Inonga, Kapombe wachuana Tuzo za Simba
WACHEZAJI nyota watatu wa Klabu ya Simba, wamechaguliwa kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora ya Februari inayopigiwa kura na mashabiki wao.
Wachezaji hao ni Henock Inonga, Shomari Kapombe na Mzamiru Yassin ambao kwa nyakati tofauti wameonesha ubora wao ndani ya mwezi huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na klabu hiyo Dar es Salaam jana, iliwataja nyota hao na kuwataka mashabiki kuingia katika tovuti ya klabu hiyo ili kumchagua wanayeona alifanya vizuri zaidi.
Katika hatua nyingine, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msingwa, mwishoni mwa wiki alikabidhi sh. milioni 5 kwa klabu hiyo ikiwa ni motisha kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akitekeleza ahadi yake.
Dkt. Samia alitoa ahadi ya kutoa sh. milioni 5 kwa kila bao litakalofungwa na wawakilishi wa nchi, timu za Simba na Yanga katika michuano ya kimataifa ya CAF.
Simba ilikabidhiwa kiasi hicho baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Vipers ya Uganda katika mchezo uliofanyika jijini Entebbe.
"Kama ambazo Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyoahidi, mkifunga nyumbani au ugenini kila bao atatoa sh. milioni 5 kama motisha, na hii ndio utekelezaji wake," alisema Msigwa huku akikabidhi fedha hizo kwa nahodha wa timu hiyo, John Bocco.
Akishukuru kwa niamba ya uongozi wa Simba, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Salim Abdallah 'Try Again', alimshukuru Rais. Dkt. Samia kwa kuonesha moyo mkubwa kwa kuwatia moyo ili kuhakikisha nchi yake inafanya vizuri katika soka.
"Si jambo dogo hasa likitoka kwa mama ni jambo kubwa kwetu, mpe salama na watahakikisha Vipers na Horoya wanalipa kisasi lakini pia hawatokubali kudhalilika tena kule (Raja Casablanca)," alisema kiongozi huyo.