Mzozo wa mafuta Kenya na Uganda una athari kwa EAC

Na Daniel Mbega, Dar es Salaam

MKUTANO wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika umemalizika Alhamisi, Novemba 23, 2023 jijini Arusha, lakini kwa bahati mbaya hoja ya mzozo wa mafuta baina ya Kenya na Uganda haikuweza kujadiliwa.

Na haikuweza kujadiliwa kwa sababu haikupelekwa kuwa miongoni mwa agenda za mkutano huo.

Hata hivyo, kiuhalisia, mzozo huo unaweza kuwa na athari hasi kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa jitihada za makusudi hazitachukuliwa kuwaweka chini viongozi wa nchi hizo mbili.

Kuanzia mapema mwezi Novemba, kuliibuka mzozo mkali kuhusu usambazaji wa mafuta kati ya Kenya na jirani yake Uganda ambayo haina bandari, huku Rais wa Uganda Yoweri Museveni akisema nchi yake “inadanganywa” na “vimelea” na wafanyabiashara wanaohudumu kama ‘mawakala’.

Inafahamika kwamba, kwa miongo kadhaa, Kenya imekuwa ikiagiza mafuta kutoka nje na kuyauza kwa majirani zake wa Afrika Mashariki, hasa Uganda – lakini jukumu lake kama lango kuu la kusambaza mafuta katika eneo hilo sasa liko hatarini.

Mapema mwezi Novemba 2023 Rais Museveni alishutumu wafanyabiashara wa kati wa Kenya kwa kupandisha bei ya mafuta kwa hadi asilimia 58, na kusababisha “hasara kubwa” kwa nchi yake.

Pia alikashifu “vimelea vya ndani” kwa “kulaghai” Uganda kwa kushindwa kuingilia kati tangu bei ilipoanza kupanda mapema mwaka 2022.

Uganda kwa miaka mingi imeagiza 90% ya mafuta yake kutoka kwa makampuni ya uuzaji wa mafuta ya Kenya, ambayo huuza kwa kampuni zao tanzu za Uganda – yanayosalia hununuliwa kupitia Tanzania.

Kauli ya Museveni ilikuja huku Bunge la Uganda likiidhinisha uamuzi wa kusitisha biashara hiyo ambapo Serikali yake imeweka wazi kuwa inataka uhuru zaidi juu ya mikataba ya baadaye ya mafuta.

“Kenya kwa miongo kadhaa imeamua ni bidhaa gani za petroli Uganda itanunua, lini, wapi, kiasi gani, nani ananunua na kwa bei gani,” alielezea Waziri wa Nishati wa Uganda Ruth Nankabirwa.

Lakini kampuni za uuzaji wa mafuta nchini Kenya zimenyooshea kidole cha lawama kwa bei ya juu ya hivi majuzi kwa serikali ya Kenya.

Inaelezwa kwamba, hapo awali, mchakato wa kutoa zabuni na makampuni mbalimbali ya Kenya ulifanyika. Kampuni iliyoshinda zabuni ingeagiza mafuta kwa niaba ya wengine. Ilikuwa ni shughuli ya kulipa kadri uwezavyo iliyotekelezwa kwa Dola za Marekani.

Lakini mwezi Machi 2023, serikali ya Kenya iliingilia kati kwa sababu ya uhaba wa Dola za Marekani nchini humo, jambo ambalo lilisababisha matatizo kwa wafanyabiashara wote wanaoagiza bidhaa kutoka nje kwa vile benki zilikuwa zikitoa mgao wa dola.

Serikali ilijadiliana kwa upande mmoja kuhusu bei na makampuni ya kimataifa ya mafuta ili kusambaza mafuta kwa mkopo kwa soko la ndani na nje ya nchi.

Mpangilio huo unamaanisha malipo kwa wasambazaji wa kimataifa yanacheleweshwa kwa miezi sita.

Chini ya mpango huo, wateja wa ndani wa makampuni ya uuzaji wa mafuta ya Kenya hulipa bidhaa zao kwa shilingi za Kenya, lakini wale wa nchi jirani hulipa kwa dola.

Pesa zote huwekwa kwenye akaunti ya kupata riba kubwa kwa muda wa miezi sita kabla ya malipo kufanywa – na hivyo kupunguza mzigo wa uhaba wa dola.

John Njogu, Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wauzaji wa Mafuta nchini Kenya, anaelezea hii kama “laini ya mkopo” na anasema mpangilio kama huo unafanya mafuta kuwa ghali zaidi kwa wanunuzi.

Anasema, Uganda ilikuwa na haki ya kuikataa kwani haikuwa na tatizo la uhaba wa dola na haipaswi kutarajiwa kulipa zaidi.

Huku Uganda sasa ikijiondoa, Kenya sasa itapata tatizo lake la uhaba wa dola kukithiri zaidi – kwani Njogu anasema Uganda inalipa Dola milioni 180 kwa mwezi kwa makampuni ya Kenya kwa ajili ya mafuta.

Mkataba huo pia umekosolewa na kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga, ambaye aliutaja kama “ulaghai kubwa” – akipendekeza Wakenya wanalazimishwa kulipa bei ya juu huku wengine, zikiwemo baadhi ya kampuni za uuzaji wa mafuta, wakipata faida.

Anataka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi nchini Kenya (EACC) kuchunguza masharti ya mpango huo, ambayo alisema yanafaa kuwekwa hadharani.

“Watu wa kati anaowazungumzia Rais Museveni ni maafisa wa serikali ya Kenya,” anasema.

Lakini Waziri wa Nishati wa Kenya, Davis Chirchir, anatetea mpango huo wa mkopo, akiwaambia wabunge kwamba umesaidia kuwaepusha Wakenya kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta na mishtuko kutoka nje.

Bila hivyo bei inaweza kuwa kubwa zaidi, hasa kutokana na kushuka kwa thamani ya sarafu dhidi ya dola, alisema.

Vita hivi vya maneno vimeambatana na kashfa ya kutatanisha nchini Kenya kuhusu uagizaji wa tani 100,000 za mafuta yenye thamani ya Dola milioni 110 – ambayo umiliki wake umebishaniwa na kesi iko mahakamani.

Wakili wa mfanyabiashara huyo Mkenya anayehusika na madai kuwa alitekwa nyara kwa siku kadhaa na wale waliokuwa wakitaka “kuiba” shehena hiyo.

Serikali ya Kenya inakanusha kuhusika na imesema kampuni yake haina leseni.

Sio tu watumiaji wa Kenya na rais wa Uganda ambao hawana furaha. Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda na Sudan Kusini pia hupata kiasi kikubwa cha bidhaa zao za petroli kupitia Kenya.

“Kanda inanung’unika,” Dzombo Mbaru, Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya mafuta ya Kenya ya Mardin Energy, anasema.

Anasema sio mpango mpya pekee ambao una makosa, akipendekeza ushuru wa Kenya unaotozwa kwa bidhaa zote za petroli unaweza kuwa sababu na unahitaji “mapitio muhimu”.

“Eneo hili halijalala na limeunganisha miradi ya miundombinu ili kudhibiti udhibiti wetu. Lina chaguzi na baada ya muda Kenya itapoteza mengi,” Mbaru anaonya.

Tayari Uganda imesema imefikia makubaliano na kampuni ya Vitol Bahrain kufadhili hatua ya Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda kutafuta na kusambaza mafuta. Pia imetangaza kuwa itaweka akiba yake ya mafuta nchini Tanzania.

Mbaru ansema, miundombinu nchini Tanzania haijaendelezwa kama ilivyo nchini Kenya, lakini kwa ushirikiano mpya hili linaweza kubadilika.

Hapa ndipo panapozua maswali na kuleta hofu, kwani upo uwezekano wa Kenya kudhani Tanzania inahusika kushawishi Uganda ijitoe huko na badaka yake isafirishie mafuta yake kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

Kenya ni kama ‘mana wa kufikia’ ambaye siku zote ana lawama. Hata kama amefanya makosa, mwana wa kufikia anapoadhibiwa hudhani anaonewa kwa kuwa ‘anayemlea si mama yake mzazi’.

Huenda Uganda itakapoanza kuzalisha mafuta yake yenyewe hivi karibuni na kupanga kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta itaweza kutoa “bidhaa za petroli zenye ushindani, bila [gharama] zinazosababishwa na wafanyabiashara wa kati” ndani ya miaka michache kwa Afrika Mashariki.

Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema, hatua ya Uganda ni mwamko unaohitajika kwa tasnia ya uagizaji mafuta nchini Kenya, kwamba unahitajika mpango bora zaidi katika kuwa washindani na kuwa na weledi katika kupata biashara.

Lakini ni somo chungu ambalo litaathiri sana uchumi wa Kenya kwa siku zijazo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *