa taifa hilo.
Salva Kiir anakabidhiwa uenyekiti wakati jumuiya hiyo ikiwa inakabiliwa na changamoto ya baadhi ya nchi wanachama kutolipa ada zao za uanachama kwa wakati, na mataifa yaliyokuwa yanaongoza kutolipa ni yenyewe Sudan Kusini na Burundi.
Hata hivyo, Sudan Kusini ilitangaza kukamilisha malipo ya malimbikizo ya madeni yake hivi karibuni, ambayo jumla ya Dola za Marekani 7 milioni (Sh17.528 bilioni) zikiwa zimebaki siku chache kutwaa uenyekiti wa jumuiya hiyo.
Suala la madeni ya wanachama ni mojawapo ya changamoto ambazo Salva Kiir anapaswa kulisimamia kuhakikisha wanachama walnalipa ada kwa wakati.
Jambo jingine ni kwamba, Kiir anatakiwa kuhakikisha amani inaendelea kuwepo kwa kuwa nchi za Afrika Mashariki, wakiwemo wanachama wawili, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Sudan Kusini yenyewe zinakabiliwa na vita.
Lakini pia nchi jirani zinazopakana na EAC kama vile Ethiopia, Somalia, Msumbiji zinakabiliwa na mapigano ya mara kwa mara, jambo linalohitaji usimamizi na mikakati ya kuhakikisha amani inakuwepo.
Aidha, ni muhimu Sudan Kusini ikaendelea kuondoa vikwazo vya watu kusafiri sambamba na kusafirisha bidhaa ndani ya jumuiya, ili kuongeza mwingiliano utakaokuza biashara na shughuli za kiuchumi.
Jambo muhimu sana ni kuhakikisha misingi ya kidemokrasia inaendele kulindwa kama ilivyokuwa Liberia, ambapo Rais George Weah amekubali kushindwa na anaondoka kwa amani. Hii inamaanisha kwamba chaguzi ziwe huru na haki ili amani isitiwe doa.
Kimsingi, Sudan Kusini wanapaswa waanze kujiweka sawa wenyewe ndani kwa sababu itaweza kuwa na ushawishi katika kuongoza wengine. Ndani ya taifa hilo kuna majibizano na sintofahamu kati ya Serikali na wapinzani au wale wanaoipinga Serikali.
Kwa kifupi, hta kama ni taifa changa, Sudan Kusini ina kazi kubwa ya kuonyesha kwamba inaweza kuwa na ushawishi na kuweza kusukuma gurudumu la kidiplomasia katika nchi nyingine.
Ni muhimu Rais Kiir na watu wake waonyeshe uwezo. Bahati nzuri kuna kanuni na miongozo ya uendeshaji wa jumuiya, ziko wazi. Lakini uwepo wa kanuni peke yake hautoshi, lazima waje kuonyesha kitu kipya ambacho wengine hawakufanya.
Alikotokea Salva Kiir Mayardit
Salva Kiir Mayardit, ndiye Rais ya Kwanza ya Sudan Kusini. Amekuwa Rais wa nchi hiyo tangu mwaka 2011, wakati Sudan Kusini ilipopata uhuru kutoka Sudan. Kabla ya uhuru, Kiir alikuwa Makamu wa Rais wa Kwanza wa nchi ya Sudan na Rais wa eneo la Kusini la Sudan.
Alizaliwa Septemba 13, 1951 katika mji wa Gogrial, nchini Sudan akitokea katika kabila la Wadinka. Baba yake Kiir alikuwa mchungaji wa ng’ombe na mama alikuwa mkulima. Kiir alikuwa mmoja wa watoto tisa. Sasa, ana wake wawili na watoto wawili, wote wasichana, ambao ni Mary Ayen Mayardit na Aluel William Nyuon Bany.
Tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan, Kiir ametegemeza harakati ya uhuru kwa Sudan Kusini. Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya kwanza, Kiir alipigana katika kikundi cha Anyanya, ambacho kilitaka uhuru kwa Sudan Kusini. Halafu, wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya pili, Kiir alipigana akiwa na Sudan People’s Liberation Army (SPLA), na hatimaye, alikuwa kiongozi wa jeshi hilo hasa baada ya kifo ch kiongozi wa kwanza, John Garang, mwaka 2005.
Baada ya kifo cha Makamu wa Rais wa Sudan, John Garang, mwaka 2005, Kiir alichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Kwanza wa Sudan na Rais ya Sudan Kusini.
Katika uchaguzi wa mwaka 2010 wa Sudan, Kiir alishinda tena. Alipata asilimia 93 ya kura, na nchi nyingi za kidemokrasia zilishutumu uchaguzi huo. Hata hivyo, ushindi mkubwa wa Kiir ulikuwa muhimu sana kwa uhuru wa Sudan Kusini mwaka 2011.
Mnamo Januari 2011, watu wa Sudan Kusini walipiga kura kujitenga kutoka Sudan kwa sababu ya migogoro kati ya kaskazini na kusini ya Sudan.
Watu wengi wa Sudan Kusini ni Wakristo, na watu katika kaskazini na serikali ya Sudan ni Waislamu, kwa hiyo watu wa kusini walihisi wanakandamizwa. Mwaka 2011, asilimia 99 ya watu wa Sudan Kusini walitaka kuondoka.
Wakati Sudan Kusini ilipopata uhuru kutoka kaskazini, Kiir alikuwa Rais ya Kwanza ya Jamhuri ya Sudan Kusini, kwani alishinda uchaguzi mwaka uliotangulia.
Mara baada ya kuingia madaraka hasa kuzaliwa kwa Sudan Kusini, Kiir alianza urais wake kwa kusamehe watu ambao waliipinga SPLM. Lakini aliwafukuza baadhi yao kwenye Baraza lake la Mawaziri, akiwemo Makamu wa Rais wake, Riek Machar. Pia, alifukuza majenerali wa jeshi 117. Watu wengi, akiwemo Machar, wanasema kwamba hii lilikuwa jaribio la Kiir kuwa na nguvu zaidi.
Kiir anatajwa kutokuwa na uhusiano mzuri na wanahabari, kwani aliwahi kuwatishia waandishi wa habari ambao waliandika vitu vibaya dhidi yake.
Itakumbukwa kwamba, mwaka 2015, Kiir alisema waandishi wa habari hawapaswi kufanya kazi nchini mwake au dhidi ya nchi wake, na kwamba ataonyesha kwamba nchi yake inaweza kuua watu. Mwaka huo huo, waandishi wa habari sita waliuawa.
Lakini Kiir ana msimamo thabiti wa kupinga ushoga, ambapo waliwahi kukaririwa akisema ushoga ni “ugonjwa wa ubongo” na akaonya kwamba kama nchi za Magharibi zikijaribu kuleta ushoga mpaka Sudan Kusini, watu hawatakubali.
Mapigano na Riek Machar
Tangu mwaka 2013, kumekuwa na migogoro ya kisiasa katika Sudan Kusini kati ya Kiir na wapinzani wake. Baada ya Kiir kumfukuza Makamu wa Rais wake, Riek Machar, Machar alianza kupambana dhidi ya serikali ya Kiir.
Mnamo Desemba 2013, baada ya mkutano kati ya Kiir na Machar, kulisikika risasi nyumbani kwa Rais Kiir. Kiir alisema kwamba hii ilikuwa jaribio la Machar kupindua serikali yake.
Ingawa Machar alikanusha hili, tukio hili likaanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan Kusini. Machar alisema alipanga kushinda uchaguzi wa 2015. Leo, Kiir na Machar bado wanapigana kwa nguvu. Pia, mapigano kati ya Kiir na Machar ni matokeo ya tofauti ya makabila.
Wengi wanajiuliza, je, EAC itegemee nini chini ya uenyekiti wa Kiir ambaye mwenyewe bado ana chngamoto lukuki? Tusubiri tuone.