Na Mwandishi Wetu, Kigoma
CHAMA cha ACT-Wazalendo kimemshauri Wizara wa Maliasili na Utalii kusikiliza kero ambazo zinawakabili wananchi wa Kata ya Kagera Nkanda, Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma na kuzitatua.
Pia chama hicho kimeishauri Wizara hiyo kuwaondoa Maafisa wa Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS) katika wilaya hiyo.
Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe alitoa ushauri huo jana kwenye mkutano wa hadhara baada ya wananchi kuwalalamikia Maofisa wa taasisi hiyo kwa kushirikiana na viongozi wa Wilaya ya Kasulu wanaodaiwa kuwapora maeneo yao ya ardhi kwa madai ni sehemu ya hifadhi, kuyakodisha kwa ajili ya shughuli za kilimo.
“Kama ardhi imechukuliwa kwa matumizi ya hifadhi ibaki hivyo, kitendo cha kuwataka wananchi walipie hela kwa ajili ya kutumia ardhi hiyo ni ufisadi mkubwa.
“Mbaya zaidi fedha hizi zinaingia kwenye mifuko ya watu binafsi bila ya kutolewa risiti yoyote,” alisema.
Akizungumzia mipaka kati ya Pori la akiba la Kagera Nkanda na Mvinza Msitu wa Makere Kusini, Kabwe alisema mipaka ya mwaka 1956 ilitenganisha eneo la hifadhi na mipaka ya Kijiji lakini sasa hifadhi imeingia katika maeneo ya kijiji.
Alisema kilichotakiwa kufanyika ni kuongeza eneo la kijiji kwa sababu idadi ya watu iliyokuwepo wakati huo si idadi ya watu waliopo sasa, mahitaji ya ardhi yanaongezeka na siyo kupungua.
Kuhusiana na eneo la hekari 10,000 zilizotolewa kwa wananchi na Rais wa Awamu ya tano, Hayati Dkt. John Magufuli katika eneo la Kagera Nkanda, Kabwe alimtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jery Silaa kusimamia ahadi hiyo kwa kuhakikisha zinawanufaisha wananchi.
Mbali na kuwanufaisha wananchi, chama hicho kimetaka viongozi wote wa CCM, serikali waliohusika kukwamisha wananchi kutumia ardhi hiyo wachukuliwe hatua stahiki kwa sababu wamewafanya wananchi washindwe kutumia ardhi hiyo kujizalishia mahitaji mbalimbali ya kijamii
Kwa upande wake, Mhifadhi wa Wakala wa Misitu (TFS) kutoka Kigoma, Deograsian Kavishe, alisema TFS ndio inasimamia ya msitu wa Makere Kusini, miongoni mwa vijiji vinavyopakana na hiyo hifadhi ni Kagera Nkanda pamoja na Mvinza.
Alisema Kijiji cha Mvinza kuna maeneo ambayo walikuwa wanafanya kazi ambazo si za halali, haramu ndani ya hifadhi ambazo ni uchungaji mifugo na kilimo kwa kipindi kirefu wakiwa kama wavamizi.
Alifafanua kuwa, vimetengwa viunga mbalimbali kutoka kwenye eneo hilo, anayehitaji kutoka nje ya Kasulu na ndani anaweza kupangisha akafanya kilimo.
“Kuhusu hekta 10,000, hekta 2,374 wakapewa kijiji cha Mvinza, walitakiwa walipangie matumizi lakini wao wakaendelea kubaki kwenye maeneo mengine ambayo sekretarieti haikuyaainisha.
“Upande wa Kijiji cha Nkanda, walipata hekta 496 maana yake maeneo yaliyoenda kwenye hivyo vijiji wao ndio walikuwa na dhamana ya kuyapangia matumizi,” alisema.
Kavishe alisema, dhana ya wananchi wamenyang’anywa maeneo na kukodishiwa watu wengine si ya kweli.