NMB yazindua ugawaji mizinga ya nyuki Gairo

Na Mwandishi Wetu, Gairo

BENKI ya NMB imezindua Programu Endelevu ya Ugawaji Mizinga ya Nyuki 500 kwa vikundi 17 vyenye wafugaji zaidi ya 300, katika mikoa ya Morogoro, Tabora na Njombe kwa kushirikiana na Mamlaka ya Uhifadhi wa Misitu Tanzania (TFS).

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa programu hiyo uliyofanyika katika Msitu wa Msingisi – Gairo, Ofisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB, Alfred Shao, amesema kuwa, NMB imewezesha kutengeneza mizinga 500 ya kisasa kwaajili ya kuwagawia wafugaji nyuki katika mikoa ya Morogoro, Tabora na Njombe.

Amesema pia benki hiyo imetenga Sh. milioni 41 kwaajili ya kuwezesha mafunzo kwa wanufaika wa mizinga hiyo katika mradi wa kusapoti ufugaji wa nyuki.

“Nyuki ili wazaliane ni lazima misitu ilindwe na moja ya sababu ya NMB kutoa mizinga hii 500 ni juhudi za kulinda misitu yetu ikienda sambamba na upandaji miti ambapo mpaka sasa miti 750,000 tayari imepandwa nchini kwa kushirikiana na TFS na wananchi wanapata mazao ya misitu kwa kutunza mazingira,” amesema Shao.

Shao ameeleza zaidi kuwa katika mgao wa mizinga hiyo 500 Mkoa wa Morogoro umepata mizinga 200, Tabora 200 na Njombe 100 na kupitia NMB Foundation watatoa elimu kwa vikundi 17 vya ufugaji nyuki juu ya ufugaji nyuki wa kisasa, fedha na uvunaji wa asali ili asali itayovunwa iwe ya ubora wa kiwango cha juu cha kuuzwa nje ya nchi.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, ameipongeza Benki ya NMB kwa kuja na programu ambayo pia inaisadia serikali katika kuipa thamani zaidi Kampeni ya Achia Shoka, Kamata Mzinga na hivi karibuni. Serikali imeiingiza sekta ya asali na nyuki katika programu ya Kujenga Kesho Iliyo Bora kwa Vijana na Wanawake nchini (BBT).

Amesema juhudi hizi ni sehemu ya maandalizi ya Serikali kuelekea Mkutano Mkuu wa Wafugaji Nyuki Duniani utakaofanyika Tanzania mwaka 2027, ambao utawahusisha waataalum wakimataifa zaidi ya 4000.

Dkt. Abbas amesisitiza kuwa Tanzania ina mazingira mazuri ya uzalishaji wa mazao ya nyuki yenye kiwango cha juu cha ubora kutokana na uwepo wa misitu yenye mimea inayotoa chakula kwa nyuki huku sekta hiyo ikichangia ajira zaidi ya watu milioni 2 na kukadiriwa kuwa na uwezo wa uzalishaji wa asali tani 138,000 kwa mwaka.

Kamishna wa Uhifadi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, alisema Benki ya NMB imekuwa na ushirikiano nao katika utunzaji mazingira na upandaji miti tangu mwaka 2022 kupitia kampeni yao ya miti milioni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *