Dkt. Mahera atoa agizo Vyuo vya Afya

Na Mwandishi Wetu, Tanga

NAIBU Katibu Mkuu-Afya, Dkt. Wilson Mahera, ameviagiza Vyuo vya Afya nchini ambavyo havina kozi ya Shahada ya Udaktari wa Kinywa na Meno kuianzisha ili kuongeza upatikanaji watalaamu wengi zaidi nchini.
Dkt Mahera aliyasema hayo jjana ijini Tanga wakati akifungua Mkutano wa Madaktari wa Kinywa na Meno Tanzania Kitaifa unaofanyika mkoani humo.

Alisema atafikisha ujumbe huo kwa wakuu wa vyuo hivyo nchini ili kungeza wataalamu wengi ambao watasaidia kutoa huduma kwa wananchi wenye changamoto mbalimbali za afya ya kinywa na meno.

“Kupitia mkutano huu, niviagize vyuo vya Afya nchini ambavyo havina kozi ya Shahada ya Udaktari wa Kinywa na Meno kuanzisha ili kusaidia kuongeza upatikanaji watalaamu hapa nchini,” alisema.

Mwaka 2022 kitaifa kulikuwa na wagonjwa wa kinywa 747,858, waliooza meno 522,777 sawa na asilimia 68.9 ya wagonjwa wote wa kinywa, meno na waliokuwa na matatizo ya fizi 78,755.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, tatizo la kuoza meno bado ni kubwa nchini ambapo wagonjwa  156,576 sawa na asilimia 30 waliooza meno, yalizibwa na wagonjwa 265,249 walioaza meno yaliny’olewa.
“Niwaombe wataalamu  mjikite kutibu na sio kuyang’oa maana Serikali imewekeza miundombinu yote wezeshi ya kuhakikisha wananchi wanapatiwa tiba ya meno na sio kung’oa jino,” alisema.

Hata hivyo, alisema kuna maeneo huduma za kinywa na meno hazipatikani hivyo wananchi hutembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya ya kinywa na meno.

Aliwataka wakuu wa mikoa na halmashauri, kuhakikisha vituo vya afya vya kimkakati na visivyo vya kimkakati vinaaza kutoa huduma ya matibabu ya kinywa na meno ili kuepusha wananchi kutembelea umbali mrefu.

Pia aliwataka  kuhakikisha wanakuwa na vifaa stahiki ikiwemo viti vya kutolea huduma na vifaa vya kisasa zikiwemo mashine za kufanyia uchunguzi wa afya ya kinywa, meno kulingana na miongozo inayotolewa.

Awali Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Japhet Simeo alisema Mkoa huo upo salama, aliwataka wajumbe kuhakikisha wanakuwa makini na vitu ambavyo vitawasilishwa kwenye mkutano huo.


Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Kinywa na Meno kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Baraka Nzobo, alisema kikao hicho cha kinywa na meno kwa madaktari kitasaidia kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekta hiyo.

Alisema tangu wameanza vikao hivyo, kila mwaka wameweza kuvifanya, sekta ya kinywa na meno imebebwa sana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa sababu Hospitali za Rufaa Kanda na Taifa, Wilaya, vituo vya afya ni vichache.

Alisema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI wamekuwa wakiratibu vikao hivyo na kuna baadhi yao hawatilii mkazo vikao vya maamuzi kwani huandikiwa barua lakini hawafiki.

“Nikuombe ikikupendeza uwachukulie hatua kwani maendeleo hayawezi kupatikana kama watu wanapuuzia vikao vya msingi vya kisekta ambavyo vinaleta mabadiliko ya kutoa huduma bora ya kinywa, meno.

“Ofisi hii iliziandikia halmashauri 36 kuleta wataalamu ngazi ya halmashauri lakini hadi leo wamefika 17, tunaomba ofisi yako ituulizie kwa wakurugenzi hao 18 kwanini hawajafika mahali hapa, wamekaidi,” alieleza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *