Na DW
VIONGOZI mbalimbali duniani wamepongeza makubaliano ya kubadilishana mateka kati ya Israel na Hamas.
Makubaliano hayo yatasababisha kuachiliwa kwa baadhi ya mateka wa Israel huku mapigano yakisimamishwa kwa muda wa siku nne.
Kwa mujibu wa taarifa ya Israel, mateka 50 wa nchi hiyo waliotekwa na kundi la wanamgambo wa Hamas wakati wa mashambulizi ya kigaidi ya Oktoba 7 wataachiliwa.
Mateka wote watakaoachiliwa ni wanawake na watoto.
Kwa upande wa Hamas, wamesema Israel itawaachilia wanawake na watoto wa Kipalestina 150 wanaoshikiliwa katika jela za Israel.
Makubaliano hayo pia yanajumuisha kusitisha mapigano kwa siku nne.
Israel imesema itaongeza muda wa kusitisha mapigano kwa ziada ya siku moja kwa kila mateka 10 watakaoachiliwa na Hamas.
Hata hivyo, kabla ya kuidhinishwa kwa makubaliano hayo, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesisitiza kwamba kusitisha mapigano hakutamaanisha mwisho wa vita dhidi ya kundi la Hamas.
Naye Rais wa Marekani Joe Biden, amesema ameyapokea vyema makubaliano ambayo yatafanikisha kuachiliwa kwa mateka waliochukuliwa na Hamas wakati wa mashambulizi ya kigaidi ya Oktoba 7 dhidi ya Israel, na ameongeza kuwa mateka wa Marekani watakuwa miongoni mwa watakaoachiliwa.
Rais huyo wa Marekani alizishukuru Misri na Qatar kwa kusaidia katika upatanishi kati ya Israel na kundi la Hamas.
Waziri Mkuu wa Qatar Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani, amesema anatumai mpango huo wa kubadilishana watu waliotekwa nyara utawezesha kufikiwa mchakato wa amani katika Ukanda wa Gaza.
Rais Mahmud Abbas na uongozi wa Mamlaka ya Palestina wamesema wamependezwa na makubaliano yaliyofikiwa na amesema wapalestina wanathamini juhudi za usuluhishi zilizofanywa na Qatar na Misri.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock ameungana na viongozi wa dunia katika kukaribisha hatua ya kufikiwa makubaliano kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas.
Amesema hayo ni mafanikio makubwa na amehimiza juu ya kutumia kipindi chakusimamishwa mapigano kupeleka msaada muhimu kwa watu wa Gaza.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula Von Der Leyen, amesema aliiamuru Tume yake ya Ulaya kuongeza upelekaji wa misaada huko Gaza kufuatia tangazo la kusitishwa mapigano kwa siku nne