Na Mwandishi Wetu, Singida
SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imekabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya sh. milioni 222.472, mkoani Singida.
Vifaa hivyo ni majenereta na vifaa vitakavyotumika kuhudumia watoto wanaozaliwa kabla ya muda, huduma nyinginezo vilivyokabidhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Kituo cha Afya Sepuka, Hospitali ya Wilaya ya Singida na Ilongero.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo ambayo ilishuhudiwa na wabunge, watendaji wa idara mbalimbali za sekta ya afya, wananchi na wanachama wa CCM, Meneja wa MSD Kanda ya Dodoma, Mwanashehe Jumaa, alisema kazi ya usambazaji vifaa hivyo ni jukumu lao walilopewa na Serikali.
“Kazi kubwa ya MSD ni kununua, kuzalisha, kuhifadhi na kusambaza bidhaa za afya na vitendanishi nchini ambayo tunaifanya kwa mamlaka ya kisheria,” alisema.
Jumaa alisema, MSD Kanda ya Dodoma imepokea maombi ya vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 700, pia kuna vifaa vya zaidi ya sh. milioni 700 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa ajili ya vituo vya afya na zahanati.
“Ukiangalia muda tuliopokea fedha hizi, utekelezaji wa kupeleka vifaa hivyo ni mfupi sana kutokana na serikali kuboresha huduma za MSD,” aliongeza.
Serikali imekuwa ikitoa fedha na MSD imekuwa ikinunua na kusambaza vifaa tiba katika hospitali na vituo vya afya kote nchini akisema hatua hiyo inajenga morali kwa watumishi wa sekta ya afya, kuipenda kazi yao.
Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu aliishuru Serikali na MSD kwa kupeleka vifaa hivyo na kueleza kuwa, sekta ya afya ni uhai, watu wakiwa na afya njema ndipo wataweza kufanya kazi zao vizuri.
Alisema kujenga majengo ya hospitali haitoshi bila kuwa na vifaa, madaktari, wataalamu wengine waliosomeshwa na serikali ili kutibu maradhi mbalimbali.
Mtaturu alisema Serikali ya Rais Dkt. Samia imefanya mapinduzi makubwa katika sekta ya afya hivyo kila mtu mpenda maendeleo anapaswa kumshukuru kwa jinsi anavyoiendesha nchi kwenye sekta mbalimbali.
Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu alisema miongoni mwa vifaa alivyo pokea kutoka MSD ni jenereta lenye ukubwa wa KVA 60 na vifaa vingine 11 ambavyo
baadhi ni toroli la kuwekea vifaa wakati madaktari na wauguzi wanapokwenda kutoa huduma.
Aliishukuru Serikali kwa kutoa fedha na kupongeza maboresho makubwa yaliyofanywa ndani ya MSD ambayo inaendeshwa kisasa, kuwa mkombozi kwa wananchi katika sekta ya afya.
Mbunge wa Singida Kaskazini, Ramadhani Ighondo, aliishukuru Serikali kwa kuwapelekea jenereta na gari la kubebea wagonjwa, wajawazito ambao wengi wao walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukosa umeme wa uhakika wakati wakipata huduma hasa za upasuaji, kukosekana kwa gari la kuwapeleka hospitali wanapokuwa wagonjwa.
Alisema pia Serikali kupitia MSD imewapelekea kifaa kinachotumika kwa ajili ya kuwaongezea joto watoto wanaozaliwa chini ya muda.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Dorisila Mlenga, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Singida, Grace Ntogwisangu na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Sepuka, Kesia Daniel waliishukuru Serikali kwa kuwapelekea vifaa hivyo ambavyo vinakwenda kuwarahisishia utendaji kazi wao wanapotoa huduma kwa wananchi.
Walisema watavisimamia na kuvitunza ili viweze kudumu muda mrefu kwani Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuvinunua.